Hamahama ya wazazi inavyoathiri malezi ya watoto
Muktasari:
- Ingawa fedha ni muhimu katika ustawi wa mtoto, lakini hazitoshi kumlea mtoto kisaikolojia na kijamii. Mtoto anahitaji uwepo wa mzazi, ushirikiano wa karibu na uangalizi wa kila siku unaojenga tabia, maadili na utambulisho wake wa kihisia
Dar es Salaam. Katika miaka ya hivi karibuni, ongezeko la uhamaji wa wazazi kutoka maeneo ya vijijini kwenda mijini, au kutoka nchi zao kwenda ughaibuni kutafuta ajira na maisha bora, imekuwa na mchango mkubwa kiuchumi katika familia nyingi, japokuwa madhara yake kimalezi, ni kubwa.
Hata hivyo, wataalamu wa malezi na uchumi, wanasema hali hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha hali ya uchumi wa familia nyingi.
Inaelezwa kwamba hali hiyo pia inaacha pengo kubwa katika mfumo wa malezi ya watoto wanaoachwa nyuma na wazazi wao.
Wanasema ingawa fedha ni muhimu katika ustawi wa mtoto, lakini hazitoshi kumlea mtoto kisaikolojia na kijamii. Mtoto anahitaji uwepo wa mzazi, ushirikiano wa karibu na uangalizi wa kila siku unaojenga tabia, maadili na utambulisho wake wa kihisia.
Yupo mtaalamu mmoja wa saikolojia ya watoto nilikutana naye kwenye mkutano uliokuwa unazungumzia makuzi na malezi ya mtoto wiki iliyopita, aliniambia kuwa watoto wanaoachwa na wazazi kwa muda mrefu, hupitia changamoto za kihisia zinazoweza kuathiri maisha yao ya baadaye.
Mtaalamu huyo alisema mtoto anapokosa uwepo wa mzazi kwa muda mrefu, huanza kujenga hisia za kuachwa, kukataliwa au kutothaminiwa.
Hali hii inaweza kusababisha huzuni ya muda mrefu kwake, wasiwasi na hata wakati mwingine hupoteza ile hai ya kufurahia maisha.
“Na hata baadhi ya watoto hujaribu kujaza pengo hilo kwa njia zisizo salama, kama kutafuta upendo kutoka kwa makundi ya rika yasiyo sahihi, jambo ambalo linaweza kuwaingiza katika tabia hatarishi kama uvutaji wa sigara, matumizi ya dawa za kulevya au kujiingiza kwenye uhusiano wa mapenzi mapema na mengine yasiyofaa,” aliniambia.
Ilinifikirisha. Nikawaza kuwa, huenda watoto hawa ndiyo miongoni mwa wanaoharibikiwa kitabia, kwa sababu wanaweza kuonesha mabadiliko yanayoonekana polepole lakini yenye athari kubwa.
Ndiyo tunajikuta tukiwashuhudia baadhi wakipoteza hamu ya masomo, wengine huanza kuwa na tabia ya ukaidi, kutoheshimu walezi waliopo au kujitenga na familia.
Hali hii mara nyingi husababishwa na ukosefu wa uhusiano wa karibu wa kihisia kati ya mtoto na mzazi.
Profesa Davoo Mvungi, mtaalamu wa sosholojia ya familia, aliwahi kusema kwamba uhamaji wa wazazi umebadilisha kwa kiasi kikubwa muundo wa malezi ya Kiafrika ambao ulitegemea ushirikiano wa familia pana.
“Zamani, mtoto alilelewa na jamii nzima. Lakini sasa, mzazi anapohama, jukumu linabaki kwa bibi, babu au ndugu ambao mara nyingi hawana muda, nguvu au mbinu za kisasa za malezi ya kihisia,” anaonya.
Anaongeza kuwa changamoto kubwa si tu kukosekana kwa mzazi kimwili, bali pia kupungua kwa mawasiliano ya mara kwa mara na mtoto.
Hali hii husababisha mtoto kuhisi kutengwa na familia yake, jambo linaloweza kuathiri uwezo wake wa kujiamini na kujenga uhusiano bora na watu wanao mzunguka.
Kutokana na hilo, wazazi wanapaswa kufahamu kwamba kuna umuhimu wa wazazi walioko mbali kutumia njia mbadala za mawasiliano ili kuendelea kushiriki kikamilifu katika maisha ya watoto wao.
Mzazi akiwa mbali, haimaanishi ametoweka katika maisha ya mtoto. Ni muhimu akawa anapiga simu mara kwa mara, kuzungumza kuhusu shule, marafiki na changamoto anazopitia mwanawe.
Hata hivyo, tukumbuke kuwa mawasiliano ya simu pekee hayawezi kuchukua nafasi ya uwepo wa kimwili wa mzazi.
Watoto wanahitaji pia mguso wa moja kwa moja wa malezi kama kushiriki chakula, mazungumzo ya ana kwa ana na mwongozo wa kila siku unaojenga tabia na maadili kutoka kwa baba na mama.
Wataalamu wengine wa afya ya akili wanasema watoto wanaokua katika mazingira ya kutokuwa na mzazi karibu, mara nyingi hupata changamoto za kujithamini, msongo wa mawazo na wakati mwingine hata matatizo ya kitabia yanayoathiri maisha yao ya baadaye.
Hata hivyo, si kila uhamaji wa wazazi una matokeo hasi. Ikiwa utaandaliwa vizuri, kwa kuwepo kwa mpango madhubuti wa malezi mbadala, mawasiliano ya mara kwa mara na ushirikiano wa familia, watoto wanaweza kuendelea kukua katika mazingira yenye afya ya kihisia na kijamii.
Kwa mfano, familia zinazoweka utaratibu wa mara kwa mara wa kuwasiliana, kufuatilia maendeleo ya shule na kushirikisha watoto katika uamuzi muhimu, imeonekana kupunguza athari za kihisia kwa watoto wao hata kama wazazi wako mbali.
Hivyo, uhamaji wa wazazi ni suala lenye pande mbili; linaweza kuboresha maisha ya kifedha ya familia, lakini pia linaweza kuathiri malezi ya watoto ikiwa halitasimamiwa vizuri.
Kwa maana nyingine, familia inapaswa kulichukulia suala hili kwa umakini zaidi kwa kuhakikisha mtoto hapotezi haki yake ya msingi ya kulelewa kwa upendo hata kama wazazi watakuwa mbali.