Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Msingi wa afya ya mtoto huanzia nyumbani

Picha na Mtandao.

Muktasari:

  • Mtoto anayelelewa katika mazingira yanayothamini lishe bora na mtindo wa maisha wenye afya, ana nafasi kubwa ya kukua akiwa mwenye nguvu, uwezo wa kujifunza, kujiamini na kuwa mtu mzima mwenye maisha yenye tija.

Wazazi wengi hufikiri jukumu lao katika afya ya mtoto linaishia kumpeleka hospitalini anapougua au kuhakikisha anapata chakula kila siku.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba afya ya mtoto hujengwa hatua kwa hatua kupitia uamuzi unaofanywa ndani ya familia. Namna mtoto anavyolishwa, anavyoishi na tabia anazojifunza akiwa nyumbani, vina mchango mkubwa katika kuamua afya yake ya sasa na hata ya baadaye.

Katika miaka ya mwanzo ya maisha, mtoto hujifunza zaidi kwa kuangalia na kuiga kuliko kwa kusikiliza maelekezo. Hivyo, wazazi wanakuwa walimu wa kwanza wa lishe na mtindo wa maisha.

Wataalamu wa lishe mara nyingi husisitiza, mtoto anayekulia katika familia inayothamini ulaji wa vyakula vyenye virutubisho, kunywa maji ya kutosha na kufanya mazoezi ya mwili hujenga tabia hizo mapema na huwa na nafasi kubwa ya kuziendeleza anapokuwa mtu mzima.

Hivyo, lishe bora si suala la kushiba pekee. Bali mzazi anapaswa kuhakikisha mtoto anapata virutubisho vinavyohitajika kwa ukuaji wa mwili, maendeleo ya ubongo na kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa.

Schola Nela, mtaalamu wa lishe bora kwa watoto anasema, mlo unaojumuisha nafaka, vyakula vya protini, mboga za majani, matunda na mafuta yenye afya humwezesha mtoto kukua vizuri na kuwa na uwezo mzuri wa kujifunza. “Lakini kinyume chake, ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi, mafuta mengi na chumvi kupita kiasi unaweza kuchangia matatizo ya afya yanayoanza mapema na kuendelea hata utu mtoto akifikia utu uzima,” anasema Nela.

Jambo la kutafakari katika hili ni kwamba, watoto hawachagui wanachokula kwa hiari yao. Mara nyingi hula kile wanachoandaliwa au kununuliwa na wazazi. Hii ina maana kuwa uchaguzi wa chakula unaofanywa na mzazi ndiyo unaojenga msingi wa tabia za ulaji wa mtoto.

Iwapo familia itajenga utaratibu wa kula pamoja na kuandaa milo yenye uwiano wa virutubisho, mtoto atajifunza kuwa lishe bora ni sehemu ya maisha ya kawaida.

Mbali na lishe, mtindo wa maisha una nafasi kubwa katika kujenga afya ya mtoto. Katika dunia ya sasa, watoto wengi hutumia muda mwingi mbele ya televisheni, simu za mkononi au michezo ya kielektroniki.

Ingawa teknolojia ina faida zake, matumizi yasiyodhibitiwa yanaweza kupunguza muda wa kufanya shughuli za mwili. Matokeo yake ni kuongezeka kwa hatari ya unene uliopitiliza, usingizi usio wa kutosha na hata changamoto za afya ya akili.

Ili kudhibiti haya, wazazi wana nafasi ya kubadili hali hiyo kwa kuweka utaratibu unaowahamasisha watoto kushiriki michezo au kufanya shughuli nyingine zinazochochea harakati za mwili. Si lazima shughuli hizo ziwe za gharama kubwa. Hata michezo ya kawaida ya nje, matembezi ya kifamilia au kazi nyepesi za nyumbani zinazolingana na umri wa mtoto, zinaweza kuwa sehemu ya kujenga afya bora.

Inaelezwa kwamba, mtoto anayelala kwa muda unaofaa huwa na uwezo mzuri wa kujifunza, kukua na kudhibiti hisia zake. Ratiba nzuri ya kulala na kuamka huusaidia mwili kufanya kazi ipasavyo na kupunguza uchovu unaoweza kuathiri maendeleo yake.

Hivyo jukumu la wazazi halipaswi kuishia katika kutoa maelekezo tu, bali kuwaaminisha kile wanachokiona mzazi anakitekeleza.

Mzazi anayesisitiza umuhimu wa kula matunda lakini yeye mwenyewe hafuati utaratibu huo, atakuwa na ugumu wa kumshawishi mtoto. Vivyo hivyo, mzazi anayehimiza mazoezi huku akitumia muda mwingi bila kufanya shughuli za mwili, hupunguza nguvu ya ujumbe wake. Mfano wa vitendo ndiyo njia yenye ushawishi mkubwa katika malezi.

Pia ni muhimu kutambua kuwa afya ya mtoto haihusiani na mwili pekee. Mazingira ya familia yenye upendo, mazungumzo ya kujenga na muda wa kuwa pamoja huchangia afya ya akili na ustawi wa mtoto.

Wanaopata uangalizi wa karibu kutoka kwa wazazi wao, mara nyingi hujenga kujiamini, nidhamu na uwezo mzuri wa kufanya uamuzi unayolinda afya zao.

Wapo wazazi wanaodhani kuwa lishe bora ni kwa familia zenye kipato kikubwa. Dhana hii si sahihi. Tanzania ina vyakula vingi vya asili vyenye virutubisho vinavyopatikana kwa gharama nafuu, ikiwemo mboga za majani, kunde, nafaka mbalimbali, viazi, ndizi, mihogo, matunda ya msimu, mayai na samaki wanaopatikana katika maeneo mengi nchini. Kilicho muhimu ni kupanga matumizi ya rasilimali zilizopo na kuzingatia uwiano wa makundi ya vyakula katika mlo wa kila siku.

Malezi bora ya afya yanahitaji pia ushirikiano kati ya familia, shule na watu wanaomzunguka mtoto. Anapopata ujumbe unaofanana kuhusu lishe, usafi, mazoezi na mtindo bora wa maisha kutoka katika mazingira yote anayoishi, huwa rahisi kujenga tabia zinazodumu.

Hivyo, wazazi wanapaswa kutambua kuwa zawadi kubwa wanayoweza kumpa mtoto si mali pekee, bali afya njema. Afya hiyo haijengwi kwa siku moja, bali kupitia uamuzi mdogo unaofanywa kila siku mezani, nyumbani na katika maisha ya familia kwa ujumla.

Mtoto anayelelewa katika mazingira yanayothamini lishe bora na mtindo wa maisha wenye afya, ana nafasi kubwa ya kukua akiwa mwenye nguvu, uwezo wa kujifunza, kujiamini na kuwa mtu mzima mwenye maisha yenye tija. Kwa msingi huo, malezi ya afya si chaguo, bali ni wajibu unaopaswa kupewa kipaumbele katika kila familia.