Fahamu historia ya urembo vikuku

Vikuku vinaweza kuwa vya shanga, ngozi au hata madini kama dhahabu, fedha na shaba zenye muundo kama wa bangili ambazo huvaliwa miguuni na jinsi ya kike.

Kikuu kinaweza kuvaliwa mguu mmoja au miguu yote na kumekuwapo na tafsiri tofauti baina ya makundi ya watu katika jamii kuhusiana na urembo huu, wapo wanaouchukulia urembo huu kwa upande hasi na chanya.

Katika ulimwengu wa mitindo, vikuku ni miongoni wa fasheni inayopendelewa na wanawake, licha ya kuwapo na mitazamo hiyo.
Uvaaji wa vikuku ni urembo, pia ni utamaduni wa Mwafrika. Awali urembo huu ulionekana zaidi katika baadhi ya makabila ya Kiafrika ukivaliwa na watu wa rika zote; kuanzia watoto wadogo, wasichana, wanawake wa makamo, hata wazee.

Kwa baadhi ya makabila, vikuku vimekuwa vikivaliwa kama mila kwamba kila mwanamke anapozaliwa lazima avae urembo huo kwa kufuata desturi na tamaduni zao, tofauti na ilivyo sasa ambapo wengi huvaa kama urembo wa kawaida.
Wanajamii wengi wamekuwa na mtazamo tofauti kuhusu uvaaji wa vikuku, wakihusisha na mambo yasiyofaa na kuonyesha kuwa wengi wanaovaa wamepotoka au kwenda kinyume na maadili ya Kitanzania.

 

Historia yake

Zamani vikuku vilivaliwa na jinsia zote, yaani wanaume na wanawake, hasa katika jamii ya Wamasai ambao mpaka sasa ni sehemu yao ya urembo.

Akizungumza na Mwananchi, Mwamvi Mwapili, mzaliwa wa Tabora anaeleza neno vikuku lilitokana na aina ya kuku ambao sehemu ya chini ya miguu yao walikuwa na manyoya yaliyokuwa yamenyanyuka na kutengeneza muundo kama wa bangili, hivyo kutokana na kushahabiana na kuufanya urembo huo kuitwa vikuku.

Awali urembo huo ulivaliwa na mabinti vigoli hata wanawake kama sehemu ya pambo la mwanamke. Mtazamo ulibadilika baada ya kuanzishwa kwa madanguro ya wanawake wanaofanya biashara ya kuuza miili yao, hivyo njia waliyoitumia kujibainisha walivaa vikuku miguuni kuwapa ishara wateja wa huduma hiyo. Hapo ndipo mtazamo hasi wa vikuku ulipoanzia.

Vikuku vimekuwepo tangu nyakati za kale. Iliaminika, kutokana na utafiti kwamba wanawake wazee katika Afrika na Misri walivaa ili kuonyesha uzuri, hadhi, haiba na uhalisi nchini, hasa nchini India.

 

Mtazamo wa vikuku katika jamii

Ester Azizi, muuzaji wa urembo akizungumza na Mwananchi anasema vikuku ni urembo wa kawaida na unawafanya wanawake wengi wapendeze, tafsiri ya kuchukuliwa kama uhuni inatokana na baadhi ya watu walioamua kuvipa maana yao.
Kwa upande wake, Swaumu Abdallah anasema hawezi kuvaa vikuku kwa sababu anaona kuwa ni uhuni, hasa ukivaa katika miguu yote miwili.

Gadner Mbonela, anasema akimuona mwanamke amevaa vikuku huweka hisia kuwa anafanya biashara ya kuuza mwili wake kwa sababu wakati wa makuzi yake na jamii inayomzunguka hakuona wasichana wakivaa vikuku kutokana na kujua kuwa wanawake wanaovaa hivyo ni wahuni.

Lakini baada ya kufika mjini, alishangaa kuona kuwa wanawake kuvaa vikuku ni kawaida tu. Hata hivyo, anasema hatamani kuona mke wake akiwa amevaa vikuku.
Muyonga Jumanne anaeleza anavutiwa na urembo huo kwa mwanamke kwa sababu humpa mvuto wa kipekee.

 

Upande wa wanamitindo

Tydo Master, mbunifu wa mavazi ya kike na kiume anaeleza kuwa katika tasnia ya urembo na mitindo, vikuku ni urembo wa kawaida na unatengeneza maudhui ya pambo la mwanamke na kuhifadhi mila na tamaduni.

Anasema kuna wakati huonyesha mavazi ya jamii ya Kimasai au Kinyamwezi, hivyo hawezi kuacha kuwavalisha ushanga wa miguuni kwa sababu ni urembo uliovaliwa na wanawake.

Ngokolii, Mmasai na muuzaji wa ushanga anasema katika jamii yao mtoto akizaliwa huchukua siku chache ili ngozi itengemae, baada ya hapo anavalishwa vikuku haijalishi atakuwa wa jinsia gani.

“Ni urembo ambao kwetu ni mila na tamaduni ambao hauwezi kufa,” anasema.