Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fanya haya kumsaidia mtoto anayepitia udhalilishaji

Kipindi cha nyuma mwanangu, wakati huo akisoma chekechea, alilalamika mara nyingi kuonewa na wenzake.

Malalamiko yake yalikuwa kunyang’anywa vitu vyake, kutukanwa na kuchokozwa na wenzake.

Mwanzoni niliona ni malalamiko ya kitoto. Sikuyapa uzito. Lakini siku niliposikia akiota usiku na kulalamika kwa sauti nikagundua kuna tatizo kubwa.

Nilichukua hatua haraka. Pengine na wewe mzazi unaye mtoto anayepitia wakati kama huo wa kuonewa na kudhalilishwa na wenzake.

Shule ni eneo linalokutanisha watoto wenye tabia mbalimbali. Ingawa mazingira yanaweza kutofautiana kulingana na aina na mahali shule ilipo, upo uwezekano wa mwanao kusoma na wenzake wenye tabia ya kufurahia kunyanyasa wenzao.

Mara nyingi hawa ni watoto wanaojisikia kupungukiwa kitu ndani yao. Matusi, kuonea wenzao, uchokozi na vitendo kama hivyo huwa ni jitihada za kuziba utupu wanaojisikia ndani yao.

Udhalilishaji katika makala haya ni vitendo kama mtoto kuzomewa, kutukanwa, kuibiwa, kunyang’anywa vifaa vyake, kuchokozwa na wakati mwingine kupigwa bila sababu ya msingi.

Waathirika wa unyanyasaji mara nyingi huwa ni watoto wenye umri mdogo kuliko wenzao. Katika mazingira ambayo mtoto mwenye umri mdogo anasoma na wenzake wanaomzidi umri inakuwa rahisi kujikuta ananyanyasika.

Lakini pia kuna wale watoto wapole wanaoamini hawana sababu ya kujitetea hata pale wanapoonewa. Wenzao wasumbufu hutumia hulka hiyo kama fursa ya kuwaonea.

Vile vile kuna suala la jinsia. Katika mazingira yetu, mtoto wa kike anakuwa kwenye hatari ya kunyanyaswa zaidi kuliko mtoto wa kiume. Baadhi ya watoto wa kiume huamini wao ndio wenye haki zaidi kuliko wenzao wa kike. Katika mukhtadha huu, inakuwa rahisi mtoto wa kike kujikuta anapata msukukosuko usio na sababu.

Ukiacha matukio ya udhalilishaji shuleni, siku hizi hata mitandao inaweza kutumika. Mitandao ya kijamii, kama zilivyo shule, inakutanisha watu wenye hulka tofauti.

Wapo watu waliokata tamaa na maisha wanaopenda kutoa maoni yanayolenga kumdhalilisha mtu mwingine. Mtoto anayetumia mitandao hii anaweza kujikuta anadhalilika kwa sababu tu ya picha au bandiko lake mtandaoni.


Athari za unyanyasaji

Mtoto anayeonewa na kudhalilishwa mara nyingi hupoteza kujiamini. Fikiria mtoto anyechekwa na wenzake kwa sababu tu ametoa jibu lisilo sahihi darasani.

Kwa mtoto mdogo kuchekwa kuna tafsiri mbaya. Kuchekwa kunamaanisha hawezi, hana thamani na kwa maana hiyo hafai. Hisia kama hizi za kujiona kama kuna kitu kimepunguka zikiendelea kwa muda mrefu, mtoto hufika mahali akaamini kuwa kweli hawezi.

Imani kuwa hawezi inaweza kuzaa tatizo la upweke. Wageni wanaweza kuja nyumbani na ungetazamia, kama kawaida, yake angewachangamkia. Lakini ghafla unashangaa mtoto anawaogopa na hataki kujichanganya na watu. Usichukulie hali hii kirahisi kwa sababu inaweza kumfanya awe na sonona.

Mtoto mwenye sonona hukosa furaha, huonekana mwenye uso wenye masikitiko na muda mwingi hulalamika. Kukata tamaa kunaweza kusababisha awe mgomvi akiwa na wenzake, ajibu kwa ukali jambo ambalo angeweza kuliongea kwa upole na anaweza pia akafika mahali akajidhuru au kudhuru wengine.

Dalili kuwa mambo hayako sawa kwa mtoto ni pale anapoanza kuogopa kwenda shule. Inapotokea mtoto anakosa msisimko wa kwenda shule kwa siku kadhaa mara nyingi inaweza kuwa anaogopa kukutana na wenzake wanaomdhalilisha.

Pia linaweza kujitokeza tatizo la kupoteza vitu bila maelezo yanayoeleweka. Jioni anarudi na madaftari yake lakini asubuhi hayajulikani yalipo. Upotevu unatokana na kukosa uzingativu na hivyo kusahau mambo kirahisi.


Msaada tunaoweza kumpa

Kudhalilishwa kunaweza kuharibu namna mtoto anavyojitazama. Upo uwezekano wa kuanza kuhisi hana mtu anayemwelewa. Msaada hapa ni kujenga mazingira ya kuaminika kwa kutomhukumu. Maneno kama ‘Kwa nini unawaacha wakusumbue?” huleta picha ya kutomwelewa mtoto na kuhukumiwa.

Pili, kuna hili la kumlazimisha mtoto kufunguka’ haraka. Unapolazimisha sana mtoto huanza kukuona ‘polisi’ na hatakuwa na uhuru wa kukueleza yote yanayoendelea maishani mwake. Mnaweza kuzungumza mambo yanayomhusu bila kumuuliza maswali mengi kuhusu matukio asiyopenda kuyasimuliaa.

Tatu, kumhakikishia mtoto kuwa yeye ni mtu wa thamani hata katika mazingira ya kunyanyasika kuna umuhimu wake. Sauti yako kama mzazi anayemwamini ni muhimu sana isikike kuondoa ile imani inayojengeka ndani yake inayomfanya ajione ana shida mahali.

Nne, ona uwezekano wa kumshirikisha mwalimu kwa msaada zaidi. Kwa kawaida, watoto huamini sana sauti za walimu wao. Mwalimu akionekana anachukua hatua itaongeza imani kwa mtoto.

Hata hivyo, fanya hivyo kwa tahadhari kuondoa hatari ya mwalimu kukutafsiri kama aina ya mzazi anayekuza mambo madogo na anayemdekeza mtoto.