ANGEL CLIFF: Msomi wa Makerere aliyerudi nchini na kufanya kazi ya upagazi

Septemba 28 nilibahatika kuwa mmoja wa waandishi waliopanda mlima Kilimanjaro katika kampeni ya ‘Twenzetu Kileleni’.

Kampeni hiyo iliratibiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamis Kigwangalla kama moja ya njia ya kuhamasisha utalii wa ndani.

Katika safari hiyo mbali na waandishi wa habari, Waziri huyo aliambatana na wasanii zaidi ya 25 wa Bongofleva na wale wa filamu, tukio lililokuwa likifuatiliwa na watu wengi.

Kati ya mambo yaliyonivutia katika safari hiyo ni kukutana na wapagazi wa kike wakifanya kazi hiyo kwa makini.

Nilizungumza na mmoja wao aliyejitambulisha kwa jina la Angel.

Kazi ya Angel kama walivyo wapagazi wengine kwenye eneo hilo la Mlima Kilimanjaro ni kuwasaidia watu wanaopanda mlima (mimi nikiwemo), kuwaongoza na kuwabebea mizigo.

Katika mazungumzo yetu alijinasibu kuwa na uwezo wa kupanda mlima huo na kushuka ndani ya siku tatu.

Anasema alianza kuupanda mlima huo mwaka 2015 baada ya kumaliza kidato cha sita na hii ni baada ya familia yake kushindwa kumuendeleza chuo pamoja na kufaulu vizuri masomo yake.

“Niliona hakuna uwezekano wa familia yangu kunisomesha mpaka chuo japo nilifaulu vyema, hivyo nilipanda mlima ili nipate fedha za kujisomesha.

Anasema kabla ya kuwa mwongozaji alianza kupanda mlima huo kama mbeba mizigo akiwa anafanya kazi na kampuni ya utalii ya Asante.

“Mwanzoni nilikuwa ninawashangaa wanawake waliokuwa wakifanya kazi hiyo bila woga wala kuchoka, nikaapa kufanya vema zaidi yao na nimefanikiwa kulitimiza hilo,” anasema.

Anasema alifanya kazi Asante kwa muda wa miezi mitatu na baadaye alipata kazi katika kituo cha kulea watoto na wazee kiitwacho ‘ Share Tanzania’, kilichopo mkoani Moshi, alifanya kazi hapo mwaka 2015 hadi 2016.

“Nilifanya kazi vizuri kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi mitatu, mwajiri wangu aliniuliza anifanyie nini kama zawadi.

“Nikamwambia nataka kujiendeleza kielimu, akanilipia ada ya kusoma Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda,” anasema.

“Mwaka 2017 alinilipia na nikajiunga na chuo hicho nikisomea Mahusiano ya Kimataifa, mwaka 2019 nikiwa mwaka wa tatu nililazimika kukatiza masomo yangu na kurudi nyumbani baada ya kukosa ada na mahitaji mengine muhimu,” anasema.

Anafafanua hilo lilitokea baada ya mfadhili wake kuumwa na kushindwa kumlipia ada.

“Hivyo ikabidi nirudi kuendelea na kazi yangu ya kupanda mlimani ili kukusanya fedha zitakazonisaidia kurudi kumalizia mwaka wa mwisho na ninashukuru kampuni ya Asante ilinipokea,” anasema.

Changamoto

Matatizo yanayowakuta watu wanaopandisha watalii mlimani yapo mengi ikiwemo wanaowapandisha kupata matatizo mbalimbali kama kukosa hamu ya kula hususani unapokaribia kileleni.

Anasema hali hiyo hata wao licha ya kupanda muda mwingi huwatokea pia.

“Mtu akiwa juu hamu ya kula inapotea, kunywa maji jambo ambalo si zuri kwani katika kupanda mlima unatakiwa kunywa maji mengi na kula chakula cha kutosha kwa kuwa unapoteza nguvu nyingi.

“Katika hili kuna wasiofuatilia hivyo wanapatwa na magonjwa na wasiovaa nguo za kujikinga na baridi, wengi uhadaika na jua kumbe mlimani hata kama linawaka inabidi uvae nguo hizo.

“Mara nyingi husumbuliwa na maradhi ya kichwa kuuma, kutapika, damu kutoka puani, maji kujaa kwenye mapafu kutokana na ukosefu wa hewa ya oksijeni.

Anafafanua njia pekee ya kujiokoa na hali hiyo ni kula na kunywa maji kwa siku kuanzia lita tatu hadi tano.

Wito wake kwa kina dada ni kuwa hakuna kazi ya mwanaume wala mwanamke wanapaswa kuelewa kazi zote zinaweza fanywa na jinsia zote mbili.

Kuhusu wapagazi wanawake kutongozwa na wageni alisema kutokana na hali ya hewa na mazingira magumu ya upandaji mlima jambo hilo ni gumu kutokea.

Malengo

Moja ya mambo ambayo angependa kuja kufanya katika maisha yake, anasema ni pamoja na kutoa msaada kwa nchi zile zinazokumbwa na majanga kama njaa, vita nk.

‘Kama nilivyosema chuo cha Makerere nasomea masuala ya Mahusiano ya Kimataifa, kazi inayoendana na kutoa msaada wa kibinadamu kwa nchi zilizokumbwa na machafuko, hivyo lengo langu ni kuona hilo nalifanikisha siku moja katika maisha yangu.

“Huwa naumia ninavyoona wazee, kina mama na watoto wanavyopoteza maisha na kujeruhiwa katika machafuko huku wakikosa msaada, ”anasema.

Alikotokea

Angel alizaliwa miaka 26 iliyopita Machame, Kilimanjaro na kusoma Shule ya Msingi Kisereni, Moshi kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari Nkuu na kumaliza kidato cha nne mwaka 2010.

Mwaka 2012 kutokana na matatizo ya kifamilia, alimfuata mama yake aliyekuwa Uganda na kusoma huko kidato cha tano na sita na kumaliza 2014 na mwaka 2015 akarejea tena nchini kutafuta maisha na alipata kazi katika shirika la Share Tanzania’ ambalo mwaka 2017 lilimdhamini kwenda kusomea masuala ya Uhusiano wa Kimataifa Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda.