Hashim Kambi: Umakini zaidi unahitajika katika uigizaji
Muktasari:
“Pia katika uigizaji, kwa siku unaweza kuigiza scene tano tu. Tofauti na hapa ambapo filamu nzima inaweza kuigizwa siku moja,”
Msanii mkongwe wa fani ya maigizo nchini, Hashim Kambi(49), amewataka waigizaji, waongozaji na watengenezaji wa filamu nchini kuongeza umakini wanapofanya kazi zao.
Akizungumza na Starehe, Kambi alisema kuwa umakini ndiyo utakaoziwezesha filamu za kitanzania kuwa na ubora unaokubalika kitaifa na kimataifa, tofauti na sasa ambapo nyingi zina makosa mengi tofauti na za wenzetu.
Msanii huyo ambaye hivi karibuni alikuwa nchini Ghana akiigiza filamu mpya inayofahamika kwa jina la Day After Death, ameielezea safari yake hiyo kuwa imemfunza mambo mengi na kugundua kwamba bado kazi kubwa inahitajika kuipeleka mbele tasnia ya filamu nchini.
“Kwenye filamu hiyo mpya nimeigiza na mwigizaji mwenye asili ya Ghana, Van Vicker, John Dumelo pamoja na Lidya Folson. Lakini sioni aibu kusema ni filamu yangu ya kwanza itakayokuwa na ubora wa kipekee,”alisema.
Alibainisha kuwa ubora wa filamu hiyo mpya umetokana na umakini aliokuwa nao mwongozaji wa filamu hiyo wakati wa kufanya kazi, pamoja na vifaa vya kisasa vyenye ubora wa hali ya juu.
Kambi alitaja baadhi ya mambo aliyojifunza nchini Ghana kuwa ni pamoja na kutenga muda wa kutosha katika maandalizi ya filamu akitoa mfano kuwa tukio ( Scene) moja linaweza kuchukua zaidi ya saa mbili za maandalizi.
“Pia katika uigizaji, kwa siku unaweza kuigiza scene tano tu. Tofauti na hapa ambapo filamu nzima inaweza kuigizwa siku moja,” alisema Kambi na kuongeza:
“Kingine kinachokosewa katika filamu zetu ni tafsiri isiyo sahihi ya maneno ya kiswahili yanayozungumzwa. Bora waandaaji wasingeweka maneno ya Kiingereza kama tafsiri ya filamu zao, kwani kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakichangia kudharaulika kwa filamu zetu.”
Kambi alisisitiza kuwepo kwa haja ya kurudi shuleni kwa waigizaji wa filamu na kusomea kazi hiyo, vingevyo fani hiyo haitaweza kupiga hatua.
“Pia ni vyema tukakubali kuwa hatujui Kiingereza, hivyo tukisomee zaidi ili tuweze kukitumia kwenye kazi zetu za kila siku,” alihitimisha.