Prime
Usikae mbali na fasheni msimu wa mahafali
Sehemu nyingi rangi za majoho wanayovaa wahitimu huwa ni nyeusi, hivyo ili wapate mwonekano mzuri wa mavazi watakayovaa ndani ya majoho ni muhimu kuzingatia rangi zitakazoweza kufanya mitindo ya nguo kuonekana vizuri na kuvutia.
Mbunifu wa mavazi, Tydo Master anasema kwa upande wa wanawake nguo zinazotakiwa kuvaliwa ndani ya joho zisiwe zenye ukubwa sana kwa sababu zitaleta muonekano mbaya nje. Anasema wazingatie nguo zinazoshika mwili kwa kiasi fulani.
"Kuna wahitimu wanataka kuvaa magauni ambayo yameachia mwili na kuwekewa wavu kwa ndani, kiukweli huwa hawapendezi kwa sababu joho linakuwa limetuna bila kuwa na mwonekano mzuri,” anasema Master. Kwa upande wa wanaume, anasema hawana shida kutokana na aina ya nguo zao.
Zipo rangi nyingi za kuvutia, lakini zingatia rangi zitakazowaka na kuonekana vizuri, hii inawahusu wote kwa jinsi ya kike na kiume.
Jinsi ya kiume hupendelea kuvaa suti, lakini wahakikishe ndani ya suti zao kuna rangi katika mashati zinazowaka.
Ili kupata muonekano huo wa kipekee, hasa kwa wahitimu wa vyuo vikuu wanapaswa kuzingatia mambo mbalimbali, ikiwamo uvaaji wa nguo 'classic' zinazoendana na tukio lenyewe, uvaaji wa viatu rasmi vitakavyokufanya kuwa huru na upakaji wa ‘make up’ ya wastani kwa wahitimu wa kike.
Akizungumza na Mwananchi, mtaalamu wa masuala ya urembo, Ester Azizi anasema mahafali ni moja kati ya siku muhimu sana kwa mwanafunzi katika maisha yake ya kielimu, hivyo ni muhimu aonekane katika mvuto wa kipekee.
“Kwa sababu wahitimu wengi hudai siku hiyo haijirudii maishani,” anasema Ester.
Pia, anasema mahafali ni sherehe lakini ipo katika mfumo rasmi, hivyo ni vyema kuvaa nguo rasmi lakini zilizo katika mtindo unaovutia.
"Zile nguo zetu za kung’aa za kwenye harusi na sendoff, kwenye sherehe za mahafali siyo mahala pake," anasema Ester.
Pia, anashauri wahitimu wa kike kujiepusha na uvaaji wa nguo fupi na zenye kubana sana kwa kuwa zinaweza kuwafanya kushindwa kuwa huru kusherehekea.
"Ili kupata mavazi yatakayokupa muonekano mzuri, ni vyema kufanya maandalizi mapema ni wapi utapata nguo nzuri au mbunifu wa mavazi atakayeweza kukushonea nguo itakayokupa muonekano mzuri katika siku hiyo muhimu," anasema Ester.
Kwa upande wa viatu, anasema uvaaji wa viatu huendana na tukio linalofanyika katika eneo husika.
"Piga picha mwanamume kavaa suti nzuri halafu chini akavaa sendo au ndala, hii itaharibu mvuto wake kutokana na kutokuwa na muunganiko kati ya nguo na aina ya viatu alivyovaa, ukizingatia aina ya tukio lenyewe," anasema Ester.
Anawataka wahitimu wa kike kuacha tabia ya kuiga kuvaa viatu virefu sana, ambavyo hawana uwezo wa kutembea navyo.
Kuhusu ‘make up’ na nywele kwa wahitimu wa kike, mtaalamu mwingine wa masuala ya urembo, Elizabeth Nziku anasema ni vyema wahitimu hao kujiepusha na usukaji wa nywele au rasta zenye rangi rangi kwa kuwa zinaweza kuleta tafsiri tofauti kwa kuwa tukio hilo ni rasmi.
“Na waepuke kubond au kusuka nywele zitakazowapa tabu wakati wa kuvaa kofia ya joho. Pia, kwa upande wa wanaume wazingatie kunyoa kwa vinyozi ambao wamewazoea ili kuepusha kunyolewa vibaya.
"Tukio hilo ni rasmi, hivyo usukaji wa nywele za rangirangi au unyoaji wa mitindo isiyokuwa rasmi inaweza kuleta tafsiri isiyo nzuri kwa wageni waalikwa,” anasema Ester.
Kwa upande wa ‘make up’, Eliza anasema sio lazima japo inafanya muonekano wake kuvutia zaidi na ni vyema kupaka inayodumu kwa muda mrefu.
Eliza anashauri kabla ya tukio hilo ni vyema kufanya majaribio ya ‘make up’ ili kujua kama siku hiyo itakupendeza au.
“Make up haina ulazima japo humfanya mtu awe na mwonekano wa kuvutia, kuna wanawake wakipaka rangi ya mdomo na wanja tu wanakuwa na mwonekano mzuri. Hivyo, wakitaka kupaka ‘make up’ wazingatie aina ya makeup kulingana na sura ya mtu.”
Hata hivyo, wahitimu wanapaswa kuzingatia gharama nafuu zitakazokuwa ndani ya uwezo wao, lakini zitawafanya wapate muonekano wa kuvutia katika siku yao muhimu.
Hii ikiwa ni kupunguza baadhi ya vitu ambavyo havina umuhimu, hasa katika suala zima la fasheni.