Hekaya za Mlevi: Mama zetu sio mitambo
Muktasari:
- Lakini katika wakati huu wa teknolojia tumeshtukia kuwa wazee hawa walikuwa wakimlinda mama kutobeba mtoto mkubwa kiasi cha kusababisha uzazi kwa njia ya upasuaji, ambao haukuwepo. Matokeo yake kuwa ni mmojawapo; aidha mama au mtoto kupoteza maisha
Dar es Salaam. Nilikuwa na rafiki yangu aliyeumbwa na kichwa kisichoota nywele. Kwa imani za zamani, wazee wangesema mama yake alikula mayai wakati wa ujauzito wake!
Lakini katika wakati huu wa teknolojia tumeshtukia kuwa wazee hawa walikuwa wakimlinda mama kutobeba mtoto mkubwa kiasi cha kusababisha uzazi kwa njia ya upasuaji, ambao haukuwepo. Matokeo yake kuwa ni mmojawapo; aidha mama au mtoto kupoteza maisha.
Rafiki yangu kipara alikuwa tofauti na vipara wenzake. Kila siku alipotoka kazini ilikuwa ni lazima aweke kituo kwa kinyozi. Siku za Jumapili alishinda huko akikinyoa kipara chake toka asubuhi mpaka jioni.
Vinyozi walishamzoea hivyo hakuwasumbua; kila aliposema “bado” walimpitishia mashine ya kunyolea kichwani na kumpaka mafuta kipara king’are, kisha wakampa gazeti asome wakisubiri “bado” nyingine. Utafikiri alitamani angezaliwa bila kichwa!
Baadaye tuligundua kuwa tatizo la rafiki yangu lilikuwa hisia zake tu. Ni kwamba alizichukulia nywele kama uchafu, alizihisi kabla hajaziona. Fikiria gari likitimba kwenye dimbwi la kinyesi kando yako, hata kama kilikukosa hutakuwa sawa.
Ni lazima utarudi nyumbani, utaoga sana, utabadilisha nguo na kujipulizia uturi mwingi. Lakini pamoja na yote hayo, bado utaihisi harufu mbaya kila utakapokaa. Kumbe ni hisia tu zinazokuendesha.
Mama watoto wangu ana wenge kama hilo. Hata nyumba isafishwe na wataalamu wa usafi, yeye ataiona chafu. Mimi namchukulia kama mwenye uraibu wa usafi, maana atarudia kuosha kwa sabuni kikombe kilichooshwa kwa sabuni ileile na muda uleule.
Wakati mwingine huwa tunagombana anapoziona hata zana zangu za kazi kuwa uchafu. Mwaka juzi nilipata fursa ya kufanya utafiti. Alikusanya makaratasi yangu ya utafiti na kuyachoma moto. Nilikasirika zaidi ya uwezo wangu, lakini mwenzangu alinicheka tu akiniona mchafu.
Inawezekana kuwa hii ndiyo silika ya mama zetu. Siku moja nilienda kwenye maonesho ya Kimataifa ya Mwalimu Nyerere, maarufu kama Sabasaba. Nikapita kwa mlinzi mwanaume aliyenizungushia kifaa cha ukaguzi kutoka kichwani mpaka miguuni.
Aliporidhika akaniruhusu. Siku ingine nilikutana na mlinzi mwanamke. Kwanza aliniamuru kutoa vitu vyote mifukoni mwangu, ikiwemo leso. Akaniskani mwili mzima, kifaa chake hakikuonesha ishara yoyote. Hakuridhika, akaniamuru nivue kofia. Niliogopa sana kwani nilihisi ambacho kingefuata ni kuvuliwa nguo!
Hapo nikagundua kitu: mwanamke akipewa jukumu, hulifanya kwa umakini wa hali ya juu. Tatizo si uwezo wao, ila ni jamii kupenda kuwaongezea kazi kila wanapoonesha wanaweza.
Leo mama ni mlezi, mfanyakazi, mjasiriamali, mshauri wa ndoa, mwalimu wa nyumbani, daktari wa kwanza wa familia, bado unamweka kuwa fundi wa umeme wa dharura, mjenzi, dereva wa malori na bondia wa kulipwa. Atamudu kuzaa na kulea watoto wangapi?
Kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, wanaume wanaonekana kuelemewa na uzito wa mahitaji ya familia. Kutokana na hali hii, wanawake wamekuwa msaada mkubwa kwa waume zao.
Wamekuwa wakijitoa kupitia vikundi vyao vya kuchangishana, kilimo na ujasiriamali. Wakati mwanaume anajadili mpira na siasa, mwanamke anajadili bei ya mbolea, soko la nyanya na mkopo wa kikundi. Ukimkuta anafurahi ujue hesabu zake zimekaa sawa; ukimkuta akiwa na huzuni ujue rejesho halijatimia.
Wanawake hivi sasa wana fursa nyingi za mafunzo kupitia taasisi mbalimbali. Ni jambo zuri kwani huenda linawakwamua kuondokana na utegemezi. Lakini swali linabaki: je, haya yanapunguza mzigo au yanaongeza? Mama anaamka saa kumi alfajiri.
Anaandaa watoto, anaandaa kifungua kinywa, anakimbia kazini, anarudi jioni, anaendelea na biashara ndogo, anasimamia kazi za shule, kisha usiku anaandaa mpangokazi wake wa kesho. Huyu ni binadamu au mashine ya kiwandani?
Lakini si vema wakafanya kila kazi zinazofanywa na wanaume. Tukumbuke kuwa wanawake pekee ndio waliojaliwa uzazi na ulezi wa watoto. Hili si jambo rahisi kwao. Tukiwaongezea majukumu mengine chungu nzima wanaweza kupunguza uwezo wao.
Ni sawa na kumpa dereva gari, pikipiki na baiskeli kwa wakati mmoja, halafu unasubiri hesabu ya kila chombo saa ilitimu.
Nadhani kuwaongezea akinamama uwezo kunashabihiana na kuachiwa malezi ya watoto peke yao. Hii inasababishwa kwa ukubwa na hali mbaya ya uchumi kwa wanaume.
Hapa ndipo dhana ya mwanamke kumsaidia mumewe inapojengeka. Lakini msaada usigeuke kuwa mzigo wa kudumu. Tuyarejee maandiko na tamaduni za waliotutangulia kwa huyu mwanamume kutimiza wajibu wake.
Ipo haja ya kuwaongezea wanaume fursa za kazi za kiufundi, sambamba na ujuzi wa kazi nyepesi kwa wanawake. Si kwa lengo la kugawanya kwa ubaguzi, bali kwa mizani ya haki.
Kama tulivyogundua tatizo la rafiki yangu kipara nywele bali hisia zake, nasi tujifunze kuwa tatizo si uwezo wa wanawake, bali namna tunavyogawa majukumu. Tusije tukaandaa Taifa lisilo na vizazi hapo baadaye.
Mwisho wa siku, familia ni timu. Ukimpa mchezaji mmoja majukumu yote, atachoka na timu itapoteza. Labda si wanawake wapunguziwe majukumu kwa sababu hawawezi, bali kwa sababu wanafanya mengi kuliko tunavyokubali.
Na kama tutashindwa kuliona hilo, basi tutabaki kama rafiki yangu tukinyolea tatizo juu juu, huku chanzo kikiwa bado kichwani. Kuna mtu aling’oa meno yote kabla hajagundua kuwa tatizo lilikuwa ufizi!