Wazazi chanzo watoto kukacha elimumsingi
Muktasari:
- Changamoto inayotikisa sekta ya elimu kwa sasa ni ongezeko la wanafunzi wanaokatisha masomo kabla ya kufikia ngazi wanazopaswa kuhitimu.
Dar es Salaam. Katika miaka ya karibuni, Tanzania imeendelea kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha watoto wanapata elimu bila vikwazo, ikiwamo kuondoa ada na gharama nyingi zilizokuwa zikiwakwaza wazazi.
Hata hivyo, licha ya jitihada hizo, changamoto kubwa inayotikisa sekta ya elimu kwa sasa ni ongezeko la wanafunzi wanaokatisha masomo kabla ya kufikia ngazi wanazopaswa kuhitimu.
Tatizo hili linaonekana kuongezeka zaidi katika maeneo ya vijijini na jamii za wafugaji, ambako wazazi wengi bado hawaoni faida ya moja kwa moja ya kumpeleka mtoto shule.
Hivi karibuni Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) lilitaja kuwa wanafunzi 26,093 waliosajiliwa kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2025 hawakufanya mtihani huo.
Hilo lilionekana pia mwaka 2024 ambapo wanafunzi 25,875 waliosajiliwa hawakufanya mtihani huo huku hali ikiwa mbaya zaidi mwaka 2023 ambapo wanafunzi 40,901 walikacha mtihani huo.
Mbali na hao ripoti ya takwimu za elimu ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa iliyotolewa mwaka 2025 inaonesha mwaka 2024 wanafunzi 139,192 wa shule za msingi walikatisha masomo.
Kwa upande wa sekondari nako ripoti inaonesha mwaka 2024 wanafunzi 100,998 walikatisha masomo, idadi hiyo ikiwa ni upungufu wa asilimia 28.10 ya idadi ya waliokatisha masomo mwaka 2022 ambapo ripoti inaonesha walikuwa 136,313.
Wadau wa elimu wameonya tatizo hili wakieleza si tu linazalisha kizazi kisicho na ujuzi wala maarifa ya msingi, bali pia kinaathiri maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Taifa kwa ujumla.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Christian Bwaya anasema suala la wanafunzi kukatisha masomo, ni tatizo kubwa hasa kwenye jamii za wafugaji ikiwa ni matokeo ya wazazi kutoona thamani ya elimu.
Anasema hayo ni matokeo ya kushindwa kuifanya elimu itoe tafsiri ya moja kwa moja kwenye maisha ya watu, kwa sababu ilivyo sasa ipo kinadharia zaidi na sio vitendo.
“Kilichopo ni kwamba bado hatujaweza kuifanya elimu itoe tafsiri kwenye ustawi wa maisha ya watu. Mzazi anataka kuona manufaa ya moja kwa moja ya elimu.Hadi sasa bado kuna wazazi ambao wanaona kuliko kumpeleka mtoto shuleni ni bora amuingize kwenye shughuli za uzalishaji,’’ anasema na kuongeza:
“Kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaokatisha masomo tafsiri yake ni kwamba bado hatujaweza kuifanya elimu kuwa halisi kwenye maisha yao. Hii inafanya mzazi asione tija, tusiishie kwenye kuwalaumu au kuona suluhu kuwakamata tujikite kwenye kuwaelimisha umuhimu wa elimu na tija yake ionekane kwa vitendo tuache na zile nadharia kwamba akisoma atafuta ujinga.”
Mhadhiri huyo bobezi kwenye saikolojia, pia anasema ipo haja uelimishaji huo kufanyika kwa kuangalia tafsiri ya mafanikio katika jamii husika.
“Zipo jamii ambazo tafsiri ya mafaniko ni kuwa na mifugo mingi au mashamba makubwa, sasa wakati tunawaelimisha kuhusu umuhimu wa elimu, tunapaswa kuangalia tafsiri waliyonayo na namna ya kuwasaidia katika uelekeo wenye tija,” anasema Bwaya.
Kwa upande wake, Mkuu wa shule ya Moga Leonard Ntimba anasema tatizo limeanza kuota mizizi huku waathirika wakubwa wakiwa ni watoto kutoka katika shule za umma.
Anasema hilo ni matokeo ya kupungua kwa msukumo kwa wazazi kupeleka watoto shuleni licha ya Serikali kutekeleza mpango wa elimu bila ada.
“Msukumo wa kuwapeleka watoto shule umepungua kwa kiasi kikubwa tofauti na ilivyokuwa hapo awali, nafikiri kuna haja ya kuwa na sheria itakayosimamia vikali suala hili na wazazi wachukuliwe hatua. Serikali isiishie kusema elimu bure ichukue hatua kwa wazazi wanaoshindwa kuwafuatilia watoto kupata elimu.
