Prime
Wadau, Serikali waanika njia za kuikwamua elimu jumuishi - 3
Muktasari:
- Mbali na kuboresha miundombinu na mabweni, Serikali inakusudia kuongeza walimu maalumu watakaosaidia kutekeleza programu ya elimu ya nyumbani
Dar es Salaam. Licha ya hatua zinazochukuliwa na Serikali za kuimarisha elimu jumuishi, wadau wanasema safari bado ni ndefu ya kuhakikisha kila mtoto, bila kujali aina ya ulemavu au changamoto alizonazo anapata haki ya elimu katika mazingira yanayokidhi mahitaji yake.
Tanzania inatekeleza sera na miongozo inayolenga kuwajumuisha watoto wenye mahitaji maalumu katika mfumo wa elimu wa kawaida, ukiwamo Mkakati wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi 2022/2026.
Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi uliofanywa katika wilaya za Bagamoyo mkoani Pwani na Kilombero mkoani Morogoro, umebaini changamoto za uhaba wa walimu wenye ujuzi maalumu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, pamoja na miundombinu isiyokidhi mahitaji ya wanafunzi hao, zimeendelea kuathiri ubora wa huduma zinazotolewa shuleni.
Wataalamu wa elimu wanaonya kuwa bila uwekezaji wa kutosha katika maeneo hayo, lengo la kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma katika kupata elimu linaweza kuwa gumu kufikiwa.
Kwa mujibu wao, elimu jumuishi haiwezi kufanikiwa kwa kutegemea sera pekee, bali inahitaji rasilimali, usimamizi na ushirikiano wa wadau wote kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.
Mapendekezo ya wadau
Clarence Mosha, Mratibu wa miradi wa Shirika la Sawa Education linalofanya shughuli zake Ifakara, wilayani Kilombero, anasisitiza umuhimu wa kuimarisha utekelezaji wa sera na miongozo iliyopo, badala ya kuishia katika hatua ya kuziandaa.
Anasema Tanzania ina sera na miongozo inayotambua haki ya watoto wenye mahitaji maalumu kupata elimu, lakini changamoto kubwa ipo katika utekelezaji kutokana na bajeti ndogo zinazotengwa kwa ajili ya shughuli za elimu jumuishi.
“Ikiwa tunataka kila mtoto apate elimu bora ni muhimu kuwekeza katika miundombinu ya shule, upatikanaji wa walimu wa kutosha, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, pamoja na mazingira rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu,” anasema.
Mosha anasema kuongeza fedha pekee haitoshi kama hakutakuwa na mfumo wa kufuatilia namna rasilimali hizo zinavyotumika sambamba na utaratibu wa mara kwa mara wa kutathmini utekelezaji wa sera za elimu jumuishi katika shule zote nchini.
Vilevile, anasema ni muhimu kuwashirikisha wadau wote katika ngazi za jamii, akieleza kuwa wazazi wanapaswa kuhakikisha watoto wanapelekwa shule, huku viongozi wa mitaa na vijiji wakifuatilia waliopo kwenye maeneo yao ili wasikose haki ya elimu.
“Watumishi wa umma na wadau wa elimu wanapaswa kuendelea kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu jumuishi ili kila mtoto apate fursa sawa ya kujifunza na kufikia ndoto zake,” anasema.
Digna Mushi, Mkuu wa miradi wa shirika la Ocode linalofanya shughuli wilayani Bagamoyo mkoani Pwani anasema kuna wadau wengi wa elimu jumuishi wanaofanya kazi kwa juhudi kubwa lakini bila mfumo mmoja wa uratibu unaoeleweka kitaifa.
Kutokana na hilo, anasema ni vyema kuwa na mfumo wa kitaifa wa kuwasajili na kuwapanga wadau wote ili iwe rahisi kujua kila mmoja anafanya nini, yuko wapi na anahudumia eneo lipi.
Mbali ya hilo, anasema bila bajeti madhubuti mikakati mizuri inabaki kuwa mipango isiyotekelezeka kikamilifu, hivyo anapendeleza Serikali itenge fungu maalumu la elimu jumuishi na kuongeza ruzuku ya elimu kwa watoto wenye mahitaji maalumu.
Hatua hiyo anasema itasaidia katika ununuzi wa vifaa saidizi kama vile vya usikivu, vitabu vya nuktanundu na vifaa vingine vya kujifunzia.
Mtaalamu wa elimu jumuishi, Amina Mfaume, anaamini mafanikio yanaanza na utambuzi wa mapema wa mahitaji ya mtoto, akieleza wengi wenye changamoto za kuona, kusikia au kujifunza hushindwa kupata msaada kwa wakati kwa sababu hawabainiki mapema wanapoanza shule.
“Mtoto asipotambuliwa mapema, mwalimu hawezi kujua namna sahihi ya kumsaidia. Matokeo yake anaweza kuonekana hana uwezo wa kujifunza wakati tatizo ni changamoto ambayo ingeweza kushughulikiwa mapema,” anasema.
Kutokana na hali hiyo, anapendekeza Serikali na wadau wa elimu kuongeza uwekezaji katika vifaa vya uchunguzi na tathimini ya watoto pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu ili kuwawezesha kutambua dalili za awali za mahitaji maalumu.
Mhadhiri wa masuala ya elimu maalumu, Dk Josephina Mallya anasema mafanikio ya elimu jumuishi yanategemea pia uwezo wa walimu kutumia vifaa na mbinu zinazohitajika katika ufundishaji.
