Mtikisiko mpya kidato cha 5&6

Wahitimu wa kidato cha nne katika shule moja ya sekondari nchini. Kwa sasa kuna wimbi kubwa la wahitimu hao kukacha masomo ya kidato cha tano, hata kwa wale wenye ufaulu mzuri na kwenda kujiunga na mafunzo vyuo vya kati. Picha Maktaba

Ni kupoteza muda. Hii ndiyo kauli iliyo kwenye midomo ya wahitimu wengi wa kidato cha nne walioamua kujiunga na vyuo vya kati, badala ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita, licha ya kuwa na ufaulu mzuri.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwapo kwa wimbi kubwa la wanafunzi wanaojaza fomu maalumu za kujiunga na vyuo ya kati badala ya kuchagua tahasusi katika ngazi ya kidato cha tano. Lakini pia wapo wanaochaguliwa kujiunga na ngazi hiyo ya elimu, lakini wanaikacha na kukimbilia vyuo vya kati.

Bhoke Edson aliyemaliza kidato cha nne mwaka 2021, ni mmoja kati ya wahitimu wengi wanaoamini kuwa kupita ngazi ya kidato cha tano na sita ni kupoteza muda.

Akiwa sasa mwanafunzi wa stashahada ya maendeleo ya jamii, anasema wakati unasoma kidato cha sita, mwenzako aliyejiunga na chuo kutoka kidato cha nne, anakuwa ameshahitimu astashahada na kuanza stashahada, huku akijihakikishia ajira akitolea mfano wa ndugu zake wawili.

“Nina kaka na dada yangu, kaka amehitimu shahada na dada amehitimu stashahada, lakini kwa sasa, dada ameajiriwa kaka bado yupo nyumbani ingawa alihitimu kabla ya dada,” anasema na kusisitiza kuwa idadi kubwa ya wanaoajiriwa ni wale wenye elimu ya stashahada na sio shahada anayoifananisha na sifa tu kwa mbele ya jamii lakini haina tija kwenye ajira.

“Nilivyoona hivyo nikasema sina sababu ya kupoteza muda mwingi miaka mitano yote hiyo, nikajiunga na chuo,” anasema.

Mwanafunzi mwingine aliyeamua kukacha kidato cha tano, Mussa Hassan anasema uamuzi huo ulimsababishia ugomvi na familia yake.

Anasema wazazi wake wanaamini katika elimu ya kidato cha tano na sita kisha shahada, lakini kwake ni tofauti.

“Niliingia kwenye mgogoro na familia yangu nilipotaka kujiunga na astashahada wakati nimefaulu vizuri kuendelea na kidato cha tano,” anasema.

Uamuzi wake huo, ulitokana na kile alichokifafanua kuwa, hakuna kitakachomsaidia kitaaluma katika ngazi ya kidato cha tano na sita, hivyo ni vema aanze astashahada ili ajenge umahiri.

“Unakwenda kidato cha tano unasoma vitu vilivyopo nje ya taaluma utakayokwenda kusoma chuoni. Mimi nilifanya uchunguzi wa kujua nini kinafundishwa huko, nilipoona hakuna jambo nikaona nisipoteze muda,” anaeleza mwanafunzi huyo katikati ya harakati zinazoendelea sasa za wadau wa elimu kutaka wanafunzi wa vyuo vya kati nao wafikiriwe kwenye mikopo..


Wanachosema wazazi

Haikuwa rahisi kwa wazazi kukubali uamuzi wa watoto wao, kama anavyosimulia mmoja wa wazazi, Muhsin Imlan.

Anasema kwa mara ya kwanza alidhani mwanawe ameanza kuchoka masomo, hivyo ilikuwa vigumu kumuelewa.

“Nikawa namwambia asipende njia fupi, kama Mungu amempa uwezo kafaulu hana sababu ya kuacha njia sahihi na kufuata mkato, aling’ang’ana akanielewesha nikamruhusu.

Tofauti iliyopo, anasema ni gharama za masomo akifafanua kuwa astashahada ada yake kubwa ukilinganisha na kidato cha tano na sita.

