Pekosi inaboa au inabamba?

Pekosi ni aina ya suruali yenye muonekano unaoshika mwili kuanzia usawa wa kiuno hadi kwenye magoti, lakini kushuka chini huachia, tofauti na suruali nyingine zinazoshika mwili kuanzia juu hadi chini.

Katika historia ya mitindo pekosi zilivaliwa sana kipindi cha miaka ya zamani hadi sasa na jinsi ya kike katika mitindo mbalimbali, lakini likichukuliwa kama vazi la kawaida.

Ndipo ilipoingia fasheni ya ‘skini jeans’, muundo wake hushika mwili kuanzia sehemu ya kiunoni hadi miguuni, mpaka leo nguo hizo zinavaliwa sana na jinsi ya kike na kubakia kuwa fasheni inayobamba.

Baada ya kuingia fasheni ya ‘skin jeans’ watu walioendelea kuvaa pekosi walionekana kama wamepitwa na fasheni, hivyo kuufanya mtindo huo kutokuwa na thamani si kwa watoto wala wakubwa.

Kama waswahili wanavyosema cha kale dhahabu, msemo huo unajidhihirisha katika fasheni ya pekosi, siku za hivi karibuni mtindo huo umerudi kwa kasi ukiwa wenye hadhi ya kifasheni, pia kushika soko la biashara ya nguo.

Thamani ya mtindo huo imekua kutokana na vazi hilo kuvaliwa sana na wasanii wa jinsia zote, hivyo kutoa mwitikio chanya kwa watu wengine wanaoendana na ‘trend’ ya fasheni kupata mwonekano wa kipekee.

Kwa sasa vazi hilo lipo katika namna mbili, ile ya awali ikiwa na ubunifu wa rangi nzuri zinazovutia na ya pili mtindo wa kunakshiwa kwa mifuko mingi kuanzia juu mpaka sehemu za miguuni, ikijulikana kama ‘Cargo jeans.’
Jina hilo lililotokana na fasheni hiyo kuwa na mifuko unayoweza kuwekea vitu vingi kwa wakati mmoja bila kuathiri mwonekano wako.
 

Wanamitindo wanalizungumziaje?

Akizungumza na Mwananchi, mbunifu wa mavazi, Tydo Master anasema pekosi imekuwa inabamba kutokana na namna ilivyochukua sura mpya bila kubagua jinsi tofauti na awali.

Anasema zamani lilikuwa likivaliwa na wanawake tu, lakini mtindo huo umebamba kuanzia mwaka 2023 hadi sasa upo katika chati.

“Hili vazi lilikuwepo na kuna watu waliendelea kuvaa, lakini mwaka 2023 lilibamba na kuingia katika chati ya mitindo, hasa lilipovaliwa sana na watu maarufu nchini na wasanii. Zamani pekos ilikuwa ikivaliwa na wanawake tu, lakini sasa hivi kuna cargo jeans mtindo wa pekosi inavaliwa na jinsi zote,” anasema Tydo.

Mbunifu mwingine, Frivola mwenye brand ya Vola Entire anaeleza namna unavyoweza kuvaa pekosi na kupata mwonekano wa kipekee.

Pekosi huvaliwa na tisheti kubwa au saizi yako chini ukaivalia na raba kwa upande wa wanaume, wanawake unaweza kuvaa pekosi na crop top, vest, damini koti au tisheti kwa chini ukavaa sendo, croksi na raba. Utapata mwonekano mzuri wa kuvutia.
 

Wavaaji wamelipokeaje?

Akizungumza na Mwananchi, Aisha Mbuma anasema amelipokea vazi la pekosi kwa mikono miwili kwa sababu anapenda kupendeza na kuendana na ‘trend’ ya fasheni. Anasema pekosi humpa mwonekano unaovutia, hasa akivaa na topu rangi isiyoendana na suruali hiyo.

“Raha ya kupendeza uendane na ‘trend’ ya fasheni, cha muhimu ikupendeze maana sio kila nguo inampendeza mtu. Pekosi hunipa mwonekano wa kipekee ulionifanya niwe nazo za rangi tofauti kama nne, nikiwa navaa huwa naivalia na topu za rangi tofauti na rangi ya suruali niliyoivaa,” anasema Aisha.