Anasema shule nyingi zinaweza kupatiwa vifaa lakini vikashindwa kuleta matokeo yaliyokusudiwa ikiwa walimu hawajapatiwa mafunzo ya kutosha.
“Tunahitaji mfumo unaounganisha vifaa, mafunzo na wataalamu wa ushauri,” anasema.
Dk Mallya anasema ni muhimu kujenga mfumo wa ushirikiano kati ya sekta za elimu, afya na ustawi wa jamii ili watoto wenye mahitaji maalumu wapate huduma zote wanazohitaji kwa wakati mmoja.
Baadhi ya wazazi wa watoto wenye ulemavu wilayani Bagamoyo wanasema kwa muda mrefu walikuwa na hofu ya kuwapeleka watoto wao shule kutokana na ukosefu wa mazingira salama na huduma zinazokidhi mahitaji yao.
Miongoni mwao, Rehema Sultani, mzazi wa mtoto mwenye ulemavu anasema ujenzi wa bweni katika Shule ya Msingi Nianjema umeongeza imani kwa wazazi wengi ambao awali walisita kuwapeleka watoto wao shule.
“Mtoto mwenye ulemavu anahitaji mazingira maalumu ili aweze kujifunza kwa utulivu kama watoto wengine. Tunapoona miundombinu kama mabweni, tunaamini watoto wetu watakuwa salama na kupata huduma wanazohitaji,” anasema.
Shaban Mwinyimkuu anasema uwepo wa huduma umewahamasisha wazazi waliokuwa wamewaficha watoto nyumbani kuanza kuwapeleka shule.
“Mazingira yanapokuwa rafiki, mzazi anakuwa na amani ya moyo. Tunaona mabadiliko makubwa kwa sasa kwa sababu wazazi wameanza kuamini kuwa watoto wao wanaweza kusoma na kufanikiwa,” anasema.
Kauli za wazazi hao zinathibitishwa na mkuu wa kitengo maalumu katika Shule ya Msingi Nianjema, Suzana Nkya anayesema miundombinu wezeshi imekuwa nyenzo muhimu ya kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu uwezo wa watoto wenye ulemavu.
“Watu wengi walikuwa wanaamini kuwa watoto wenye ulemavu hawawezi kujifunza au kujitegemea. Lakini wanapoona watoto hawa wakisoma, wakicheza na kushiriki shughuli mbalimbali za shule wanabadilisha mtazamo wao. Hii ndiyo sababu miundombinu rafiki ni sehemu muhimu ya mafanikio ya elimu jumuishi,” anasema.
Nini mikakati ya Serikali
Wadau wakitoa mapendekezo hayo, Mkurugenzi wa Elimu Maalumu, Dk Magreth Matonya anasema Serikali imejipanga kuimarisha elimu jumuishi kwa kuanzisha shule maalumu za mfano katika kila halmashauri nchini.
Mpango huo anasema unalenga kuwa na shule mbili katika kila halmashauri (moja ya msingi na moja ya sekondari), ambazo zitakuwa na miundombinu na huduma zote muhimu kwa watoto wenye mahitaji mbalimbali ya elimu.
Shule hizo zitajengwa kwa kuzingatia misingi ya elimu jumuishi ili kuhakikisha watoto wote, bila kujali aina ya ulemavu au changamoto walizonazo wanapata fursa sawa za kujifunza na kufurahia maisha ya shule.
Mbali na kuboresha miundombinu na mabweni, Serikali pia inakusudia kuongeza walimu maalumu watakaosaidia kutekeleza programu ya elimu ya nyumbani.
“Utafiti uliofanyika umebaini kuna baadhi ya watoto wenye ulemavu mkubwa ambao hawawezi kuchangamana na wenzao darasani, licha ya kuwa na uwezo mzuri wa kiakili. Wapo pia watoto wenye changamoto za kiafya zinazowalazimu kutumia vifaatiba muda wote, hali inayowafanya washindwe kuhudhuria shule za kawaida,” anasema.
Kutokana na hali hiyo, mfumo wa elimu ya nyumbani umeonekana kuwa suluhisho muhimu kwa watoto hao.
Serikali inalenga kutumia walimu wa ziada kutoka katika shule hizo za mfano ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi wanaohitaji huduma hiyo, kwa kuzingatia kaulimbiu ya kutomwacha mtoto yeyote nyuma.
Vilevile, Serikali inaendelea kutekeleza programu ya elimu kwa watoto wanaolazwa hospitalini.
“Kuna watoto wengi wanaotoka mikoa mbalimbali kama Mtwara, Lindi na maeneo mengine hupelekwa katika hospitali kubwa kama Muhimbili na Bugando kwa matibabu yanayoweza kuwafanya wakae hospitalini kwa miezi sita hadi saba bila kuendelea na masomo,” anasema.
Kupitia programu hiyo, anasema walimu hushirikiana na hospitali na shule za watoto husika ili kufuatilia ratiba zao za matibabu pamoja na maendeleo yao ya masomo.
“Baada ya mtoto kumaliza ratiba zake za kitabibu, mwalimu huingia na kuendelea kumfundisha kulingana na mtaala anaousoma shuleni kwake. Hili limeshaanza kufanyika Hospitali ya Taifa Muhimbili na linaonesha matokeo mazuri,” anasema na kuongeza:
“Hata hivyo, ili kuupanua na kuwafikia watoto wengi zaidi wenye mahitaji maalumu ya elimu, Serikali inahitaji kuongeza idadi ya walimu watakaohudumu katika programu za elimu ya nyumbani na elimu kwa watoto waliolazwa hospitalini.”