Lakini, anasema njia hiyo imemjengea msingi mzuri mwanawe tofauti kama angeanza kidato cha tano kisha cha sita.

“Kwa sasa anasoma stashahada tayari ni mtaalamu anaweza kufanya vitu vingi vya kitaaluma, angekuwa kidato cha sita maana yake muda huu asingeweza na angeenda shahada akiwa ndiyo kwanza mgeni wa taaluma yake,” anasema.

Mzazi mwingine, Nelson Mikosi anasema awali hakuruhusu hilo lifanyike kwa mwanawe, lakini baadaye alikuja kumuelewa hasa baada ya kuhitimu stahashada na kuanza kazi.

“Niligharimika na elimu yake ya astashahada na stashahada lakini mwenyewe ananiambia atakapojiunga na shahada atajigharimia mwenyewe,” anasema.


Walimu waguswa

Inaaminika kuwa elimu ya kidato cha tano na sita inakatisha ndoto za baadhi ya wanafunzi kama inavyofafanuliwa na Mwalimu Concheska Kilamba wa Shule ya Sekondari Sunshine ya Kibaha mkoani Pwani.

Mwalimu huyo anasema mwanafunzi anapofaulu kidato cha nne huchagua mchepuo atakaosoma kidato cha tano na sita.

Pamoja na uchaguzi huo na kufaulu mtihani wa kidato cha sita, anasema baadhi yao wanakosa nafasi za vyuo kutokana na ushindani wa kitaaluma.

“Mwanafunzi anachagua mchepuo wa sayansi akitamani kusomea udaktari atakapofika chuoni, kidato cha sita anafaulu kwa kupata daraja la pili.

“Anapofanya maombi kwenye vyuo vya udaktari anakosa nafasi kwa sababu ya ushindani, huwa wanachagua waliofaulu kwa daraja la kwanza tena la juu,” anasema.

Hali hiyo anasema inakatisha ndoto za kijana kwa upande mmoja, lakini inampotezea matumaini ya elimu kwa upande mwingine.

Si hivyo tu, anasema wengine huamua kukacha kidato cha tano na sita kwa kuwa kuna wakati wanachaguliwa kujiunga na ngazi hiyo ya elimu katika mchepuo tofauti na ule wa ndoto zao.

“Mfano anachaguliwa michepuo ya HKL, HGL, HGK n k lakini ndoto yake kubwa ni kusoma programu za afya, anaamua kupitia astashahada ili kufuata ndoto zake akiamini kidato cha tano na sita kutampotezea muda, lakini atasoma asichokipenda,” anasema na kushauri maboresho ili elimu ya kidato cha tano na sita ili imjengee mwanafunzi mazingira ya kuwa na uhakika wa kile anachokisomea.

Anapendekeza kuwepo mlinganyo wa ajira kwa ngazi ya stashahada na shahada ili kusiwepo na kundi linaloona lina nafasi zaidi ya lingine.

“Vyuo vikuu vinatakiwa kuboresha mifumo ya ufundishaji kwa kuwawezesha wanafunzi kupata uzoefu wa taaluma zao wakiwa vyuoni, hii itasaidia kuondoa tofauti iliyopo baina ya stashahada na shahada,” anasema.

Hilo lisipofanyika, mwalimu Concheska anapendekeza kufutwa kwa elimu ya kidato cha tano na sita.


Wanafunzi wachague wanachotaka

Mwalimu na mtunzi wa vitabu, Richard Mabala anasema kwa kuwa utaratibu wa elimu nchini una mikondo miwili, si dhambi mwanafunzi kuchagua anachokitaka.

Hata hivyo, anaeleza kuwa wingi wa wahitimu wa shahada mitaani bila ajira, ni sababu inayochagiza wahitimu wa kidato cha nne kuchagua vyuo vya kati badala ya kwenda kidato cha tano na sita wakihofia kupoteza muda.

