Tokelezea na nguo zenye rangi ya chui ‘Leopard Print’
Leopard Print au mavazi yenye rangi ya chui ni aina ya nguo ambayo imezidi kubamba katika suala zima la mitindo, ambapo huvaliwa na rika zote.
Leopard Print imekuwa ikivaliwa sana hasa na jinsia ya kike kama mavazi mengine lakini wabunifu wa nguo wanadai nguo za rangi ya chui zina maana yake na hunasibishwa na tabia zinazowahusu watu wanaovaa nguo hizo.
Nguo za rangi ya chui ‘Leopard Print’ ni aina gani ya nguo?
Ni aina ya nguo ambazo michoro yake inashabihiana na rangi ya ngozi ya mnyama chui. Michoro hio huwa katika vitambaa vya aina mbalimbali kama kitambaa cha sufi, mng’ao ‘Satin’ na ngozi ‘Lether’ katika mitindo mbalimbali.
Asili ya nguo za rangi ya chui
Jarida la mitindo la Mindless mag nchini Marekani limeeleza asili ya nguo za rangi ya chui;
Kuvaa nguo za rangi ya chui awali ilikuwa ishara ya utajiri na nguvu kutokana na gharama yake, huvaliwa na kutumiwa na wafalme na malkia, mara nyingi iliaminika kuwapa hisia ya ulinzi. Chui mara nyingi wamekuwa ishara ya ujasiri, ukali na umbo la kike.
Leopard print lilikuwa vazi maarufu na muhimu katika miaka ya 1930. Ambapo ilionekana katika, sinema ya Tarzan ilithibitika kuwa ilikuwa chanzo kikuu cha msukumo wa kuchapishwa kwa nguo hizo, na kuleta hisia ya kuvutia kwake miongoni mwa wanawake.
Pia mbunifu Jo Weldon ameeleza katika mtandao nguo za rangi ya chui zilivaliwa sana na wanamziki wa kike.
Mmoja wa wavaaji wa kwanza wa chapa hiyo katika miaka ya 1950, mwimbaji Eartha Kitt ambaye aliamini kuwa alama ya chui inaashiria nguvu. Pia ilijenga picha ya kimaadili ya miaka ya 50, Kitt alikuwa anafananishwa miguu katika mitindo ya chui, na alionekana kuwa mkaidi na mwenye kujiamini, na hatimaye alifanya vazi la rangi ya chui kupata umaarufu mkubwa. Hivyo kuongezeka kwa uchapishaji wa rangi ya chui.
"Kitt alikuwa sehemu yangu ya kuanzia kutengeneza nguo za rangi ya chui kwani nilivutiwa naye sana kama mbunifu alionekana mzuri sana katika picha zake -- umbo thabiti. Lakini pia alikuwa mwanamke wa hali ya juu." Anasema
Jo Weldon
Nguo za rangi ya chui zina maudhui gani?
Mbunifu wa mavazi ya kike Julie kutoka London anasema Nguo za rangi ya chui ni nguo nzuri zinazovaliwa kwa wanawake wenye tabia ya kujiamini sana ambao wanajua nini wanakitaka katika maisha yao, wapambanaji na wanauwezo wa kufanya vitu visivyotegemewa machoni kwa watu. Maudhui haya yanatokana na tabia halisi ya mnyama chui ambaye anajiamini pale anapotafuta mawindo yake, ni mkali na ana mvuto wa asili.
Leopard print ina historia ndefu na katika miongo kadhaa imekuwa na mitindo mingi ya gharama ya juu na ya chini, lakini imekuwa ikirejea katika ubora wake bila kupoteza mvuto wake.
Kitu kinachofanya nguo za rangi ya chui kuwa ya kipekee ni ukweli kwamba inaweza kuvaliwa na kila mtu, kutoka kwa watu wa kawaida hadi nyota wa muziki duniani, na kufanya utengenezaji kuwa wa kisasa, japokuwa imeonekana kuwa haina mvuto kwa wengine kwa wakati mmoja.
Ingawa uzalishaji ulikua kwa kiwango kikubwa, katika karne ya ishirini na moja uchapishaji unakaribia kuchanganyika kutokana na umaarufu wake mkubwa wa kila mara, na kuifanya kuwa sehemu ya mtindo wa kila siku.
Pia wanawake wenye ushawishi kama mke wa rais wa zamani wa Marekani, Michelle Obama alivaa vazi la rangi ya chui Septemba 7, 2010 wakati wa hafla ya Mkurugenzi wa Sanaa wa Tamthilia ya Dansi ya Marekani Alvin Ailey Judith katika ukumbi wa Ikulu ya Marekani Mjini Washngton. Pia mwanamziki kutoka Marekani Beyonce alivaa vazi la rangi ya chui 2020 katika alibamu yake ya ‘Black is King’ ambapo anaeleza ilichukua masaa 1000 kutengeneza hio nguo yake.
Hii kwa mara nyingine tena ilileta maoni kwamba alama ya chui ni ishara ya mwanamke mwenye nguvu na huru, kama ambayo chui huonekana.
Je wanaume huvaa nguo za rangi ya chui?
Akizungumza na Mwananchi, mbunifu wa mavazi ya kiume, Samweli Chirumba anasema nguo za rangi ya chui huvaliwa mara chache kwa jinsia ya kiume hasa wanapokuwa wanafanya maonesho ya mavazi, lakini sio katika mizunguko ya kawaida.
“Inajulikana kuwa nguo za rangi ya chui mara nyingi huchukuliwa kama chapa ya kike, mara chache huvaliwa na wanaume, hata hao wanaume wanaokuwa wamevaa wengi wao huwa katika maonesho ya mavazi tu.” Amesema Chirumba.
Bado hadi leo, hata hivyo, alama ya chui inachukuliwa kuwa ya bei nafuu na ya kupendeza na wengine kutokana na historia yake ya awali.
Namna unavyoweza kutokelezea na nguo za rangi ya chui?
Akizungumza na Mwananchi mbunifu wa mavazi ya wanawake, Upendo Benedict alisema nguo za rangi ya chui ili zionekane na mvuto kuna namna, mda wa kuvaa na kuzingatia eneo husika.
“Nguo hizi unaweza kuvalia na nguo zenye rangi nyeusi, nyeupe, kahawia na peach”.
Kwa mtoko wa usiku unaweza kuvaa nguo ya rangi ya chui yenye kitambaa cha satini au veliveti kwa sababu inamng’ao unaopendeza zaidi wakati wa usiku.
Katika mizunguko ya kawaida au ofisini unaweza kuvaa rangi ya chui ikiwa na kitambaa cha pamba ‘Cotton’ ili kuzuia joto.
Katika kipindi cha baridi unaweza kuvaa rangi ya chui ikiwa katika mtindo wa ngozi ‘Leither’ kwa sababu inasaidia kukinga baridi.