ONGEA NA AUNT BETTIE: Hii mimba sio ya mume wangu

Anti nimeolewa huu mwaka wa sita, mume wangu anapenda pombe na mtu wa kunipuuzia sana, hasa linapokuja suala la kukata kiu yangu ya faragha. Nimekuwa nikitumia nguvu sana kupata huduma hiyo ninapoihitaji. Anti bila kuongeza uongo kuna wakati ninapata huduma hiyo kwa mwezi mara moja, ilhali mume wangu ana miaka isiyozidi 35, mimi nina 32 damu inachemka.

Katika hali hiyo kuna kijana alikuwa ananitaka muda mrefu, nimejikuta naingia kwenye uhusiano ili nikate kiu yangu. Ila kilichotokea ndiyo kimenifanya nikuandikie unipe ushauri. Nimepata mimba, ila ninahisi siyo ya mume wangu kulingana na siku nilizokutana naye yeye na mume wangu.

Naomba unishauri nifanyeje, maana naona hili suala linanitafuna na mimba inakua sasa inakwenda miezi minane.


Makubwa haya! Pamoja na utetezi ulioanza nao kuwa ulikuwa hukatwi kiu yako na mumeo bado hukuwa na sababu ya kutoka nje ya ndoa. Kweli inawezekana kama binadamu ulikuwa unazidiwa, ulichopaswa kufanya ni kutafuta suluhisho ndani ya ndoa yako kwa kutafuta ushauri kama huu, ikiwezekana hata kuhusisha viongozi wa dini na wasimamizi wenu wa ndoa kuliko ulivyofanya.

Kuhusu hiyo mimba huna namna, wahenga walisema kila muomba chumvi huombea chungu chake, nawe umeombea chako huna budi kukabiliana na ulichokifanya.

Hivyo tafuta namna bora ya kufanya ili umueleze suala hili mumeo, hakutakuwa na maana kulificha. Ila si rahisi kufanya hivyo lakini utalazimika kufanya.

Sina namna nzuri ya kukueleza jinsi ya kufikisha suala lako kwa mumeo, lakini usiruhusu kuzaa mtoto wa familia nyingine na kumpa mumeo tafadhali.

Pia, sitaki kushiriki katika hili, nani ataelewa changamoto zako za kutopewa unyumba umegeuka kuwa mkosaji kwa kujifanya hakimu wa kuamua mambo kwa njia za mkato. Mweleze mumeo hakuna namna na ujiandae kisaikolojia, sijui kama kutakuwa na ndoa tena hapo. Sijapenda kabisa tabia yako.

Nakutana na warembo wengi, lakini nakosa mke

Nashangaa sijui inakuwaje, natafuta mchumba lakini sipati licha ya kukutana na warembo wengi. Natamani nijipe muda, lakini naona ninazidi kuzeeka.

Nifanyeje?


Mmh! Kweli unakosa mchumba? Siamini. Inawezekana kinachokukwamisha ni vigezo unavyovitaka au mahali unakowatafuta. Ungeniambia huwa unakwenda kuwatafuta au wanapatikana wapi mara nyingi ningejua jinsi ya kukushauri.

Ninachojua watu huoana kwa kujuana, kupendana au kupata taarifa za wanayetaka kumuoa kupitia ndugu, jamaa na marafiki. Sasa ajabu wewe unawatafuta mwenyewe na unakosa, ina maana hujawahi kupenda au kupendwa?

Kuna kitu unazidisha, nadhani unatafuta mke wa aina fulani ambaye pengine hapatikani maeneo unayoishi na kutembelea au hajawahi kuwepo kwenye dunia.

Naomba siku nyingine niandikie unatafuta vipi, wapi mchumba. Unataka vigezo gani ili nijue naanzia wapi, kwa swali lilivyo nashindwa kuwa na majibu ya moja kwa moja.

Nakushauri punguza matarajio makubwa unapotafuta mke kwa kuwa hakuna binadamu aliye mkamilifu.

Unachopaswa ni kuangalia vitu muhimu kama anavyo, ikiwamo ustaarabu na uelewa, maana huwezi kuishi na mtu anayekosa vitu hivyo miongoni mwa vingi anavyopaswa kuwa navyo.

Najua huwezi kukaa bila kuwa na uhusiano na kwa kuwa hujaoa na kimjini mjini utakuwa naye zaidi ya mmoja (samahani kama haupo hivyo), chagua miongoni mwao huwezi kukosa wa kuoa.