Mercy aiangukia tasnia ya urembo

Mercy Kindamba, (22) mshindi wa nafasi ya nne katika mashindano ya Miss Ocean World, yaliyofanyika nchini India

Dar es Salaam. Mratibu wa Miss Utalii nchini, Erasto Chipungahelo amesema tasnia ya urembo ni taaluma kama taaluma kama taaluma zingine hivyo washiriki hawana budi kutambua hilo.


Alisema hilo si eneo la kutafutia umaarufu na pesa kama baadhi yao  wanavyodhani, bali ni sehemu ya ajira.

"Hili ni daraja la mafanikio, mshindi wa mashindano ya urembo ndani na nje ya nchi anaweza kuanzisha Taasisi au shirika la kuisaidia jamii, haya si mashindano ya kushiriki tu na kuishia hapo," alisema Chipungahelo jana alipotembelea makao makuu ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata jijini Dar es Salaam.

Kauli yake imekuja siku kadhaa, baada ya mrembo Mercy Kindamba, (22) kuiwakilisha nchi na kumaliza wa nne kwenye mashindano ya dunia ya Miss Ocean, yaliyofanyika nchini India.

Chipungahelo ambaye ni Muasisi wa taasisi ya Africa Tourism Promotion Centre inayoratibu mashindano ya Miss utalii nchini na ndiyo ilimsimamia Mercy kwenye fainali hizo alisema ni wakati wa washiriki wa kitaifa kutambua jamii inawatazama.

Alisema katika jamii kuna matatizo mengi hivyo warembo wanaoshinda wanapaswa kuanzisha jukwaa la usaidizi akitolea mfano ukeketaji na kuelekeza kuwa mshindi anaweza kuanzisha taasisi ya kupinga ukatili huo jambo ambalo ni faida kwa jamii na si kuangalia zaidi zawadi atakazozipata huko.  

Aidha ameiomba Serikali kutunga sera za kuwatumia watu wanaoipeperusha vyema bendera ya nchi.

“Lazima kuwe na sera za kuwatambua watu wanaoipeperusha bendera yetu kimataifa ‘International icons’ tuweze kuwatumia. Sio tu katika urembo bali hata kwenye mpira, muziki tunaishia tu kuwapa pongezi lakini lazima tuwatumie kama nchi,” alisema Chipungahelo.

Akielezea mafanikio aliyoyapata Mercy nchini India alisema kupitia mrembo huyo kama nchi imepata faida kuitangaza Tanzania kwa kiasi kikubwa hasa katika utalii kama Serikali ya awamu ya sita inavyopambana katika sekta hiyo.

“Mbali ya kushinda nafasi ya nne pia Mercy ameshinda tuzo ya vazi bora la taifa la kiasili alilokuwa amevaa katika mashindano hayo yaliyokutanisha nchi 43 duniani.”

Alisema kupitia vazi hilo la ngozi alilovaa limetangaza utamaduni wa Tanzania kimataifa pia mrembo huyo ametangaza utalii wa fukwe zinazopatikana nchini ambapo watalii wataongezeka.