Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uchakavu Shule ya Msingi Namahonga watia hofu wazazi, wanafunzi



Tandahimba. Hofu na wasiwasi vimetanda miongoni mwa wazazi na wanafunzi katika Shule ya Msingi Namahonga, iliyopo Kata ya Maundo, wilayani Tandahimba mkoani Mtwara, kufuatia uchakavu mkubwa wa miundombinu ya madarasa.

Shule hiyo yenye zaidi ya wanafunzi 600, ikiwa na walimu sita wa ajira na mmoja wa kujitolea, inakabiliwa pia na upungufu wa madawati, ofisi ya walimu na walimu wenyewe, hali inayotajwa kushusha kiwango cha ufaulu.

Hata hivyo, licha ya kilio cha wananchi na wanafunzi, uongozi wa Serikali wilayani humo haujaweka wazi hatua za kukabiliana na changamoto hizo, walipotafutwa na gazeti hili.

Wanafunzi wa shule ya msingi Namahonga wakiwa wamekaa chini darasani

Wakizungumza na Mwananchi hivi karibuni, baadhi ya wazazi wamesema shule hiyo ina madarasa machache na mengine yamechakaa, huku baadhi ya paa zikivuja na kuta kuwa na nyufa, hali inayosababisha usumbufu mkubwa kwa wanafunzi hasa wakati wa mvua.

“Shule ina watoto wengi lakini madarasa ni machache na yamechakaa. Wanafunzi hawana sehemu ya kukaa, wanalazimika kukaa chini, wengine wakitumia viroba kutandikia ili waweze kuandika,” amesema Jaffari Pitemu.

Amesema hofu yao huongezeka zaidi nyakati za mvua, ambapo hulazimika kuwahi shuleni kuwachukua watoto wao ili kuwaepusha na hatari ya kuangukiwa na majengo yasiyo imara.

Majengo ya madarasa ya shule ya msingi Namahonga.

“Tukiona dalili za mvua, tunawahi kuwafuata watoto na wakati mwingine walimu hulazimika kuwatoa mapema. Tunaishi kwa hofu kila siku,” amesema Dadi Juta.

Dadi ameongeza kuwa hali hiyo imeanza kuathiri kwa kiasi kikubwa taaluma ya wanafunzi, kutokana na baadhi yao kushindwa kuhudhuria masomo kikamilifu, jambo linalochangia kuongezeka kwa utoro.

“Mtoto akikaa chini au kubanana hawezi kufuatilia masomo vizuri. Tatizo hili linaathiri moja kwa moja matokeo yao, na kwa sasa utoro ni mwingi kutokana na mazingira hayo,” amesema.

Naye Mustafa Nammundila amesema hata ofisi ya walimu imechakaa kupita kiasi na ipo katika hali mbaya kiasi kwamba haiwezi kutumika ipasavyo, hali inayowalazimu walimu kufanya kazi katika mazingira magumu.

Majengo ya madarasa la shule ya msingi Namahonga

“Ofisi ya walimu imechakaa sana, haiwezekani kabisa kuitumia. Walimu wanafanya kazi katika mazingira magumu na hii inaathiri sana taaluma ya wanafunzi,” amesema.

Nammundila ameomba Serikali kuchukua hatua za haraka, akisisitiza kuwa watoto wanahitaji mazingira salama na rafiki ili waweze kufikia ndoto zao za elimu na kurejesha utulivu kwa jamii.

“Tunaamini Serikali ikichukua hatua za haraka, watoto wetu watapata haki yao ya msingi ya elimu bora, ufaulu utaongezeka na walimu watafanya kazi zao kwa ufanisi,” amesema.

Wanafunzi wa shule ya msingi Namahonga wakiwa wamekaa chini darasani


‘Changamoto zipo’

Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo, Masha Rahani, amekiri kuwepo kwa changamoto hizo, akieleza kuwa majengo yaliyopo ni matatu pekee na yote yako katika hali chakavu, hivyo si salama kwa wanafunzi.

Amesema changamoto hizo zimedumu kwa muda mrefu na kamati ya shule imekuwa ikiwasilisha malalamiko kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe kabla ya madhara makubwa kutokea.

“Baada ya kuwasilisha kero hiyo kwa mkurugenzi wa halmashauri, wataalamu walitembelea shule kufanya ukaguzi wa kina na tathmini ya majengo ili kubaini hatua stahiki za ukarabati au ujenzi mpya,” amesema.

Ameongeza kuwa Aprili 6 mwaka huu, mhandisi wa halmashauri, afisa mipango miji na afisa elimu walifika kufanya ufuatiliaji, lakini hadi sasa bado wanasubiri hatua zaidi zitakazochukuliwa.

Jengo la ofisi ya walimu wa shule ya msingi Namahonga

Jitihada za kumpata Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tandahimba, Mariam Mwanzalima hazikufanikiwa, kwani baada ya kusikiliza maelezo ya mwandishi simu yake ilikatika na alipotafutwa tena simu iliita bila kupokelewa.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Michael Mtenjele alipotafutwa alihoji hatua ya mwandishi kufika shuleni hapo bila kufuata taratibu za kuomba kibali kutoka kwa mkurugenzi au ofisi ya mkuu wa wilaya.

“Aliyekupeleka huko ni nani? Unaendaje huko? Sikiliza, hii wilaya ni maalumu, kila unapokwenda lazima upate kibali kwa mkurugenzi au mkuu wa wilaya,” alisema.

Alipoelezwa kuwa mkurugenzi hakutoa ushirikiano, alihoji kwa nini mwandishi alimtafuta mkurugenzi baada ya kufika eneo la tukio.

“Huo ndiyo utaratibu? Hakuna kujiendea tu Tandahimba hii. Utaratibu ufuatwe, fika ofisini upewe kibali cha kwenda huko. Unajiendea ukipata shida utatwambia nani amekupeleka?” alisema.

Alisisitiza kuwa mwandishi anapaswa kupata kibali rasmi ndipo mamlaka zitaweza kuthibitisha usahihi wa taarifa hizo, badala ya kufika eneo la tukio bila utaratibu.