Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Walimu shule binafsi wanavyomenyeka maandalizi mitihani ya Taifa

Muktasari:

Shule nyingi binafsi humuweka mwalimu anayefundisha madarasa ya mitihani kwenye kipimo sawa na mwanafunzi.

Dar es Salaam.Elimu ya Tanzania inapimwa kwa kupitia mitihani ya kuandika ambayo huhitaji bidii ya hali ya juu.

Mitihani hii inamfanya mwanafunzi mara kwa mara akeshe usiku kucha ili kujikumbusha yote aliyosoma miaka minne mfululizo.

Hii ni tofauti na mitihani ya taasisi za elimu ya juu ambayo hupimwa kwa mfumo wa kozi, yaani mtalaa wa moduli (modular curriculum)’, ambapo kinachosomwa kwa miezi kadhaa hupimwa pasipo kujirudia kwenye tathmini ya mwisho.

Katika mfumo wa elimu ya sekondari, ngazi za upimaji hulenga kukuza mada kutoka nyepesi kwenda ngumu (simple to complex), hivyo mwanafunzi hulazimika kukomalia muhtasari kuanzia wa kidato cha kwanza hadi wa kidato cha nne.

Hali ilivyo kwa walimu

Walimu wa shule za umma hawana ugumu na msike mshike wa kuandaa wanafunzi wa madarasa ya mitihani sawa na wale wa taasisi binafsi ambao hufanya juhudi za kufa na kupona.

Hilo ni kwa sababu ajira yao hutegemea kiwango cha ufaulu wa wanafunzi wao kwenye mitihani ya Taifa.

Walimu wa shule za umma wanaweza kupata matokeo yenye sifuri hata kwa zaidi ya wanafunzi 300 pasipo hata mwalimu mmoja wa somo kuhamishwa wala kukaripiwa.

Hata hivyo, kwa sasa hali katika shule hizo ni kama imebadilika. Tumeshudia hatua za kinidhamu na matamko ya kukemea ufaulu mdogo katika shule za umma, ambazo baadhi nazo zimejikuta katika harakati za kupambania ufaulu mkubwa. Inatia matumaini!

Hata hivyo, majanga yapo kwa upande wa walimu wa shule binafsi.Hawa wataalamu wanapitia changamoto kubwa hasa kwa wale ambao masomo yao yamefan ya vibaya.

Walimu hawa huwekwa kwenye mizani kinzani pasipo kuzingatia kwamba kisaikolojia kufeli na kufaulu kwa mwanafunzi huchangiwa na sababu nyingi na si mwalimu pekee.

Shule nyingi binafsi humuweka mwalimu anayefundisha madarasa ya mitihani kwenye kipimo sawa na mwanafunzi.

Mathalani kwenye shule binafsi wanakosoma watoto wengi kutoka familia zenye uwezo, walimu hukesha na wanafunzi katika maandalizi ya mitihani hiyo, huku wakiahidiwa motisho endapo matokeo ya mitihani yatakuwa mazuri.

Hata hivyo, motisha hii huwa pengine haina uhalisia kwani haiweki mizani ya muda na uwekezaji anaokuwa ameuweka mwalimu tangu mwanafunzi akiwa kidato cha kwanza mpaka cha tatu.

 Licha ya wanafunzi kugharamia masomo ya ziada, baadhi ya shule hulipa walimu mishahara ya kawaida bila nyongeza ya posho kwa kazi hii ya kuandaa watahiniwa nje ya muda ulioainishwa kwenye mkataba.

Maandalizi ya mitihani ya mwisho ya kidato cha nne huambatana na mitihani ya majaribio (mock examinations) ambayo huandaliwa na ofisi za elimu za wilaya na mkoa.

Baadhi ya walimu hulalamikia utaratibu mzima wa kuandaa mitihani hii kwa sababu fedha kidogo hutolewa kugharamia usahihishaji na utunzi wa mitihani.

