Dalili na suluhisho la fangasi

Muktasari:

  • Kwa kawaida, uchafu huu haumbatani na harufu yoyote isipokuwa panapokuwa na tatizo la ziada kama ugonjwa wa zinaa.

Laiti kama wengi wetu tungekua na utamaduni wa kufahamu dalili na viashiria na kufika mapema katika huduma za afya basi maradhi mengi yangeepukwa.

Dalili za awali ni pamoja na sehemu ya uke kuwasha, kuwaka moto, kutoka vidonda, kupata maumivu wakati wa tendo, muwasho wa kuaibisha sehemu za siri, kuhisi kuwaka moto katika tupu na kutoka vidonda.

Dalili zingine ni pamoja na maumivu au usumbufu wakati wa kujisaidia haja ndogo, kuvimba na kuwa rangi nyekundu kwa mashavu ya ndani na nje ya uke.

Kutokwa na uchafu wa rangi nyeupe au kijivu, unaoweza kuwa mwepesi, majimaji au mzito na ambao umefanana na jibini wenye muonekano kama maziwa ya mgando.

Kwa kawaida, uchafu huu haumbatani na harufu yoyote isipokuwa panapokuwa na tatizo la ziada kama ugonjwa wa zinaa.

Uchafu huu unaotoka hapa unaweza kuenea kwenye maeneo mengine yaliyokaribu na tupu ya mwanamke kama kwenye mitoki na kusababisha kuharibika kwa ngozi katika sehemu hizo.

Uchunguzi wa maambukizi haya huanzia kwa mgonjwa mwenyewe kutoa historia nzima ya dalili alizonazo.

Baaada ya hapo ndipo daktari atakapofanya uchunguzi wa kimwili katika eneo la uke, jambo hili hufanya kwa kuzingatia maadili na huweza kubaini na kutofautisha na maradhi mengine ya ukeni.

Mhudumu wa afya atakueleza na kukuelimisha namna ya uchunguzi wa maeneo haya na huku akifanya mazingira yawe ya siri.

Mhudumu huvaa vifaa vya kujikinga na kukukinga na vimelea vya maradhi, baada ya kukulaza na kukuandaa atatumia vidole vyake viwili yaani cha shahada na cha kati kuingiza katika uke kwa ajili ya uchunguzi.

Ifahamike kufanya hivi si udhalilishaji bali ni uchunguzi rahisi na waharaka kubaini matatizo mbalimbali ya kinamama, hivyo ni muhimu sana kumpa ushirikiano mhudumu wa afya.

Matabibu kuweza kubaini uambukizi ulivyo na pia endapo kuna dalili za uvimbe, kubaini uwepo maumivu wakati wa kujamiana, kuangalia kama kuna uchafu wowote unaotoka, wingi wake, rangi yake, harufu yake, uzito wake (mwepesi, majimaji au mzito), na aina ya uchafu unaotoka kama ni sahihi kutokana na maelezo ya mgonjwa au ni tofauti.

Kuangalia kama sehemu ya siri ipo kawaida, kuangalia kama kuna uvimbe/mitoki wowote wa tezi, kuangalia maeneo yote ya uke na njia ya haja kubwa.