MAISHA NA MAHUSIANO: Aina tano za waume
Mara nyingi kwenye ndoa kumekuwa na malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wanawake walioolewa “wake”, na malalamiko haya yanaelekezwa kwenye namna waume zao wanavyoishi au wanavyofanya. Kutokana na hilo nimekuja na makala hii itakayokusaidia kuwfahamu wanaume, japo wanafanana kijinsia lakini kwenye tabia zao katika ndoa wanatofautiana.
Mume bachelor
Mume wa aina hii anapenda kufanya mambo kivyake pasipo kumshirikisha mke wake. Anapenda sana kuvinjari na kuwa na marafiki zake sana na si mke wake, anaweza akashinda baa akajisahau kama ana mke na watoto, akiwa na rafiki anajisikia furaha zaidi kuliko anapokuwa na mkewe au watoto wake.
Hata wakipanga kwenda mtoko na mkewe lazima atawaita na rafiki zake, wanaume wa hivi ni ngumu kuwapa ‘quality’ time wake zao. Mkikaa pamoja na yeye na marafiki zake basi mke fahamu umeshatengwa, wataanza kuongea ligi ya England, warudi ligi ya Tanzania halafu wakichoka mpira wahamie siasa.
Wanaume wa hivi ndoa huichukulia kirahisi tu. Ni watu wasiionyesha kupevuka kwenye mambo yanayohusiana na ndoa au familia “They are always pre-mature on things related to marriage and family”.
Mume tindikali
Yeye anachemka kama tindikali, ana fujo hatari, ngumi mkononi. Ukimjibu tu kidogo umeisha. Ukinyamaza anasema kwanini hutaki kujibu anachoongea, kwa hiyo anaweza kukuadhibu kwa kumdharau. Ni mbabe kwa kila jambo. Kiufupi ni mume hatari na wa kumwogopa wakati wowote ule maana hujui ataamka na kipi
Mume mtumwa
Hawa kila mara kiu yao ni kutaka wafanyiwe, waheshimiwe kama wafalme ila wao wanawafanya wake zao watumwa, huwahimiza kufanya mambo ya mila na tamaduni za zamani katika kuonyesha heshima kwao, hata kitu ambacho anaweza kufanya yeye atataka mke afanye.
Akiangusha kitu mke aokote, mara nyingine wanataka mke amsalimie shikamoo baba nanihii, Huwezi kusalimia mume wako haujapiga goti, au kuinama maana ni dhambi.
Mara nyingine hawapendi kuitwa kwa majina yao ya kwanza, wanapenda kuitwa majina ya ukoo au ya watoto wao.
Mume wa jumla
Mwanaume wa hivi ni wa kila mwanamke. Utaona anawajali wanawake wengine kuliko mkewe. Atawasifia walivyopendeza na walivyo wazuri wakati mke wake hajawahi kusikia sentensi kama hizo kwenye kinywa cha mumewe.
Hata kama hana mahusiano na hao wanawake lakini utaona anapenda kuwasaidia hususani kuwapa pesa wakati hata siku moja hawezi mpa pesa mkewe. Ukiwachunguza marafiki zao wengi ni wanawake kuliko wanaume.
Ni mkarimu sana kwa wanawake wengine lakini si kwa mkewe. Anaweza kuwa rafiki sana kwa marafiki za mke wake kuliko alivyo rafiki kwa mke wake.
Mume mkavu
Mume wa hivi ana mudi kila wakati, hujui saa ngapi ana furaha na sangapi kabadilika. Ni ngumu sana kuzielewa hisia zake. Unaweza kufikiri anafuraha maana alikuwa anacheka ghafla ukimgeukia unaona kishanuna.
Wabahili sana wanaume wahivi. Hawajali kabisa hisia za wake zao. Anaweza kusema neno kavu na chungu mkewe akaumia hata kutoa chozi lakini yeye bado tu anaendelea kubwabwaja maneno bila kujali kuwa amemuumiza mwenzake kihisia.
Wanaume wa hivi hawana muda wowote kwenye kuweka jitihada katika mahusiano yao ili penzi linoge. Wao wanadhani mahusiano mazuri yanakuja tu yenyewe, mkikosana, wewe ndio utahangaika sana kwenye kutafuta suluhu yeye yupo tu wala hana habari. Kiufupi ni kwamba waume wa aina hii hawana utu.