Hali hii husababisha baadhi ya taasisi binafsi kuandaa tathmini zao, kama ilivyo kwa shule kongwe hasa za Kanisa Katoliki na nyinginezo.

Wachambuzi wa elimu wanasema mitihani ya majaribio ina majibu mseto katika uwezekano wa kutabiri matokeo ya wanafunzi kwenye mitihani ya Taifa.

Wengine wanasema mitihani hiyo ni migumu mno na pengine hutungwa kwa lengo la kuwakomaza watoto kitaaluma.

Mitihani ya ndani kama sehemu ya tathmini endelevu kabla ya tathmini ya mwisho, imegeuka shubiri kwa walimu wanaoiandaa, kwani hulipwa kidogo.

Kibaya zaidi ni pale walimu wanapotishiwa na wamiliki wa taasisi hizi kwamba endapo kutakuwa na matokeo mabaya, basi tayari huwa ni hukumu kamili ya kumfukuza kazi mwalimu wa somo husika.

Katika nchi yenye wathibiti ubora wa taasisi za elimu na wanasheria wanaoweza kupitia mikataba ya wafanyakazi, ni ajabu kuona mazingira haya ya uonevu kazini yanavumilika.

Kwa hapa nchini hilo linawezekana pengine kwa kwa sababu shule za sekta binafsi nyingi ziko chini ya matajiri na wanasiasa.

Walimu katika shule hizi wanawaandaa watoto katika kile kinachojulikana kama maandalizi ya usiku, ambayo aghalabu huanza saa moja hadi saa nne.

Baadhi ya shule huruhusu wanafunzi wa madarasa ya mitihani kukesha wakijiandaa na mitihani, huku mwalimu akilazimika kukaa nao hadi usiku wa manane.

Hoja ya wamiliki ni kuwa endapo wanafunzi watakwama katika mchakato wa kujisomea, basi ‘hakimu’ awe karibu kutatua mgogoro, lakini bila posho yoyote.

Ikumbukwe mwalimu huyu anayekesha bado, asubuhi yake anatakiwa kuwahi shuleni, kama anavyotoa ushuhuda mwalimu huyu ambaye hakutaka kutaja jina lake.

 “Kaka mwaka jana nilikuwa mtumwa wa mvua za mwezi wa tatu. Naishi Mbezi kwa Msumi na shule iko katikati ya mji. Saa sita mvua ilininyeshea, hakukuwa na daladala, nikapanda pikipiki. Nilifika nyumbani alfajiri na bado nilipaswa kuwahi kazini.’’

Hakuna namna

Hali ya ajira nchini huchangia masaibu ya walimu kwani wanalipwa kiduchu na kulazimika kuwa wanyenyekevu kwa sababu ya ugumu wa maisha.

“Hakuna namna kaka, mishahara ni kidogo wakati wanafunzi wanalipa ada kubwa. Ukitoka kazi leo, kesho wanaitwa wengine. Tunaamua kukomaa,” anasema mwalimu huyo mkongwe wa somo la jiografia anayeishi jijini Dar es Salaam.

Mwalimu mwingine, Neema Mkusi (jina si lake anasema; “Ukitaka kujua ugumu wa shule binafsi ndugu njoo hapa. Yaani tangu maandalizi ya mitihani yashike kasi mimi ni mwalimu wa fizikia sionekani nyumbani kwangu wala kanisani.

Yaani naishi shuleni kulinda kibarua. Nina chumba kabisa jirani na mhudumu wa wanafunzi bwenini. Tunakula msosi wa madogo (wanafunzi)… ni hatari, wanafunzi wenyewe unawaona hawasikii, usiku kuwakimbiza hata kujisomea hawataki…wamekata tamaa.’’


Maandalizi ya mitihani ilivyo

Kuna mawazo mseto kati ya wanafunzi na walimu kuhusu maandalizi ya mitihani. Wakati walimu wakilia na hali ngumu ya maisha, wanafunzi wanasema wanafundishwa kupita kiasi.

