Patrick Mission inavyojikita zaidi kumuandaa mwanafunzi kujiajiri

Dar es Salaam. Mtaalamu wa Saikolojia, Charles Nduku aliwahi kusema kwa asilimia 70 mtoto huelewa na kujifunza haraka kwa kile anachokiona kwa vitendo.

Anasema ni kwa asilimia 30 pekee, mtoto huelewa kwa kusikiliza anachoambiwa au kufundishwa darasani.

Mtazamo huu wa kisaikolojia, unakinzana na uhalisia wa namna shule na hasa za umma nchini zinavyotoa elimu kwa watoto; masomo ya nadharia darasani huchukua sehemu kubwa kuliko vitendo.

Hata hivyo, hali ni tofauti kwa Shule za Paradise Mission ya mkoani Mbeya na Patrick Mission High School iliyopo Mivumoni, Dar es Salaam.

Shule hizi zimewekeza katika ufundishaji kwa vitendo zaidi, kama anavyoeleza mkuu wa shule hizo, Edwin Peter.

Anasema shabaha ya uamuzi huo ni kumwezesha mwanafunzi kueleza vema anachojifunza darasani kwa kumwekea kumbukumbu ya kudumu katika akili yake, jambo alilosema linapatikana iwapo atafunzwa kwa vitendo.

Katika mahojiano na gazeti hili, Peter anasema mabadiliko hayo yanalenga kuendana na mahitaji ya mitalaa ya sasa ya elimu iliyojikita katika ufundishaji kwa vitendo kuliko nadharia.

“Pamoja na ufundishaji kwa vitendo ndani ya shule, kuanzia kidato cha kwanza mwaka ujao wa masomo watakaochagua kujiunga na shule yetu watanufaika na ziara nyingi za mafunzo zilizoandaliwa ili kujifunza zaidi,” anasema.

Anasema mafunzo kwa vitendo hayatafanyika darasani pekee, bali wanafunzi watafanya ziara kutembelea maeneo mbalimbali, zikiwamo hifadhi za Taifa na mashamba ya kilimo, ili wajionee kwa macho kile wanachojifunza.

Juhudi za mafunzo kwa vitendo, anasema zimeambatana na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wanaosoma katika shule hizo, kwani taaluma bora hujengwa na mazingira rafiki.

“Mazingira hayo yanajumuisha uwapo wa madarasa ya kutosha kulingana na idadi ya wanafunzi, walimu wenye ujuzi na weledi, kuwapo kwa maktaba na maabara za kisasa pamoja na mahitaji mengine muhimu,” anasema.

Kulingana na Peter, shule hizo zina madarasa makubwa yenye viwango vya kisasa. Wastani ni wanafunzi 40 kwa darasa la shule ya sekondari na wanafunzi 35 kwa darasa la shule ya msingi.

Maabara za kisasa za baiolojia, fizikia na kemia ni miongoni mwa maeneo aliyosema uwekezaji mkubwa umefanyika; akisisitiza uwapo wa vifaa vyote muhimu kwa mafunzo kwa vitendo.

“Hii inamfanya mwanafunzi awe bora katika eneo hilo, pia tuna maktaba kubwa zenye vitabu vya kutosha vya ziada na kiada vitakavyomwezesha mwanafunzi kuongeza maarifa ya kile anachojifunza darasani kwa shule zote mbili,” anasema.

Anaeleza shule hizo zina chumba maalumu kwa ajili ya wanafunzi kujifunza masomo ya kompyuta, ambayo hufundishwa na mkufunzi wa masuala ya teknolojia ili kuwaongezea uelewa katika eneo hilo.


Ubora wa walimu

Ili uwe mwalimu katika shule hizo, anasema unalazimika kupitia mafunzo ya miezi mitatu kujengewa umahiri kuendana na mahitaji ya shule husika.

Anaeleza walimu katika shule hizo ni wabobevu na wazoefu katika masomo wanayofundisha, ili kumwezesha mwanafunzi kuandaliwa vizuri kwa ajili ya mitihani.

