BDOZEN : Ni zaidi ya mtangazaji
Hamisi Mandi a.k.a 'Bdozen'
Muktasari:
Bdozen anajulikana sana kwa uendeshaji wa kipindi cha Extra Extra Large, maarufu kwa jina la XXL. Amekuwa akifanya kazi hiyo kwa takribani miaka 11, lakini pia si kazi ya utangazaji pekee inayomuweka mjini; ni mmiliki wa duka la nguo la Born To Shine lilipo Mwenge jijini Dar e salaam.
Ukizungumzia watangazaji maarufu ambao wanakubalika kwa ubora wa kazi zao, hutaacha kumtaja BDozen wa Clooud FM.
Bdozen anajulikana sana kwa uendeshaji wa kipindi cha Extra Extra Large, maarufu kwa jina la XXL. Amekuwa akifanya kazi hiyo kwa takribani miaka 11, lakini pia si kazi ya utangazaji pekee inayomuweka mjini; ni mmiliki wa duka la nguo la Born To Shine lilipo Mwenge jijini Dar e salaam.
Hajaishia hapo, Bdozen anatumia kipaji chake cha sauti kutengeneza matangazo ya redio, kuwa mshereheshaji wa sherehe na matamasha na pia taswura yake hutumiwa na kampuni tofauti kutangaza bidhaa.
“Kitu kizuri hujiuza,” anasema Bdozen alipozungumza na Johari.
“Hiki ni kitu ambacho wasanii wengi wanakisahau. Mimi nathamini sana kipindi changu na huwa napenda kila kazi bora isinipite. Kazi ambayo haina ubora lazima niipotezee.”
Kazi ya utangazaji
Pamoja na kufanya kazi ya ushereheshaji kwenye matamasha na sherehe, Bdozen si mtu wa kujichanganya sana na huonekana kama anajitenga.
“Watu hunifikiria tofauti na nilivyo,” anasema.
“Mimi ni mtu mwenye aibu sana. Mara nyingi kama mtu simjui vizuri inanipa wakati mgumu kutoa ushirikiano kutokana na kuwa huwa najishtukia. Sio kama najitenga ila udhaifu wangu unasababisha watu kunidhania ndivyo sivyo. Lakini kwa wanaonijua vizuri, wanajua mimi ni mshikaji sana.”
BDozen amesema kuajiriwa na Clouds FM ni kitu ambacho hatakisahau kutokana na kuwa ni redio ambayo ilikuwa katika ndoto zake.
“Nilifurahi sana nilipopata kazi ya utangazaji Clouds FM. Nilikuwa naipenda sana na nilikuwa najifikiria kuwa tofauti na nilivyokuwa endapo ningefanya kazi katika hiki kituo.
Leo ndoto yangu imetimia na inanipa furaha milele,” anakiri.
Kipindi cha XXL kiliwahi kuhusishwa na ugomvi baina ya watangazaji na kuna picha zilienezwa mitandaoni kuonyesha viti vilivyovunjika baada ya ugomvi huo.
Lakini BDozen anasema hakuna kitu kama watangazaji kupigana wakiwa kwenye kipindi.
Anasema hicho kilikuwa kituko kilichopangwa katika mpango maalum wa Clouds FM kuhamasisha amani.
Jina la BDozen
BDozen, ambaye jina lake halisi ni Hamisi Mandi, ametoka mbali na jina hilo la kisanii.
Wengi wanaweza kuwa wanamkumbuka B12. Huyo B12 ndiye huyu BDozen, yaani kilichobadilika ni kuitaja namba 12 kwa jina badala ya tarakimu.
“Jina hili la sasa nimepewa na watu wawili tofauti;marehemu (mwanamuziki) Albert Ngwea na Gardner Habash (mtangazaji wa EFM ambaye zamani alikuwa Clouds FM).
“Gardner alianza kunipa jina la B12 akiwa na maana ya kwamba anakubali uwezo na pancha zangu katika utangazaji. alidai nina nguvu kubwa kama ilivyo vitamin B12,” anasema.
“Albert Mangwea aliongeza ladha kwa kutafsiri 12 kama seti ya vitu 12 ambayo inatambulika ‘dozen’ ndo nikaanza kuitwa Bdozen.”
Utangazaji kazi
Pamoja na kuwa na kazi tofauti zinazompatia kipato cha ziada, BDozen anaukubali utangazaji.
“Nimenufaika sana kwa kazi ya utangazaji lakini simaanishi kuwa natamani kuzeekea katika utangazaji,” anasema.
“Nina mipango ya kufanya mambo mengine kadri umri utakavyoruhusu kuachana na utangazaji.”
Anasema Bdozen wa miaka mitano iliyopita alikuwa ni mtu ambaye hana mototo, asiye na majukumu mengi, hakuwa anamiliki duka, lakini wa sasa ni tofauti.
Kwa mujibu wa BDozen, ndani ya miaka 11 amekuwa akitegemewa na watu tofauti na kwamba wasanii wa muziki ndio wanaoongoza kati ya hao.
Imani ya wasanii, kwa mujibu wa BDozen, ni kuwa anaweza kuwasaidia kujulikana na hivyo kufanikiwa kimaisha.
Lakini wasanii haohao ndio wanaomlaumu kuwa ana upendelea katika kutumia kazi za wasanii kwenye kipindi anachoendesha.
Lakini anaamini kuwa hana tabia hiyo bali ni tafsiri ya watu.
“Ubora wa kazi ndio unamfanya atambulishe kazi kadhaa na kuacha nyingine,” anasema.
“Wasanii wengi wanadhani kujulikana na kupata mafanikio katika maisha ni kitu rahisi. Si hivyo. Utafutaji unahitaji moyo wa ziada, kujituma, ubunifu na unyenyekevu ndio chachu ya mafanikio,” anasema.
Ushauri kwa wasanii
BDozen alizaliwa Julai 22 na siku hiyo huisherehekea kwa njia tofauti. Mwaka huu aliamua kusherehekea siku hiyo kwa kuwakumbuka watoto yatima.
Mwaka jana alifanya kitu kingine. Alikwenda gerezani kumsalimia Kajala na kumtakia siku nje ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa kuwa wawili hao wamezaliwa siku moja.
“Nakumbuka mwaka jana siku kama ya leo uliacha kazi zako zote ukaja Segerea kuni wish happy birthday siwezi kukusahau kwa hilo nakutakia bday njema.
Mungu azidi kukupa nguvu ufike miaka mingine 10000,” aliandika Kajala kwenye ukurasa wake mtandaoni.