Watoto wanawatazama na kuwafuatilia kina nani?
Muktasari:
- Katika zama hizi za mitandao ya kijamii na televisheni, swali kubwa la kujiuliza ni: Watoto wetu wanawatazama na kuwafuatilia kina nani?
Dar es Salaam. Watoto ni vioo vidogo vya jamii. Wanachoona ndicho wanachojifunza, na wanachosikia ndicho wanachojaribu kuiga.
Katika zama hizi za mitandao ya kijamii na televisheni, swali kubwa la kujiuliza ni: Watoto wetu wanawatazama na kuwafuatilia kina nani?
Je, wanawafuata watu wanaojenga maadili na kuwapa ndoto za maisha bora, au wanawafuata tu wale wanaoonekana maarufu hata kama wanaishi maisha ya kupotosha?
Ni dhahiri kuwa kila mtoto anahitaji mfano wa kuigwa. Lakini mifano hiyo iwe mizuri, yenye kujenga, na inayoonyesha kuwa maisha ya mafanikio yanajengwa kwa maadili, bidii na uadilifu.
Katika jamii yetu ya Tanzania, tuna watu wengi waliothibitisha kuwa ndoto zinaweza kufanikishwa bila kulazimika kupoteza heshima au kuharibu maadili.
Mfano mzuri ni Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli. Alijulikana kama mtu wa kazi, mchapa kazi na aliyependa kuona kila jambo linafanywa kwa umakini na pasipo ajizi.
Mtoto akimfuatilia Magufuli, ataona thamani ya nidhamu, bidii na faida ya uharaka katika uwajibikaji.
Hata baada yake, Rais Samia Suluhu Hassan, amekuwa mfano wa pekee kwa watoto wetu wa kike kwamba mwanamke anaweza kufanikisha mambo makubwa na kuongoza taifa.
Hii inawapa watoto ujumbe kwamba ndoto zao ni halali, iwe ni kwa wavulana au wasichana.
Upande mwingine
Lakini hebu tuangalie upande mwingine. Mitandao ya kijamii na televisheni zimejaa wasanii, watu mashuhuri na wanamitindo wanaopata umaarufu kutokana na maisha ya anasa, ulevi, matusi au maudhui yasiyo na maadili. Watoto wengi wanapenda kuwaiga watu hawa kwa sababu wana wafuasi wengi na wanajulikana kila kona.
Hapo ndipo tatizo linapoanzia. Umaarufu bila maadili ni sumu inayoweza kuharibu kizazi kizima.
Mtoto akiona kuwa njia ya kufanikiwa ni kutengeneza kashfa, kupiga picha zisizo na heshima au kutumia lugha chafu, atapotea mapema kabla hata hajajua maana ya maisha.
Wazazi na walimu wana jukumu kubwa, wasiwaachie watoto wao kufuatilia chochote bila mwongozo. Badala yake, wawasaidie kutambua watu wenye mchango chanya katika jamii.
Kwa mfano, wachezaji wa mpira kama Mbwana Samatta walipanda ngazi ya kimataifa kutokana na kipaji, nidhamu na bidii.
Ni wazi kuwa watoto wanaowatazama hawa wanapata hamasa ya kufahamu kuwa michezo siyo tu burudani bali pia ni taaluma inayoweza kubadilisha maisha.
Kuna wafanyabiashara wakubwa wa Kitanzania kama Said Salim Bakhresa, na zamani hayati Reginald Mengi na wengineo.
Mifano yao inawafundisha watoto kuwa biashara inahitaji maono, bidii na uvumilivu. Siyo lazima kila kijana awe mwimbaji au muigizaji maarufu, bali anaweza kuwa mfanyabiashara, mhandisi au mvumbuzi na bado akapata heshima kubwa.
Shule zinapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuongoza mwelekeo wa watoto. Badala ya shule kuruhusu watu maarufu wanaojulikana kwa kuchafua maadili kuzungumza na watoto kwa kigezo cha umaarufu pekee, zinapaswa kuwa na utaratibu wa kualika watu wenye mchango wa kweli.
Mwalimu akimleta daktari bingwa, mwanasayansi, au hata mkulima anayefanikisha maisha kwa njia halali, watoto watajifunza kuwa kazi yoyote yenye uadilifu ni ya thamani.
Tujiulize
Hebu tujiulize, ni kwa nini shule zetu zisianzishe siku maalum ya kualika watu bora angalau kila mwezi au basi hata mara kadhaa kwa mwaka?
Waalikwe watu waliofanikisha jambo fulani la mfano. Inaweza kuwa ni mwanariadha kama Filbert Bayi, aliyewahi kuwa shujaa wa mbio duniani, au msanii aliyeonesha kuwa unaweza kuwa na msanii lakini ukabaki na heshima na kulinda utamaduni.
Wanafunzi wakisikia simulizi za maisha ya watu hawa, watajua kuwa mafanikio yanahitaji nidhamu na kujituma.
Kwa mfano, kijana mdogo wa kike akikutana na Anne Makinda, Spika wa kwanza mwanamke wa Bunge la Tanzania, atapata hamasa kwamba elimu na maadili vinamwezesha kufika mbali.
Hata mkulima wa kawaida anapofanikisha maisha yake kwa kujituma, ni mfano mzuri wa kuigwa.
Watoto wasipowekwa katika njia ya kutazama mifano bora, taifa litaishia kuwa na kizazi kinachoamini kuwa mafanikio ni kuwa maarufu tu bila kujali msingi wa maadili.
Ndiyo maana kuna haja kubwa ya kulinda masikio na macho ya watoto wetu. Wazazi wafuatilie ni nani anayefuatiliwa na watoto wao kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.
Walimu wasimamie mijadala darasani kuhusu nani ni kiigizo chema. Na vyombo vya habari navyo viwajibike kuonyesha zaidi simulizi za watu wenye mchango mzuri badala ya kuwapa nafasi kubwa wachafuzi wa maadili.
Kizazi cha kesho kitapimwa kwa misingi tunayotengeneza leo. Kama tutawalea watoto wanaowaiga wahuni kwa kigezo cha umaarufu, basi taifa litaishia kuwa na viongozi na wananchi wasio na heshima wala maadili.
Lakini tukiwapa watoto nafasi ya kufuata watu wenye mwelekeo sahihi, tutapata taifa lenye viongozi wachapakazi, waadilifu na wabunifu.
Watoto wetu wanahitaji mifano hai ya kuonyesha kuwa maisha mazuri yanajengwa na juhudi, heshima na uadilifu.
Wapewe nafasi ya kuwaona viongozi, wasomi, wafanyabiashara, wanamichezo na wasanii wenye maadili. Tukifanya hivyo, tutakuwa tumetengeneza taifa ambalo maadili siyo hadithi, bali mwongozo wa maisha ya kila siku.