Alama 11 za mpenzi asiye mwaminifu

Muktasari:

  • Sasa hembu fikiri unamkuta mpenzi wako ametokea na ana harufu ya tofauti kabisa na uliyoizoea, yamkini umeisikia harufu hiyo akiwa amerudi toka kazini wakati asubuhi alipoondoka alikuwa na harufu ile uliyoizoea.

Kwa kuwa wapendanao huwa wamezoeana, mara nyingi hata aina ya manukato mmoja anayotumia yanakuwa yanajulikana kwa mwenzake, hata kama mmoja hajui jina la manukato anayotumia mpenzi wake lakini basi atajua walao jinsi yanavyonukia.

Sasa hembu fikiri unamkuta mpenzi wako ametokea na ana harufu ya tofauti kabisa na uliyoizoea, yamkini umeisikia harufu hiyo akiwa amerudi toka kazini wakati asubuhi alipoondoka alikuwa na harufu ile uliyoizoea.

Najua hali hii inaweza kuwa na sababu zinazoeleweka lakini maranyingine ni ishara ya kuashiria kutokuwepo na uaminifu baina ya mpenzi mmoja.

Mara nyingine sio harufu bali michubuko katika maeneo fulani ya mwili ambayo hayana maelezo fasaha yalikotokea, iko michubuko mingine ambayo inajieleza na kutia shaka zaidi.

Yawezekana ni mpenzi wa kiume lakini unamkuta na ishara za rangi ya midomo kwenye nguo au mwilini, sidhani kama na hapa bado maelezo yake yataingia akilini kiurahisi.

Tabia za kuanza kukufuatilia sana au hata kukuganda:

Nimeshawahi kuwa na mazungumzo na watu wa jinsia ya kike waliokuwa kwenye mahusiano ambapo wanaume wao walikuwa hawawaachi, watawapeleka kila wanakotaka, na kutoruhusu mazingira ya wapenzi hawa wa kike kuwa huru kufanya mambo yao wenyewe, wengine waliitafsiri hali hii kama penzi kubwa sana, yuko aliyeniambia “mpenzi wangu ananipenda sana, yani hawezi niache mwenyewe, kila sehemu anataka niende naye” baada ya muda mtu huyu aligundua kuwa ile ilikuwa ni ujanja wa kuficha uhalisi wake na kuzuia mazingira ya mpenzi wake wa kike kugundua au kupewa taarifa za tabia zake, na kwa muda mrefu hakugundua mpaka siku alipo pata taarifa za ukweli na ukawa mwisho wa mahusiano yao, tena mwisho wenye uchungu sana. Kuwa macho sana na tabia za mpenzi wako kukuchunguza sana unapotoka, ulipokuwa, ulikuwa nanani, mlifanya nini, nani alikuwepo mwingine, unaenda wapi, kwa muda gani. Yawezekana yote hii ni hali ya kujilinda au kujihisi dhambi inayomsumbua.

Mabadiliko katika tendo la ndoa

Jambo hili laweza kujidhihirisha katika picha mbili tofauti. Kwa kawaida wapenzi huwa na mazoea fulani katika tendo la ndoa, kwa muda waliokaa pamoja kila mmoja humfahamu mwenzake kwa kiasi fulani. Inawezekana likawa jambo la kushangaza pale ambapo ghafla unamuona mpenzi wako anapoteza kabisa hamu ya tendo la ndoa, au hata mnapokuwa katika tendo hilo humuoni akifurahia bali anakuwa kama anayelazimishwa au kutohamasishwa na chochote. Kwa upande mwingine unaweza ukakuta mpenzi wako anakuja na ujuzi wa ghafla katika mahusiano yenu ya tendo la ndoa, hali yake ya kukutamani inazidi ghafla, anahitaji mapenzi mara kwa mara na hata mnapokuwa katika tendo hilo anadhihirisha utaalamu wa tofauti na ule uliouzoea. Hali hizi mbili zifanyike tahadhari katika kukusaidia kuyatazama mahusiano yenu.

Marafiki wa mpenzi wako kukukwepa:

Ni hali ya kawaida kuwa karibu au kuzoeana na marafiki wa mpenzi wako, mara nyingine mtawasiliana nao kutaka kujua aliko mpenzi wako au kinachoendelea kwao. Inabidi ujiulize sana pale inapotokea ghafla wale marafiki wa mpenzi wako uliowazoea, uliokuwa unawapigia simu wakati wowote leo wana kukwepa, na hata simu hawapokei na mara nyingine wakipokea hawakupi taarifa yakueleweka au wanakudanganya. Hii yote inawezekana wanamlinda rafiki yao, au wanakosa cha kujibu maana wanajua uhalisia wa kinachoendelea.

Kuzungumza sentensi za kutatanisha:

Kama nilivyosema awali, wapenzi wengi hujuana kwa mengi, ikiwemo pia namna ya kuzungumza au kuonyesha hisia. Unaweza kukuta katika mapenzi yenu mpenzi wako anaanza kuwa na sentensi ngumu na zisizo kuwa na msingi kwa mfano anasema “ kwa jinsi hii sidhani kama tutafika” “mi siamini kama mapenzi yanadumu” “yaani ndio maana watu wanashindwa kukaa na mpenzi mmoja” na mara nyingine anaweza kukuuliza baadhi ya maswali moja kwa moja ili kukuona utajibuje. Sentensi hizi zina chanzo moyoni, kuwa macho.

Kuzidi kwa tabia za kutoonekana au kuponyoka:

Yawezekana mpenzi wako alikuwa na tabia ya kuwepo nyumbani mida isiyokuwa ya kazini au wikiendi, muda mwingi alipenda kuwa na wewe na akiaga basi atasema anakwenda wapi na akimaliza hurudi mapema kwa sababu ana kiu ya kuwa na wewe, mara ghafla sikuhizi haagi anakwenda wapi, ukiuliza inaweza kuwa vita. Anakuwa na vijisafari vingi na vijisababu visivyoisha vya kumuwezesha kuponyoka. Sehemu ya kwenda na kurudi saa moja anaweza kuchukua nusu siku, kila ukiuliza atakwambia nakuja, niko njiani, kuna foleni, nimekwama, na sababu nyingine nyingi sana. Ukiona haya yanazidi ujue kuna la zaidi ya foleni, na hizo sababu zote zinazotolewa zinafunika jambo.

Tabia za kuficha fedha:

Ninafahamu fika kwamba suala la uwazi katika mambo yanayohusiana na fedha na matumizi ni tatizo kubwa kwa wapenzi wengi, wengi wamegombana na hata kuachana kuhusiana na jambo hili. Japokuwa hili ni tatizo kwa wengi lakini wako wapenzi ambao wamekuwa na tabia ya kuambiana kwa uwazi matumizi na mapato yao, hakuna kitu wamefanya kuhusu fedha zao pasipo kuambiana na hivi ndivyo mlivyozoeshana, mara ghafla mmoja anaanza kuwa na siri kuhusu fedha zake au matumizi yake, na wala hapendi kuulizwa ulizwa kuhusu suala hilo. Tabia hii ikidhihirika katika mapenzi yenu usichelewe kuchunguza maana kwa kukaa kimya unaweza kujikuta umechelea mwana na maji ya moto.