Vita, machafuko vyatajwa chanzo watoto kuachishwa shule
Muktasari:
- Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa Jumanne, Juni 23, 2026 na kufanyiwa uchambuzi na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia elimu katika mazingira ya dharura, Education Cannot Wait (ECW), jumla ya watoto milioni 258 duniani kwa sasa wanakumbwa na changamoto ya elimu yao kuvurugwa kutokana na vita, machafuko ya ndani ya nchi, ukosefu wa uthabiti wa kisiasa pamoja na athari zinazoongezeka za mabadiliko ya tabianchi.
Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa (UN) imezua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa elimu duniani baada ya kubainisha kuwa karibu watoto milioni 100 wameachishwa shule moja kwa moja kutokana na migogoro inayoendelea katika maeneo mbalimbali hali inayotajwa kuwa tishio kubwa kwa maendeleo ya vizazi vijavyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa Jumanne, Juni 23, 2026 na kufanyiwa uchambuzi na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia elimu katika mazingira ya dharura, Education Cannot Wait (ECW), jumla ya watoto milioni 258 duniani kwa sasa wanakumbwa na changamoto ya elimu yao kuvurugwa kutokana na vita, machafuko ya ndani ya nchi, ukosefu wa uthabiti wa kisiasa pamoja na athari zinazoongezeka za mabadiliko ya tabianchi.
Ripoti hiyo inaeleza kati ya hao, takribani watoto milioni 93 wameachishwa kabisa elimu, huku wengine wakishindwa kuhudhuria shule mara kwa mara kutokana na mazingira yasiyo salama, uharibifu wa miundombinu ya elimu na kuhama kwa familia kutokana na vita au majanga ya asili.
Takwimu hizo zinaonesha pia kuwa karibu asilimia 60 ya watoto wote walioathirika wanatoka katika nchi tisa pekee ambazo ni Afghanistan, Bangladesh, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Ethiopia, Myanmar, Nigeria, Pakistan, Sudan na Yemen nchi ambazo zimekuwa zikikabiliwa na migogoro ya muda mrefu pamoja na changamoto za kiuchumi na kiusalama.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa ECW, Maysa Jalbout, matokeo ya ripoti hiyo yanaonesha wazi kuwa dunia inakabiliwa na ongezeko la kasi la watoto wanaokosa elimu.
Hali inayosababishwa zaidi na kuongezeka kwa migogoro ya kivita pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimekuwa zikizidisha uharibifu wa miundombinu na maisha ya jamii.
Amesema kuwa hali hiyo inaashiria pengo kubwa la uwekezaji katika sekta ya elimu ya dharura, huku akisisitiza kuwa bila hatua za haraka, mamilioni ya watoto wataendelea kupoteza fursa ya msingi ya elimu na hivyo kuathiri maendeleo ya muda mrefu ya mataifa husika.
Ripoti hiyo pia imebainisha kuwa changamoto nyingine zinazochangia hali hiyo ni pamoja na mdororo wa kiuchumi duniani, kupungua kwa misaada ya kibinadamu kutoka mataifa tajiri, pamoja na ongezeko la majanga ya hali ya hewa kama ukame na mafuriko yanayohusishwa na mabadiliko ya tabianchi na hali ya El Niño.
Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa serikali duniani kuongeza uwekezaji katika elimu ya dharura, kuhakikisha shule katika maeneo ya migogoro zinarejeshwa haraka, na kuweka mikakati ya muda mrefu ya kulinda haki ya msingi ya mtoto kupata elimu hata katika mazingira magumu ikiwa ni faida kwa kizazi kijacho.