MC Pilipili Alikimbia chaki kuwa mvunja mbavu
Emmanuel Mathias maarufu kama Mc Pilipili
Muktasari:
Na hii ndio sababu iliyochangia kuzaliwa kwa jina la Mc Pilipili. Mashabiki wake wanasema kuwa maneno yake siyo tu hufurahisha, bali huwasha hivyo hawajutii kumpatia jina hilo.
Ukubwa wa jina lake haulingani na umri wake. Umaarufu wa kazi zake pia ni tofauti kabisa na umbo lake. Ni kijana mtanashati ambaye mara nyingi amekuwa akivutia na vazi lake la suti. Anapofanya kazi kama mshereheshaji huchoki kumsikiliza kutokana na ubunifu wake wa kupangilia maneno.
Na hii ndio sababu iliyochangia kuzaliwa kwa jina la Mc Pilipili. Mashabiki wake wanasema kuwa maneno yake siyo tu hufurahisha, bali huwasha hivyo hawajutii kumpatia jina hilo.
Akizungumza kuhusu jina lake , Mc Pilipili anasema kuwa, wakati akitoka kwao Dodoma miaka kadhaa iliyopita, kichwani kwake aliwaza kufupisha jina lake ili lionekane la kuvutia zaidi hasa awapo kazini.
“Nilijiita Emanu na nilijitambulisha hivyo, nilitaka nionekane wa mjini, lakini pia nilitaka nionekane mvulana mwenye jina fulani ‘amaizing’” anafafanua na kuongeza: “ Lakini wakati nikiwa kwenye kazi, nilipenda kujinasibu, nikisema kuwa mimi ndiye nitawapa raha na nitawawasha kama pilipili.”
Kwa kuwa mara nyingi alipenda kutumia maneno hayo, haikuchukua muda, akajikuta akitambulika kwa jina hilo. Hivyo kila alipokuwa akitoka kwenye kazi hata wale waliotaka mawasiliano yake, walikuwa wakimuita kwa jina la Mc Pilipili.
“Leo hii jina langu limefutika kabisa.” anafafanua Mc PiliPili ambaye ni baba wa mtoto mmoja.
Aliibuka kutoka wapi?
Tofauti na wasanii wengine, Mc Pilipili kitaaluma ni mwalimu. Aliingia jijini Dar es Salaam mara baada ya kuacha kazi yake ya ualimu na moja kwa moja kujikita kwenye fani hiyo aliyoianza tangu akiwa na umri wa miaka saba.
“Nimefanya kazi ya ualimu kwa miaka saba nikifundisha masomo ya Kiswahili, Biblia, historia na masomo mengine ya sanaa.” anafafanua na kuongeza.
“Mapenzi yangu ya sanaa ya uchekeshaji, yalinichochea kuachana na ualimu na kujikita kwenye fani hiyo.”
Hadi sasa tayari amepanda majukwaa zaidi ya 100 ya kitaifa na kimataifa, akifanya kazi na wakongwe wa fani hiyo Afrika ya Mashariki kama vile Anne Kansiime na Eric Omondi.
Mc Pilipili anasema licha ya kuwa na kipaji cha uchekeshaji, safari yake ilianzia mbali kidogo kwani alianza kama mcheza shoo za muziki.
“Safari yangu ya kuwa mshereheshaji ilianzia mwaka 1992 nikiwa mdogo. Nilikuwa nikipenda kucheza muziki jambo lililonifanya kuwa mcheza shoo maarufu mjini Dodoma na kanda ya kati kwa ujumla wake. Kutokana na makeke yangu niwapo jukwaani mashabiki wangu walipendelea kuniita Mjukuu wa Pepe Kale”.
“Nakumbuka katika harakati zangu za kucheza muziki, nilikutana na mwanamuziki Lovii Longomba (Marehemu), ambaye nilimvutia na kushawishika kunichukua kwa ajili ya kwenda kucheza kwenye bendi yake lakini hilo halikufanikiwa baada ya mama kukataa. Ilikuwa katika onyesho moja ndani ya uwanja wa Jamhuri, Dodoma”.
Nani alimvutia kuingia kwenye ushereheshaji na uchekeshaji?
Mwaka 2002 akiwa kidato cha pili, tayari alikuwa mchekeshaji na mshereheshaji mwenye jina kubwa mkoani Dodoma.
“Nilikuwa nikifahamika kama Ema wa DomSec au Mc Manu. Kupitia umaarufu huo nilipata fursa ya kuitwa kwenye sherehe mbalimbali.” anafafanua.
Wakati akiwa Dodoma alikuwa akivutiwa sana na Mc George Urio, na hasa ndiye aliyeibua kiu yake ya kuwa mshereheshaji mkubwa, lakini baada ya kufika Dar es Salaam alikutana na Mc Antony Luvanda ambaye pia alikuwa na ndoto ya kuwa mchungaji wakati akiwa mtoto.
Kwa upande wa uchekeshaji anasema, wako wasanii wengi lakini baadhi yao wanaomtia hamasa ni pamoja na Joti, Mpoki na Masanja.
Wachekeshaji wan je wanaomvutia ni pamoja na Eric Omond kutoka Kenya na Basket Mouth wa Nigeria.
Nini mtazamo wake kuhusu uchekeshaji nchini?
Mc Pilipili ni miongoni mwa wachekeshaji wa kisasa anayetambua mchango wa wachekeshaji wa zamani.
Pamoja na kuamini kuwa sanaa hiyo isingefika hapa kama siyo mchango wa wale waliotangulia, anasema bado kuna mambo ya kuyafanyia kazi ili kuipeleka mbele zaidi sanaa hiyo.
“Komedi yetu inatoka kwa kina Majuto, Bi Nyakomba, Onyango na wengine na ile ya kuigiza na inapokelewa na vijana kama sisi kwa sanaa mpya iitwayo Ucheshi wa Wima ambao mtu unasimama ukiwa mtanashati na unasimama kuchekesha halaiki,” anafafanua na kuongeza.
“Tasnia ya uchekeshaji nchini inaingia katika zama nyingine, tukubali au tukatae inabidi tutoke katika komedi za kujipaka na kuvaa magauni na vitambi.”
Historia yake
Alizaliwa mkoani Dodoma Oktoba 1, 1985 na kupewa jina la Emmanuel Mathias. Ni mtoto wa pili kati ya watoto wa tano wa familia ya Mzee Matebe.
Alipata elimu yake ya msingi katika shule za Kiwanja cha Ndege na baadaye Ipangala na kuhitimu mwaka 1999.
Mwaka 2001 alijiunga na Shule ya Sekondari Dodoma kabla ya kujiunga na shule ya Jubilee kwa ajili ya kidato cha tano na cha sita.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Ekernforde 2007-2009 alipohitimu stashahada ya juu ya ualimu.
Baadhi ya shule alizowahi kufundisha ni pamoja na Shule ya Msingi Changa, Sekondari ya Kilole za Tanga na , Shule ya Msingi DCT Andrea Mwaka na Sekondari DCT Jubelee zote za Dodoma.