“Mwalimu anayechukuliwa kufundisha katika shule zetu hupitishwa katika mafunzo maalumu ya miezi mitatu yatakayomuandaa kuendana na kasi ya shule zetu na kuchunguzwa mienendo yake,” anasema.

Kila somo katika shule hiyo, anasema lina walimu watatu, huku hisabati na uchumi kwa kidato cha tano na sita, yana walimu zaidi ya watatu.

“Kuwa na mwalimu zaidi ya mmoja kwa somo katika kila darasa inasaidia mada kuisha kwa haraka pamoja na kuongeza ufanisi katika ufundishaji na upimaji wa wanafunzi,” anaeleza.

Anasema hiyo ndiyo moja kati ya sababu zinazozifanya shule hizo ziwe na mwenendo mzuri wa ufaulu katika mitihani ya kitaifa.

Akitolea mfano mwaka 2017, anasema Shule ya Sekondari Patrick Mission ilitoa wanafunzi wawili walioshika nafasi ya saba na nane kitaifa kwa ufaulu wa masomo ya lugha na sanaa.

Mwaka 2018, ilitoa mwanafunzi wa kwanza kitaifa katika masomo ya lugha na sanaa kwa upande wa wasichana wa kidato cha sita; huku mwaka 2019 ilishika nafasi ya 19 kitaifa kwa kufanya vizuri kitaaluma. Mwaka 2020 ilitoa mwanafunzi wa tatu kitaifa katika masomo ya biashara.

“Katika ngazi ya mkoa kwa matokeo ya kidato cha sita, shule imekuwa ya sita kwa mwaka 2020 na ya saba mwaka 2021. Hakuna mwanafunzi aliyepata daraja la nne wala sifuri," anasema.

Mwaka 2022, Shule ya Patrick Mission kwa upande wa kidato cha sita, wanafunzi 106 waliofanya mtihani, 76 walifaulu kwa daraja la kwanza na 30 la pili; huku kukiwa hakuna daraja la tatu, nne wala sifuri.

“Matokeo ya mwaka huu 2023, wanafunzi 123 waliofanya mtihani 99 wamefaulu kwa daraja la kwanza na 23 la pili. Hakuna la tatu, nne wala sifuri," anasema.

Si taaluma pekee, mkurugenzi wa shule hizo, Ndele Mwaselela anasema nidhamu, ulinzi, chakula na malazi ni mambo mengine yanayozingatiwa shuleni hapo.

Pamoja na uwapo wa walinzi, katika madarasa yote ya shule hizo, anasema kumefungwa mfumo wa kamera za CCTV kuimarisha usalama wa wanafunzi na kufuatilia utekelezaji wa ratiba ya ufundishaji kwa walimu.

“CCTV zilizofungwa katika madarasa zinasaidia kufuatilia kama ratiba ya ufundishaji inazingatiwa na kuchunguza mienendo yao kwa ujumla. Kwa yeyote anayekwenda kinyume cha utaratibu hatua kali huchukuliwa kwa mujibu wa miongozo ya shule," anasema.


Kukuza vipaji

Mwaselela anasema katika shule hizo kuna viwanja vya michezo ikiwamo mpira wa kikapu, pete, wa miguu na riadha kwa ajili ya kukuza vipaji vya wanafunzi.

“Kupitia michezo shule yetu imezalisha vijana wanaocheza katika timu mbalimbali nchini,” anasema.

Suala la kukuza vipaji anasema limewekewa mkazo kwa kuajiri walimu maalumu wa kuwafundisha wanafunzi michezo kulingana na vipaji vyao.

“Pamoja na kuwasaidia wanafunzi kukuza taaluma, pia tunafanya hivyo katika vipaji. Kuna walimu kwa ajili ya kuwanoa wanafunzi wenye vipaji vya kuimba na kucheza,” anasema na kuongeza: “Kupitia ukuzaji wa vipaji vya wanafunzi, tumetoa mwanafunzi anayefanya vizuri katika soka la watoto nchini Brazili.”


Kwa mawasiliano Mkuu wa Shule 0783399713