Safari ya Laura kuwa mtunzi wa kimataifa wa riwaya

Katika mitandao ya kijamii amepewa jina la ‘Fundi mshona maneno’. Ni jina la utani la mwandishi anayekuja kwa kasi kwenye uandishi wa vitabu hususani utunzi wa riwaya.
Hivi karibuni amezindua kitabu kipya kiitwacho ‘Kiroba Cheusi’, kikiwa ni cha pili baada ya ‘Dira ya Moyo’.
Huyu ni Laura Pettie, ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari aliyepata shahada ya kwanza ya taaluma hiyo katika chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT). Katika mahojiano haya Laura pamoja na mambo mengine anaeleza safari yake ya uandishi wa riwaya.
Swali; Wasomaji wetu wangependa kukufahamu historia yako na kujua Laura Pettie ni nani hasa?
Jibu: labda nianze na nilikozaliwa. Mimi nimetokea mkoani Mara kwa maana nimezaliwa huko. Makuzi yangu yamekuwa Dar es Salaam tangu ningali mdogo. Jiji la Dar es salaam kwa hakika limenikuza.
Safari yangu ya uandishi ilianza nikiwa shuleni, wakati huo niliandika hadithi fupi.
Hadithi yangu ya kwanza kabisa iliyojaa daftari zima, niliitunga nikiwa darasa la saba pale Shule ya msingi Mugabe. Nilipoingia sekondari Forodhani, nilipanua wigo wa uandishi. Pale, nikaanza kuandika insha, mashairi, ngonjera na tamthiliya. Nilifanikiwa kutoa hadithi yangu ya kwanza gazetini, na huo ukawa mwanzo wa safari nyingine.
Wakati wanafunzi wenzangu waliposoma vitabu kwa ajili ya kujibu mitihani ya Kiswahili, mimi niliwasoma kina Shaaban Robert, Amandina Lihamba na wengineo, si tu kwa lengo la kujibu mtihani bali pia, kujifunza zaidi kutoka kwao. Nilitaka kuwa mwandishi bora wa riwaya ningali shuleni. Naendelea kuikimbilia ndoto hiyo.
Kwa sasa, nimetunga hadithi nyingi. Fupi na ndefu. Nikizitaja chache tu ni Dira ya Moyo, Nahiyari Mauti, Tabaka – Zuena, Karata tatu, Malkia wa Gitaa na hii ya Kiroba Cheusi. Hivyo, Laura Pettie ni mwandishi kitaaluma, mtunzi na mwandishi wa riwaya, mtoa elimu kwa jamii.
Swali: Unapoandika dhamira yako kuu huwa ni ipi?
Jibu: Kwanza ni kufikirisha kupitia burudani. Ninaposema kufikirisha, ninamaanisha kujitathmini, kuhoji, kukitazama kitu katika mitazamo tofauti na kujifunza. Naweza kutumia mtindo wa mzaha au lugha nyepesi kutimiza haya mambo manne pasipo msomaji kuchoka.
Nafahamu jamii niliyopo, inapenda vitu vyepesi na vitu vilivyo katika hali ya mzaha, visivyotafuna sana akili. Nikaamua, nitawafanya wazitafune akili kwa staili nyingine pasipo wao kuchoka. Hivyo, ninapoandika mada zangu, huwa silengi kuburudisha tu, dhamira yangu kuu huwa kumfikirisha msomaji wakati akiburudika.
Kwa mfano, katika riwaya ya ‘Kiroba Cheusi’, nimezungumzia tatizo la msongo wa mawazo linavyoweza kumuweka mtu kitandani na asijue anaumwa nini. Nchi zilizoendelea, hii ndiyo mada inayopigiwa kelele yaani afya ya akili. Wakati huku Afrika bado tunaamini usipojua unachoumwa basi wewe umelogwa. Hivyo, kupitia riwaya hii nimetimiza dhamira ya kuifikirisha jamii kupitia burudani. Nimelenga kumfanya wasomaji atafakari, wapi tunakosea tunapoutazama msongo wa mawazo miaka hii.
Swali: Hiki ni kitabu chako cha pili kwa lugha ya Kiswahili. Kwa nini umechagua lugha hii au unavitafsiri kwa lugha ya Kiingereza pia?
Jibu: Nakipenda Kiswahili; ninajivunia kukijua na kukitumia. Pili, wasomaji wengi nchini wanakihusudu Kiswahili. Nadhani umeshasikia vuguvugu lililopo nje ya Tanzania juu ya matumizi ya lugha ya Kiswahili. Mpaka hapo nahitaji sababu gani tena kujivunia kazi zangu za Kiswahili?
Ninatarajia kusikia nikiulizwa kwanza juu ya ubora wa lugha ya Kiswahili katika riwaya kabla ya kuulizwa sababu za kukitumia... Ninatamani sana baadaye kazi zangu zipatikane katika lugha ya Kiingereza na Kifaransa.
Changamoto ni gharama ya kuzitafsiri na watenda kazi. Mbali na hayo, ninaujua umuhimu wa vitabu kuwa katika lugha tofauti.
Swali: Unakutana na changamoto gani katika uandishi wa vitabu?
Jibu: Kwangu, changamoto kubwa ni uchache wa mawakala waaminifu kona zote za nchi. Nadhani hii si kwangu peke yangu. Tukifanikiwa kuwa na sehemu za kufikisha vitabu na mapato kurudi mkononi kwa uaminifu, tutapiga hatua kubwa mno katika tasnia hii. Pili, ni gharama za uchapaji. Tunahitaji kampuni za kuchapisha kwa mtindo wa kugawana faida na mwandishi, kwa makubaliano yenye faida pia kwa mwandishi mwenyewe. Itamrahisishia mwandishi kazi ya kuchapa na kusambaza.
Jingine ni sheria za nchi na mitazamo ya kijamii. Kuna mahali mwandishi unajikuta tu unarudisha kalamu chini bila kupenda. Kuna vitu jamii haitaki au inashindwa kuvijadili kwa uwazi. Leo tuna ushoga na usagaji kwenye jamii. Tatizo linalokomaa siku hadi siku. Lakini jamii imegoma kuwa wazi si kwa kukemea wala kujadili vyanzo vya matatizo.