“Hawa wanafanya uamuzi sahihi kwa sababu wanaangalia idadi ya waliomaliza shahada kwa kupitia kidato cha sita hawajapata kazi pamoja na kutumia miaka mingi, lakini wanabaki kama wengine mtaani,” anasema.Mwalimu Mabala anapendekeza utaratibu wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, ufanyike hata kwa wale wanaojiunga na vyuo vya kati, kwa kuwa ndilo kundi kubwa linaloajirika.

“Tukubali kwamba maisha hayana njia moja, kuna fursa anuai, wapo vijana wengine wanafuata mkumbo wa kwenda kidato cha tano na sita mwishowe wanaangukia pabaya,” anasema.

Anabainisha uwepo wa tatizo kwenye vyuo vikuu, akisema vimegeuka shule za msingi kwa kuwa zinafundisha zaidi masomo ya darasani, badala ya kuwaachia wanafunzi nafasi ya kusoma na kupanua mawazo.

Vyuo vya kati ni fursa

Mtafiti wa masuala ya elimu, Muhanyi Nkoronko anasema vijana wamegundua kuwa Tanzania inatoa fursa zaidi za ajira za kada ya kati.

“Muundo wa sasa wa nchi yetu unatoa zaidi fursa za ajira ya kada ya kati na si vinginevyo kwa hiyo vijana wameona wakimbilie vyuo vya kati kupata fursa hizo,” anasema.

Kwa mujibu wa Nkoronko, hofu ya kufeli mtihani wa kidato cha sita ni sababu nyingine inayochagiza wahitimu wa kidato cha nne kukimbilia vyuo vya kati.

Anayejiunga na chuo cha kati ana faida zaidi ya yule anayepitia kidato cha tano na sita kwa kuwa ana fursa ya haraka ya kupata ajira.

Nkoronko anasema kwa dunia ya sasa kunahitajika njia nyingi mbadala zitakazomwezesha mwanafunzi kufikia elimu ya juu akiwa tayari ana ujuzi wa kile anachokwenda kusomea.

Naye mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam (DUCE), Dk Almas Mazigo anasema kujiunga kidato cha tano au astashahada ni uamuzi wa mwanafunzi.

Uamuzi huo unatokana na kile alichokifafanua kuwa, Serikali imeweka njia mbadala za kupita hadi kufikia elimu ya juu, hivyo ni hiari ya mwanafunzi kuchagua apite ipi.

Lakini, anasema anayejiunga na chuo cha kati ni yule ambaye tayari ameshakuwa na chaguo la taaluma anayotamani kusoma, hivyo uamuzi wake unalenga kuanza na msingi wa fani hiyo.

Hali ni tofauti kwa wale wanaohitimu kidato cha nne wakiwa bado hawajapata machaguo ya taaluma wanazotarajia kuzisoma vyuoni, hivyo wanalazimika kuendelea na kidato cha tano na sita ili kupata chaguo sahihi.

“Kwa kadri unavyokwenda kidato cha tano na sita unaelewa mambo mengi na utapata chaguo sahihi la kipi utasoma chuoni, lakini aliyeenda chuo akiwa kidato cha nne, huyu amejua mapema chaguo lake,” anasema.

Mhadhiri mwandamizi wa Elimu, kutoka Chuo Kikuu cha St. Joseph, Dk Kassim Nihuka anaeleza wingi wa vijana wanaojiunga na vyuo vya kati badala ya kwenda kidato cha tano ni kiu ya kupata ujuzi wa kuajiriwa au kujiajiri.

Mtaalamu wa rasilimali watu, Paul Mn’gongo,anasema mabadiliko ya ulimwengu ni chachu ya waajiri kupendelea zaidi wahitimu wa stashahada.

“Watu wanaanza kutoka kwenye vyeti wanaenda kwenye matokeo. Mwajiriwa atakayependwa zaidi ni yule anayeleta matokeo,’’ anasema.

“Wameona fursa haraka zaidi kwa hiyo wameamua kukimbilia kusoma chuo ili wapate ujuzi utakaowawezesha kuishi,” anasema.

Hata hivyo, anasema kupita kidato cha tano na sita ni muhimu zaidi kwa kuwa ndiko kunakomjengea mwanafunzi ukomavu na kumuandaa kujiunga na chuo kikuu.