Tuwafunze watoto lugha nyingi inavyowezekana
Muktasari:
- Tanzania ni taifa lenye bahati kubwa kwa kuwa na lugha ya Kiswahili kama nguzo ya umoja.
Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa leo unaobadilika kwa kasi, lugha imekuwa zaidi ya chombo cha mawasiliano.
Ni daraja linalounganisha tamaduni, njia ya urithishaji maarifa na urithi wa vizazi, na pia ni nguzo ya kujitambulisha katika jamii ya kimataifa.
Tanzania ni taifa lenye bahati kubwa kwa kuwa na lugha ya Kiswahili kama nguzo ya umoja. Kiswahili si tu lugha ya Taifa, bali ni alama ya mshikamano inayotufanya sote tuwe familia moja licha ya tofauti za makabila yetu zaidi ya 100.
Hata hivyo, pamoja na kulinda hadhi hii ya Kiswahili, tunapaswa kuwa na upeo mpana zaidi; kuhimiza na kuwekeza katika ufundishaji wa lugha nyingi kwa watoto wetu kuanzia umri mdogo.
Si jambo jipya kusema kuwa mtoto anapojifunza lugha nyingi mapema huwa na uwezo mkubwa zaidi wa kufikiri kwa haraka, kubadili mawazo kwa urahisi, na kujenga misingi thabiti ya utambuzi. Lakini hoja yangu si ya kisayansi pekee, bali ni ya kijamii na ya kitamaduni pia. Tanzania ni taifa lenye hazina ya lugha za kikabila, lakini ni aibu na uchungu kuona kizazi kipya kikizaliwa katika familia ambazo wazazi wanazijua lugha hizo, lakini watoto wao hawawezi hata kutamka salamu za kiasili.
Lugha za makabila zinapotea taratibu kana kwamba hazina thamani, ilhali ndizo nguzo za historia, hekima, na hadithi za vizazi vyetu.
Swali linajitokeza: tukipoteza lugha hizi, tunabaki na nini cha kipekee? Lugha za kikabila ni sehemu ya turathi, na kuzipoteza ni sawa na kufuta kurasa za historia yetu.
Ni wajibu wa taifa na wazazi kuhakikisha kuwa watoto wanazifundishwa, iwe nyumbani au hata kupitia programu rasmi shuleni.
Lugha za kimataifa nazo...
Kwa upande mwingine, tunapokuwa na msingi imara wa Kiswahili na lugha za kikabila, tunapaswa pia kuwekeza katika kuwafundisha watoto lugha za kimataifa. Dunia ya leo haina mipaka. Fursa za kielimu, kibiashara, kiteknolojia, na kidiplomasia mara nyingi zinategemea uwezo wa kuzungumza na kuelewa lugha za kimataifa kama Kiarabu, Kiingereza, Kifaransa, Kichina na nyinginezo.
Mtoto anayejifunza lugha hizi mapema huwa na nafasi ya kuwa raia wa dunia, na mtu anayeweza kusafiri kokote, kujifunza kokote, na kufanya kazi kokote.
Tunapopiga chapuo Kiswahili kama lugha ya kufundishia shuleni, jambo ambalo linafaa na linalowezekana kwa kuwa Kiswahili kina uwezo mkubwa wa kielimu, hatupaswi kuona hilo kama kikwazo cha lugha nyingine.
Badala yake, tuone kama msingi thabiti wa kuongeza ujuzi. Kiswahili kitatufanya tuwe na umoja wa kitaifa, lakini lugha nyingine zitatusaidia kupanua upeo wa kimataifa.
Kuna hoja inayotolewa mara nyingi kuwa kumfundisha mtoto lugha nyingi kutampotezea mwelekeo. Utafiti na uzoefu vinaonyesha kinyume chake: watoto wanaweza kuhimili lugha nyingi bila kuchanganyikiwa, alimradi wanafundishwa kwa njia sahihi.
Kwa mfano, mtoto anaweza kuzungumza Kiswahili mtaani; akajifunza lugha ya kabila lake kupitia mawasiliano ya kifamilia, kisha akajifunza Kiingereza au lugha nyingine shuleni.
Badala ya kuchanganyikiwa, mtoto huyo hukua akiwa na upeo mpana, ujasiri mkubwa wa kuwasiliana, na uwezo wa kuelewa tamaduni tofauti.
Tuwekeze
Ni dhahiri kuwa uwekezaji katika ufundishaji wa lugha nyingi utahitaji sera thabiti na jitihada za pamoja. Shule zinapaswa kupewa mwongozo wa kuanzisha kozi ndogo za lugha za kikabila kwa hiari, huku Serikali na taasisi za elimu zikiimarisha mbinu bora za kufundisha lugha za kimataifa. Wazazi nao wanapaswa kushirikiana kwa dhati, kuhakikisha kuwa watoto wanazisikia na kuzungumza lugha za kifamilia nyumbani.
Faida za hili haziishii kwa watoto pekee. Jamii nzima itanufaika. Tunapofufua lugha za makabila, tunahifadhi hadithi, methali, na hekima zinazoweza kuongoza uamuzi wetu hata leo. Tunapopanua ufundishaji wa lugha za kimataifa, tunajiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kimaendeleo, kwa sababu kizazi chetu kitakuwa tayari kuzungumza lugha moja na mataifa mengine katika biashara, teknolojia na diplomasia.
Ni wazi kuwa kuwekeza kwenye lugha nyingi ni kuwekeza kwenye urithi na mustakabali kwa pamoja.
Tanzania si kisiwa. Tunaposhirikiana na mataifa mengine, lugha ndiyo pasipoti yetu ya kwanza. Mtoto aliyelelewa katika mawanda ya lugha nyingi si tu kwamba atakuwa mwepesi wa kuwasiliana, bali pia atakuwa na fikra za kidunia.
Atajua kuwa ulimwengu una zaidi ya njia moja ya kusema kitu, zaidi ya namna moja ya kufikiri, na zaidi ya tamaduni moja ya kuishi. Hii ndiyo tunu ya kweli ya elimu ya lugha nyingi.
Nisisitize kuwa j ambo hili halipaswi kuonekana kama ndoto ngumu. Tukiamua kwa dhati, tukakubaliana kwamba kila mtoto awe na nafasi ya kujifunza lugha yake ya kabila, Kiswahili, na angalau lugha moja ya kimataifa, basi tunaweza kulitekeleza.
Tumeweza kuimarisha Kiswahili hadi kuwa lugha ya kitaifa na hata kimataifa; tunaweza pia kufanikisha safari hii mpya ya kujenga kizazi cha Watanzania wenye upeo mpana wa lugha. 0754990083