Lulu Mohammed Kessy : ‘Ujasiriamali unahitaji moyo wa kujituma na kujitoa’
Muktasari:
- Lakini wapo wanaopambana kujikwamua katikati ya dunia yenye kila aina ya vikwazo na mmoja wao ni Lulu Mohammed Kessy.
- Lulu anasema kila siku mpya ni fursa ya kufanya mambo mazuri na kuuthibitishia ulimwengu kuwa mwanamke anaweza hata bila kuwezesha.
Mapambano ya wanawake wenye malengo ya kuhakikisha ndoto zao zinatimia kwa kutumia fursa zilizopo yanakumbana na vikwazo vya kukatisha tamaa katikati ya mfumo unaoibua changamoto mpya kila siku.
Lakini wapo wanaopambana kujikwamua katikati ya dunia yenye kila aina ya vikwazo na mmoja wao ni Lulu Mohammed Kessy.
Lulu anasema kila siku mpya ni fursa ya kufanya mambo mazuri na kuuthibitishia ulimwengu kuwa mwanamke anaweza hata bila kuwezesha.
Chini ya Kampuni yake ya Ralmoss General Enterprise amejipambanua kuwa mwanamke anayechukua kila fursa inayokatiza mbele yake.
“Kila siku najaribu kuanzisha biashara mpya kutokana na mahitaji. Dunia haitaki watu wenye akili mgando kwa biashara hii ndiyo nitakayoifanya maisha yangu yote. Lazima ujifunze mbinu mpya na masoko kila siku,” anasema Lulu.
Kupitia kampuni hiyo anafanya biashara za viungo vya chakula, vitafunwa, unga wa lishe na kutoa huduma za vyakula katika sherehe au maofisini.
“Ninaongeza bidhaa mpya kila kukicha. Nilianza kama mama lishe lakini sasa nimekuwa, badala ya kukaa kibandani kusubiri wateja sasa nawapelekea maofisini na kwenye masherehe,” anasema.
Mwanamke huyo mama wa watoto watatu anasema changamoto katika biashara hazikosekani lakini hazimkatishi tamaa kuendelea.
“Ninajitahidi kupata mafunzo ya mara kwa mara katika kile ninachokifanya. Ninaweza kulipa fedha nyingi kuhudhuria semina kwa sababu najua umuhimu wa maarifa,” anafafanua.
Anasema siri ya mafanikio ipo katika kutafuta maarifa zaidi kwa kuwa yanamuwezesha kujua mahitaji ya soko.
Wanawake na siasa
Mwanamke huyo anasema wengi wanakumbwa na woga katika masuala mbalimbali na wapo wanaokimbilia majukwaa ya siasa badala ya kusimamia na kuendeleza mambo mazuri waliyoanzisha.
‘’Mimi naamini mwanamke ana uwezo wa kufanya jambo kubwa kumzidi hata mwanaume muhimu ni kupaza sauti yako na kujiamini kuwa unaweza. Ukiona umekwama kwenye plan A siyo kosa kwenda hata plan D,’’ anasema.
‘’Wanawake wengine wanatafuta’status’kupitia majukwaa ya kisiasa badala ya kupigania mafanikio kupitia masuala mengine ya maendeleo kwenye jamii, ukifanikiwa katika shughuli nyingine za kijamii ni rahisi kupenya kwenye siasa kuliko kutegemea huruma kwa sababu ya jinsia,’’anasema Lulu.
‘’Kuna wanawake wanaojulikana kwenye siasa na hawajulikani kwenye mambo mengine makubwa waliyofanya kwenye jamii,wengine wamekumbwa na uoga unaowapunguzia kujiamini kufanya mambo makubwa. Kama wangefanya vizuri kwenye jamii wangeheshimika zaidi kwenye siasa.’’anasema Paschazia.
Wito wake kwa Serikali
Anasema Serikali na wadau wanatakiwa kujenga mazingira rafiki yatakayowavutia wazawa walioko ndani na nje ya nchi kuwekeza badala ya kuwekewa vikwazo vinavyokatisha tamaa.
Kwa wajasiriamali kama yeye anasema ni vyema Serikali ikawaweka katika vipaumbele vyake ili kuwapa moyo wa kuwekeza zaidi.
“Mimi ndoto yangu ni kuanzisha kiwanda cha kusindika bidhaa zangu lakini sitafanikiwa kama Serikali haitaniwekea mazingira mazuri ya kuwekeza ikiwemo kupata mkopo mkubwa unatakoniwezesha kuanzisha kiwanda.”
“Serikali pia itutambue kwa kuwa tumewaajiri Watanzania wenzetu, kuna watu wanaendesha maisha kwa kunitegemea mimi. Kama nitafunga biashara watoto wao watakosa karo, chakula na mavazi,” anafafanua.