ANTI BETTIE: Acha kulalamika mwenza wako kupungua nguvu za kiume, pambana kuzirudisha

Muktasari:

  • Neno hana nguvu za kiume si geni tena masikioni mwa watu, ni kama tusi jipya kwa wanaume. Ajabu maswali mengi kuhusu hii hali wanaoniuliza ni wanawake: “Mwenza wangu hana nguvu za kiume nifanyeje?...Mwenza wangu hana nguvu za kiume sidhani kama tutazaa....Mwenza wangu hanitoshelezi kutokana udhaifu wa maumbile yake...”

Neno hana nguvu za kiume si geni tena masikioni mwa watu, ni kama tusi jipya kwa wanaume. Ajabu maswali mengi kuhusu hii hali wanaoniuliza ni wanawake: “Mwenza wangu hana nguvu za kiume nifanyeje?...Mwenza wangu hana nguvu za kiume sidhani kama tutazaa....Mwenza wangu hanitoshelezi kutokana udhaifu wa maumbile yake...”

Ilimradi wanawake wanatafuta suluhisho la wenza wao kukosa nguvu za kiume. Karibu wote wanaouliza swali hili hakuna aliyekwenda kwa daktari na mwenza wake kupima na kuelezwa kuwa mwenza wake ana upungufu wa nguvu za kiume.

Nilichobaini wanaposema upungufu wa nguvu za kiume wanamaanisha ile hali ya mwanamume kutumia muda mrefu kushiriki nao tendo la ndoa. Wanamaanisha siyo kwamba hawezi kabisa kushiriki hapana, wanataka ashiriki nao zaidi ya kawaida.

Hakuna aliyeniambia juhudi walizofanya hata za kimaumbile kulithibitisha hili, kibaya zaidi kuna waliofunga ndoa zaidi ya miaka 10 iliyopita, nao wanalalamika wenzi wao wamebadilika tofauti na walivyokuwa zamani, uwezo wao wa kushiriki umepungua inawezekana wanatoka nje ya ndoa.

Tukubaliane kutokubaliana wanandoa wakiishi muda mrefu inafikia mahali wanaonana wa kawaida, hili linapunguza hamasa ya mapenzi.

Hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anakuja na mbinu mpya kulisisimua huba. Kama mlikuwa mnashiriki tukio kwa miaka mitatu mfululizo nyumbani jaribuni kwenda hotelini au kijijini kwenu mkalifanye katika nyumba za tembe, linaweza kuwa na msisimko wa kipekee.

Maudhi, si rahisi kila kukicha unamtukana mwenza wako kwa sababu mbalimbali halafu unategemea ukikutana naye atakuwa sawa kama ulivyokuwa mnyenyekevu.

Humpikii vyakula vya kujenga mwili na kuupa nguvu, anakula vyenye mafuta mengi, hubembelezi aache kuvuta sigara, unakunywa naye pombe hadi mnakuwa chakari, halafu kesho unataka akupe shoo ya uhakika. Si rahisi.

Mwenza ana umri mkubwa, mmekaa katika ndoa kwa zaidi ya miaka 10, unataka akupe machejo ya ujanani haiwezekani, wakati huu atakuwa mtu mzima na pengine pumzi imepungua, nenda naye taratibu.

Kabla hujalalamika mumeo kukosa nguvu za kiume, jitume sana mnapokuwa faragha kuhakikisha anasisimka, ukimsisimua mara moja na kumuacha, hataweza kukupa unachotaka. Onyesheni ushirikiano.

Muhimu wazoesheni wenza wenu tabia ya kupima afya zao, mtu hawezi kuwa na ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu, msongo wa mawazo halafu akakupiga tukio la kukata na shoka.