Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mzazi ndiye ngao ya mtoto dhidi ya shinikizo la rika

Picha na Mtandao.

Muktasari:

  • Wataalamu wa malezi wanasema  shinikizo la rika halitaisha,  kwa sababu ni sehemu ya safari ya ukuaji wa mtoto.

Malezi ya mtoto katika dunia ya leo yamekuwa na changamoto nyingi kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma. Mbali na ushawishi kutoka kwenye familia na jamii, watoto na vijana wanakutana na shinikizo kubwa kutoka kwa wenzao shuleni, mitaani na kupitia mitandao ya kijamii.

Mara nyingi, shinikizo hilo huwafanya wafanye uamuzi ambao si matokeo ya utashi wao, bali ni jitihada za kutaka kukubalika na marafiki.

Wataalamu wa maendeleo ya mtoto wanaeleza kuwa hali hiyo, inayojulikana kama shinikizo la rika (peer pressure), ni sehemu ya kawaida ya ukuaji, hasa wakati wa balehe, vijana huanza kujenga utambulisho wao.

Hata hivyo, kiwango ambacho mtoto atakubali au kukataa ushawishi huo, hutegemea msingi wa malezi alioupata nyumbani.

Wapo watoto wanaoweza kusimama imara wanaposhinikizwa kufanya jambo lisilo sahihi, lakini wapo wanaokubali kwa hofu ya kuonekana tofauti, kuchekwa au kutengwa na wenzao.

Ndipo wazazi wanapopaswa kutafakari kama wamewajengea watoto wao uwezo wa kufanya uamuzi sahihi hata wanapokuwa mbali na macho yao.

Kwa mujibu wa American Psychological Association, watoto wanaojengewa kujiamini, uwezo wa kutatua matatizo na kufanya uamuzi kwa kuzingatia maadili waliyojifunza nyumbani, huwa na uwezekano mkubwa wa kupinga ushawishi hasi wa wenzao.

Hii inaonyesha kuwa malezi bora si kutoa mahitaji ya msingi pekee, bali ni kumlea mtoto mwenye misingi ya maadili na uwezo wa kujisimamia.

Jambo la kwanza ambalo mzazi anatakiwa kulipa kipaumbele ni kujenga mawasiliano ya karibu na mtoto. Katika familia nyingi, mazungumzo kati ya mzazi na mtoto hujikita kwenye masomo, kazi za nyumbani au nidhamu pekee.

Hata hivyo, mtoto anahitaji pia nafasi ya kueleza anachokiona, anachokisikia na changamoto anazokutana nazo akiwa na marafiki zake.

Mtoto anayezoea kusikilizwa nyumbani huwa rahisi kueleza anaposhinikizwa kuonja dawa za kulevya, kukwepa masomo, kushiriki vitendo vya ukatili au kujiingiza katika tabia nyingine hatarishi.

Kinyume chake, mtoto anayehofia kukemewa kila mara anaweza kuficha matatizo yake hadi yatakapokuwa makubwa.

Kwa mujibu wa United Nations Children's Fund, mawasiliano ya wazi na yenye kuaminiana kati ya mzazi na mtoto huongeza uwezo wa mtoto kufanya uamuzi salama na kutafuta msaada anapokabiliwa na changamoto. Hilo linawataka wazazi kuwa wasikilizaji wazuri kabla ya kuwa waamuzi.

Sambamba na hilo, watoto wanahitaji kufundishwa stadi za maisha. Miongoni mwa stadi hizo ni uwezo wa kusema "hapana" kwa heshima bila kuogopa kupoteza urafiki.

Wazazi wanaweza kufanya mazoezi ya mazungumzo ya kufikirika nyumbani kwa kumuuliza mtoto angefanya nini ikiwa rafiki yake angemshawishi kuvunja sheria za shule au kutumia kilevi. Mazoezi hayo humjengea mtoto ujasiri wa kufanya uamuzi sahihi anapokutana na mazingira halisi.

Aidha, wazazi hawapaswi kupuuza kuwafahamu marafiki wa watoto wao. Kumjua rafiki wa mtoto si kuvamia faragha yake, bali ni sehemu ya wajibu wa malezi.

Ni muhimu pia kuwafahamu wazazi au walezi wa marafiki hao ili kujenga ushirikiano katika kulea watoto wenye maadili yanayofanana.

Katika zama hizi za kidijitali, ushawishi wa rika hauishii darasani au uwanjani. Simu janja na mitandao ya kijamii imepanua wigo wa ushawishi huo.

Mtoto anaweza kushinikizwa kushiriki changamoto hatarishi mtandaoni, kuiga maisha ya watu mashuhuri au kutafuta umaarufu kwa kufanya vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama na mustakabali wake.

Hivyo, wazazi wanapaswa kufuatilia matumizi ya teknolojia kwa hekima, huku wakiwafundisha watoto namna ya kutambua maudhui yenye manufaa na yale yenye madhara.

Hata hivyo, silaha kubwa zaidi katika kupambana na shinikizo la rika ni mfano wa mzazi mwenyewe. Haiwezekani mzazi awafundishe watoto uaminifu huku yeye akionyesha vitendo vya udanganyifu mbele yao.

Vivyo hivyo, mtoto hawezi kuelewa umuhimu wa nidhamu ikiwa mzazi wake mwenyewe haoneshi kuwajibika katika maisha ya kila siku. Watoto hujifunza zaidi kutokana na matendo wanayoyaona kuliko maneno wanayoyasikia.

Ni muhimu pia kuwapongeza watoto wanapofanya uamuzi sahihi, hata kama uamuzi huo utawafanya waonekane tofauti na wenzao. Pongezi hizo hujenga kujiamini na kuwafanya waamini kwamba thamani yao haitokani na kukubalika na kila mtu, bali na kusimamia kile kilicho sahihi.

Ndiyo maana wataalamu wa malezi wanasema  shinikizo la rika halitaisha kwa sababu ni sehemu ya safari ya ukuaji wa mtoto.