“Tumemaliza mtalaa wa kidato cha nne tangu mwezi wa 10 mwaka jana. Marudio yamekuwa mengi kiasi kwamba tungehitaji sana kujisomea wenyewe. Wataalamu wanasema wapishi wengi huharibu mchuzi. Sasa huku hii kufundishwa kiasi hiki, hatupumui,” anasema mwanafunzi Gregory Samuel.

Wamiliki wa shule wanatumia mbinu mbalimbali kuandaa wanafunzi kwa mitihani.

Kuna baadhi ya shule hulazimika kuwaleta wahamasishaji (motivational speakers) ambao wanachangiwa fedha nyingi na wazazi kuwapa wanafunzi mbinu bora za kufaulu mitihani.

Hata hivyo, baadhi walimu wanasema wahamasishaji hawa hawana taaluma ya masuala ya elimu na hutoa maelezo potofu kuhusu mbinu za kujibu mitihani, hivyo kuwapotosha wanafunzi.



“Haiwezekani mimi nimekaa na mwanafunzi miaka yote minne nishindwe kumshauri. Halafu mtu anakuja kupewa kitita cha laki nne kwa kuongea tu saa mbili hadi tatu ilhali mimi nakesha,’ anasema mwalimu mmoja wa hisabati jijini Dar es Salaam.

Anaongeza: ‘’Hawa watoto sipewi posho yoyote zaidi ya mshahara wangu. Hatuna tofauti na mwana mpotevu aliyechinjiwa ndama wakati mnyenyekevu akiishia kubeba kichwa cha busara tu pasipo tija.’’

Haya ndio maandalizi sahihi ya mitihani

Maandalizi sahihi kwa mitihani ya taifa ni muhimu kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata matokeo bora na kujiandaa kwa maisha ya baadaye.

Katika nchi zilizo na mifumo ya elimu iliyofanikiwa, maandalizi ya mitihani yanazingatia mbinu mbalimbali za ufundishaji na tathmini endelevu.

Wataalamu wa elimu wanasema kwamba maandalizi haya yanajumuisha majaribio ya mara kwa mara, tathmini za vitendo na ushirikiano wa karibu kati ya walimu na wazazi.

Dk John Doe, mchambuzi wa elimu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, anasema: “Mitihani ya taifa inapaswa kuwa kipimo cha jumla cha maarifa na ujuzi wa mwanafunzi.

‘‘Hata hivyo, ni muhimu kwamba maandalizi ya mitihani yasiangalie tu mtalaa bali pia yaweke mkazo kwenye kuendeleza ujuzi wa maisha na fikra huru.”

Pia, wanasaikolojia wanasema maandalizi mazuri yanapaswa kuzingatia afya ya akili ya wanafunzi.

“Wanafunzi wanahitaji muda wa kupumzika na kushiriki katika shughuli nyingine za kijamii ili kuhakikisha wanakuwa na afya bora ya akili. Shinikizo la mitihani linaweza kusababisha msongo wa mawazo ambao unaathiri utendaji wao,” anasema Dk Appolo Mugyenyi, mtaalamu wa tathmini na upimaji katika elimu kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira.

Kwa nchi kama Finland, ambapo mfumo wa elimu unajulikana kwa ubora wake, wanafunzi wanapewa muda wa kutosha wa kujisomea wenyewe, huku walimu wakipewa uhuru wa kufundisha kwa mbinu mbalimbali.

Hii inawasaidia wanafunzi kujifunza kwa kina na kufaulu mitihani kwa njia bora zaidi.

Hivyo basi, ni muhimu kwa shule za Tanzania kuzingatia mbinu bora za maandalizi ya mitihani, kwa kuzingatia mahitaji ya mtalaa, tathmini endelevu na kuzingatia afya ya akili ya wanafunzi.

Matokeo bora ya mitihani yatasaidia sio tu wanafunzi, bali pia kuboresha mfumo wa elimu kwa ujumla pasipo kumuumiza mwalimu au mwanafunzi.