Prime
Dk Kijo Bisimba: Wazazi wa miaka hii wanachoka sana

Maisha ya kustaafu
Baada ya kufanya kazi kwa miaka 41 katika kada mbalimbali, ikiwemo ualimu, sheria na asasi za kiraia hatimaye mwaka 2018 Dk Hellen alihitimisha safari yake ya utumishi wa umma na kustaafu rasmi.
Miongoni mwa vitu ambavyo anakiri hakujiandaa navyo ni maisha baada ya kustaafu, kutokana na hilo, Dk Hellen anawasisitiza vijana walioko kazini kujiandaa kwa ajili ya maisha yao ya baadaye.
Anasema katika miaka yote aliyofanya kazi hakuwahi kufikiria kuandaa maisha yake baada ya kustaafu, jambo lililomfanya hata asiwe na mpangilio mzuri wa matumizi ya fedha alizozipata baada ya kuhitimisha maisha yake ya ajira.
“Kiukweli sikuwa nimeandaa maisha baada ya kustaafu, kosa ambalo sitaki vijana waliopo kazini kwa sasa wafanye, naona huko serikalini huwa wanapewa semina za mwezi mmoja kabla ya kustaafu, kiukweli hiyo haisaidii, mtu anatakiwa kuanza kujiandaa kuishi maisha ya ustaafu mapema akiwa kazini.
“Binafsi sikuwa na elimu ya uwekezaji, akili na nguvu yangu yote ilikuwa kwenye kazi, hivyo hata ilipotokea nimestaafu nikapewa pesa zangu niliona siwezi kuanzisha kitu ambacho sina uzoefu nacho, hivyo nilitumia zile pesa kidogokidogo hadi zikaisha,” anasema Dk Hellen na kuongeza;
“Niliwahi kupata fedha nyingi za mafao wakati huo nilikuwa naenda kufanya PhD Uingereza, mtoto wangu wa mwisho alikuwa amemaliza kidato cha sita, nikaona niende naye akasome digrii ya kwanza, kwa hiyo fedha zangu nikazitumia kumsomesha. Niliporudi nikaendelea na kazi na nikapata hela, lakini sikuwa nafahamu hayo mambo ya hati fungani, huenda ningekuwa vizuri kiuchumi lakini sikuyajua,” anasema.
Anasema kutokana na kutokuwa na elimu ya uwekezaji, alipopata mafao yake ya hifadhi ya jamii na fedha alizoingiziwa na shirika lake kutokana na utumishi wake uliotukuka, alizitumia bila mpangili mzuri.
“Kwa kawaida sina tabia ya kumnyima mtu kitu kama ninacho, sasa nilipopata zile hela za kustaafu za mwisho mtu akija mama nina shida hii nampa, mara mama nina harusi ya mdogo wangu nampa, kwa kifupi nilitumia zile fedha hadi zikaisha nimebani sina hela.
“Uzuri ni kwamba naishi na mtoto wangu ambaye ananihudumia na kuhakikisha ninapata mahitaji madogo madogo, ikiwemo hela za sadaka na gari yangu inakuwa na mafuta ya kunipeleka kanisani na kunirudisha, nimemwambia wala asihangaike kunipa fedha nyingi maana nitazitumia tu,” anasema.
Anasema haikuwa rahisi kwake kuanza maisha mapya baada ya kufanya kazi kwa miaka 41 na kujihusisha na mambo mengine mengi yaliyokuwa yakimfanya asitulie sehemu moja kwa muda mrefu, hali iliyompa wakati mgumu katika siku zake za awali za kustaafu.
“Katika siku za awali nilipata tabu, haikuwa rahisi kukubaliana na ukweli kwamba muda wangu wa kufanya kazi umekwisha hivyo natakiwa kupumzika. Nikawaza na kufikia uamuzi kwamba siwezi kulima wala kuwa mfugaji lakini naweza kuendelea kuitumia akili yangu kufanya kazi.
“Nikatengeneza ofisi nyumbani kwangu, nikawa naendelea kuamka asubuhi najiandaa naingia ofisini kwangu ambako nimekuwa nikifanya shughuli mbalimbali, ikiwemo uandishi wa kitabu ambacho kimebeba historia ya maisha yangu na kazi zangu,” anasema.
Mbali na uandishi wa kitabu na kazi nyingine zinazohusisha taaluma ya sheria, Dk Hellen anasema anautumia muda wa kustaafu kuwa karibu zaidi na familia yake, shughuli za kanisani na kusoma vitabu.