Uvaaji vipini, hereni kwa wanaume ni fasheni?

Wakati inaonekana ni ajabu kwa jamii zetu za Kitanzania wanaume kuvaa vipini puani na hereni, lakini katika ulimwengu wa mitindo na utandawazi imekuwa jambo la kawaida.

Awali, baadhi ya jamii zilikuwa zinapinga urembo huo uliozoeleka kwa wanawake kuvaliwa na wanaume, lakini sasa jinsia zote zinavaa urembo huo.

Baadhi ya jamii katika nchi za Ulaya na Asia urembo wa kuvaa hereni na vipini kwa wanaume huchukuliwa jambo la kawaida.

Kwa hapa nchini baadhi ya wanaume hutumia urembo huu wa hereni na vipini na kuonekana kuupenda.

Urembo wa vipini umeanza muda kidogo na ulivaliwa sana na wanawake wa pwani, ingawa siku hizi sio wa pwani tu wanaotumia urembo huu, bali hata wengine.

Hata hivyo, siku hizi mtindo umekuja kivingine zaidi kwa kuwa kipini huvaliwa katikati ya pua na huitwa ‘kisharufu’ na wengine huvaa sehemu mbili za pua.

Tukumbuke ni asilimia ndogo sana ya watu wanaokubaliana na muonekano huu Afrika, hasa hapa nchini na huleta ugumu zaidi kwa upande wa jinsia ya kiume.

Akizungumza na Mwananchi, Sharifu Hamadi, ambaye ni mfanyabiashara wa Kariakoo anasema kazi yake kubwa ni kuuza vipini vya puani, hereni na urembo mwingine.

Anasema siku hizi soko la bidhaa zake limebadilika sana kutokana na wateja wake kuwa wa kiume ingawa na wanawake pia hununua.

“Mambo siku hizi yamebadilika, wanaume wengi wamekuwa wakipenda urembo kama wanawake, tena hasa vipini vya puani, mara ya kwanza aliwahi kuja mteja wa kiume kuulizia hereni na vipini, mimi nilijua huo urembo ni kwa ajili ya mwanamke, kumbe ulikuwa wa kwake, baada ya kumuona akivaa mbele yangu,” anasema Hamadi .

“Tangu siku hiyo, sikushangaa tena, nikajua ni mambo ya fasheni na utandawazi tunaoiga kutoka kwa wasanii wakubwa na watu maarufu duniani wanaoendana na wakati na dunia inavyotaka,” anasema Sharifu.
Mfanyabiashara huyo anatoa maoni yake kuhusiana na urembo huo akisema,

“unajua kwa maadili ya kwetu kidogo kumekuwa na ukakasi kuhusu wanaume kuingilia urembo wa wanawake, lakini sisi watu wa fasheni tunaona kawaida pia.”

Mwanamvita, maarufu Mama Abuu, mkazi wa Dar es Salaam, anasema wanaume wanaovaa vipini na hereni ni kama hawana maadili.
Anasema hakuna fasheni kwa wanaume kuvaa vipini na hereni na haifai mwanamume kuvaa huo urembo.

“Utandawazi umekuwa ukiwapeleka vijana kwenye dunia nyingine kabisa, hasa katika masuala ya fasheni kumekuwa kuna mambo ya tofauti kila siku, sasa mwanamume unavaaje kipini cha pua au hereni, haifai kabisa.

“Zamani wazee wetu walikuwa wakiwakataza watoto au vijana kuvaa urembo wa vipini puani na kutoboa pua au masikio, tofauti na sasa mambo yamekuwa tofauti,” anasema Mwanamvita.

Hata hivyo, anasema baadhi ya watu wanawaiga wasanii wanaovaa hereni na vipini wakiona na kitu sahihi, jambo ambalo sio sawa.

“Vijana siku hizi wamekuwa wakiiga fasheni kutoka kwa wasanii au watu maarufu, kitu ambacho hawafikirii kama kitakuwa na madhara au faida ili mradi waende na fasheni.”

Faithal Azizi, mkazi wa Kariakoo anasema huwa hapendi kuona mwanamume kavaa hereni wala kipini puani.

Anasema mwanamume anapaswa kuvaa cheni, saa na pete mkononi, lakini suala la kipini na hereni wawaachie wanawake.

“Ukweli ni kwamba, binafsi sipendi kuvaa kipini, ingawa sichukii kumuona mwanamke mwenzangu kavaa, na huwa namsifia lakini mimi kuvaa hapana…sasa ndio avae mwanamume, hiyo haipendezi kwa kweli,” anasema Faithal.

Hata hivyo, anasema fasheni za wanawake kuingiliwa na wanaume imetokana na utandawazi, hasa kwa vijana kuiga tamaduni za watu wa nje.