“Nasema hivi kwa sababu siku hizi imekuwa si kitu cha ajabu kukuta watoto wenye umri wa kuwa shuleni wanazurura tu mitaani, wazazi hawana muda wa kufuatilia na naona hili suala la watoto kuelelewa na mzazi mmoja linazidi kuongeza, tatizo hakuna kabisa ufuatiliaji,”anasema Ntimba.
Ufuatiliaji ni tatizo
Mtaalamu wa elimu Dk Wilberforce Meena anaunga mkono hoja ya kukosekana kwa ufuatiliaji unavyochangia idadi kubwa ya wanafunzi wanaokatisha masomo yao.
Anasema tatizo hili linaonekana kuathiri zaidi wanafunzi wanaosoma shule za umma, ikiwa ni matokeo ya uhusiano hafifu kati ya walimu na wazazi.
“Nikitolea mfano wa Marekani mtoto asipoonekana shule hata kwa siku moja lazima taarifa ifike kwa mzazi wake, lakini kwenye shule nyingi za umma hapa nchini hali haiko hivyo; hakuna uhusiano mzuri kati ya wazazi na walimu.
“Hata hivyo sioni kama mfumo wa shule na walimu wanapaswa kulaumiwa katika hili kwa sababu hata wao wanazidiwa. Unakuta mwalimu mmoja ana wanafunzi wengi na anatakiwa kufundisha katika darasa zaidi ya moja sasa huyo atawezaje kumjua kila mtoto darasani na kama yupo au hayupo,” anasema.
Hata hivyo Dk Meena anawanyooshea kidole wazazi katika hilo, akieleza kuwa kwa kiasi kikubwa wanachangia suala la ufuatiliaji wa wanafunzi kuwa mgumu.
Tulifanya utafiti kuna familia ambazo hazina muda wa kufuatilia watoto. Unaweza kukuta hata walimu wanafanya jitihada za kuwaita kuzungumzia masuala yanayomhusu mtoto lakini mzazi haitikii wito. Wazazi hawana muda hata wa kushiriki vikao vya shule kujua maendeleo ya watoto wao.
Kuna watoto wanalazimika kuingia kwenye shughuli za kiuchumi ili kutafuta kipato kwa ajili ya kusaidia familia, mtoto wa aina hii hata asipoenda shuleni haiwezi kuwa tatizo kwa mzazi yeye ataona anasaidia kuendesha familia,” anasema na kuongeza:
‘’Wapo watoto ambao wanalelewa na bibi au mzazi mmoja, kundi hili lina changamoto zaidi inawezekana bibi hana hiyo nguvu ya kumfuatilia mtoto na maendeleo yake shuleni hivyo ni rahisi akaacha shule na asifahamu chochote au huyo mzazi yuko bize na shughuli za kutafuta kipato hana muda wa kufuatilia watoto.”
Anachosema mzazi
Ambangile Mwanyembe ambaye ni mmoja wa wazazi kutoka jijini Mbeya, anasema licha ya Serikali kutangaza elimu bur, zipo familia zenye kipato duni hadi kushindwa kumudu mahitaji ya wanafunzi, akiomba kuwapo mkakati maalumu kuwafikia wenye uhitaji.
Anasema kama wanavyofanya kwa elimu ya juu kwa kutoa mikopo, mpango huo unaweza kuifikia elimu ya msingi ambayo ndio muhimu zaidi kwa maisha ya binadamu katika shughuli za kila siku.
“Pengine naweza nisieleweke, lakini ukweli ni kwamba kuna wazazi na walezi kipato ni duni sana kumudu mahitaji ya wanafunzi. Niombe Serikali kwa dhamira yake ya elimu bure, mikopo au ufadhili uanze kwa shule za msingi ambapo elimu hiyo ndio muhimu zaidi,” anasema.
Athari ya hali hii
Dk Meena anasema hatari iliyopo ni Taifa kuongeza idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika hali inayotishia ustawi wa nchi.
“Hili haliishii tu kwenye masuala ya kitaaluma na kupata maarifa, kuna hatari kubwa ya kuwa na jamii ya watu waliokosa maadili. Ukifuatilia hawa watoto wanaoacha shule wanaenda wapi utagundua wengi wanaisha mitaani na kujiunga na vikundi visivyofaa,” anaeleza.
Mtaalamu huyo anashauri ziwepo afua mbalimbali za kuwasaidia watoto hao kwa kuangalia sababu zilizomfanya kila mmoja kuacha shule na hilo litawezekana endapo kutakuwa na mkakati wa kitaifa wa kuwatambua na kuwafuatilia.