Visa, mikasa ya mahusiano siku ya Valentine
Wanasaikolojia waeleza
Mwanasaikolojia na mtaalamu wa mahusiano, Naima Omari anasema kinachosababisha mahusiano kuvunjika siku ya Valentine ni tamaa na ahadi kutotimizwa miongoni mwa wapenzi.
“Hii imekaa katika sehemu mbili, moja ni wanawake ambao mara nyingi wanayavunja mahusiano siku ya Valentine kwa sababu tu hajapewa zawadi au kufanyiwa kitu cha kipekee na mpenzi wake.
“Lakini pia wakati mwingine wale marafiki zake wa karibu wanaweza kuwa chanzo endapo wao wakipewa zawadi au kufanyiwa vitu vya kipekee na wapenzi wao katika siku hiyo,” anasema Naima, ambaye pia ni mshauri wa mahusiano.
Katika sehemu ya pili, Naima anasema wanaume wengi wanavunja mahusiano yao wakati wa Valentine kutokana na tamaa katika mahusiano.
“Wanaume wanavunja mahusiano yao kwa haraka endapo akipata mpenzi mpya ambaye anaona wanaendana, na wakati huu unawakuta wanawake wengi wanakuwa tayari kuingia katika mahusiano kutokana na asili ya mwezi na tarehe husika (siku ya wapendanao),” anaongeza Naima.
Mwanasaikolojia huyo anashauri ili kuepuka kuvunja mahusiano siku ya Valentine, ni vyema wapenzi waishi kwa upendo kila siku na si kusubiria Valentine.
“Hii siku ukisubiri upendo wa kipekee utaumia sana endapo usipoupata, kitu cha muhimu jifunze kujipenda na kuridhika,” anashauri Naima.
Ushauri wa Naima unaendana na wa mwanasaikolojia mwingine na mtaalamu wa mahusiano, Japhet Ngali ambaye anasema matarajio yaliyopita kiasi katika siku ya Valentine ni chanzo cha migogoro na mahusiano mengi kuvunjika.
“Hii siku ukiwa na matarajio ya juu sana, kwamba labda mpenzi wangu ataninunulia kitu fulani, na asipofanya hivyo utaumia maradufu na mnaweza kuachana kwa sababu utaanza kupunguza mapenzi naye,” anashauri Ngali.
Hata hivyo, Ngali anashauri ili kudumu katika mahusiano na mpenzi wako hakikisha kila siku unaishi kama ni Valentine, hii akimaanisha kuwa na upendo wa dhati na uaminifu kwa mwenza wako.
Mafundisho ya dini
Licha ya sikukuu hiyo kuwa na dhana ya kuwakutanisha wapenzi ambao aghalabu hawajafunga ndoa, kwa mwaka 2024, Februari 14 pia ni siku ya Jumatano ya majivu ambayo Wakristo, hasa Wakatoliki huanza msimu wa kufunga wa Kwaresma.
Askofu Msaidizi mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini anasema siku hiyo si ya kutenda dhambi, bali ni ya kujitakasa kwa kufanya tafakari na kutenda matendo mema.
“Hiyo ni siku ya kufunga kwa Mkristo Mkatoliki yeyote, si siku ya kutenda dhambi, na hiyo ni amri na ni siku ya kuanza mafungo,” anasema Askofu Kilaini.
“Sasa kama ukitoka kupaka majivu ndio ukatende dhambi hiyo haipo sawa, kwa sababu siku yenyewe ni ya kujitakatifuza na ukifanya dhambi yoyote umeiharibu siku hiyo,” anaongeza Askofu Kilaini.
Uhusiano wa Valentine na biashara
Licha ya kuwapo mikasa katika mahusiano katika siku ya Valentine, ukweli unasalia wakati huu maduka yanayouza zawadi na bidhaa nyingine sampuli hiyo huneemeka zaidi.
Neema Mkunda, ambaye ni muuzaji wa duka la maua jijini Dar es Salaam, anasema msimu huu biashara inakuwa kubwa kwa sababu ya uhitaji wa bidhaa hizo katika kunogesha mapenzi.
“Huwezi kudanganya kwa sasa biashara tunaifanya sana, hapa kwangu nauza maua mbalimbali, nafunga zaidi na msimu huu kuanzia Februari 1 hadi Februari 14 tunawauzia watu wengi,” anasema.
Kuhusu jinsi ya wateja wake, Neema ambaye duka lake lipo Kijitonyama jijini Dar es Salaam anasema wanaonunua zawadi au kuagiza kupelekewa (delivery) wengi ni wanaume.
Kauli ya Neema kuhusu mauzo kuongezeka inaungwa mkono na utafiti wa miamala ya kadi za mastercard uliofanywa na kuchapishwa katika tovuti ya kampuni hiyo, unaosema matumizi ya kadi hizo katika manunuzi huongezeka mara tano zaidi siku ya Valentine.
Utafiti huo wa Mastercard ulifanyika katika nchi 53 duniani. “Miamala ya jumla msimu wa Valentine (11-14 Februari) imeongezeka kwa asilimia 31 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2018, 2019 na 2020).”
Historia ya Valentine
Kwa mujibu wa tovuti ya masuala ya historia ya ‘country living.com’, Italia wakati wa karne ya tano kulikuwa na kiongozi aliyeitwa Mfalme Claudius II, ambaye aliamini kuwa askari anapooa hawi mkakamavu na pia muda mwingi anawaza kuhusu familia yake zaidi ya kitu kingine chochote.
Hivyo alipiga marufuku ndoa kwa askari. Kitendo hicho hakikuwafurahisha watu wengi, akiwamo Padri Valentino. Kiongozi huyu wa kidini aliendelea kufungisha ndoa kwa siri.
Mfalme Claudius alipopata habari hizi aliamuru Valentino akamatwe na kuuawa.
Mtakatifu Valentino aliuawa Februari 14, ndiyo maana ikatangazwa rasmi kuadhimishwa kwa ajili ya kumkumbuka kama baba wa upendo na mtetezi wa wanandoa.
Historia zinaonyesha kuwa aliyetangaza rasmi kuadhimisha siku hiyo ni Papa Gelasius. Aidha, iko simulizi nyingine inayosema kuwa akiwa gerezani kwa amri ya Mfalme Claudius, Padri Valentino aliandika barua ambayo ilikuwa na salamu kwa binti aliyekuja kumsalimia gerezani, mwisho wa barua alihitimisha kwa kusema ‘Kutoka kwa Valentino wako’. Tangu hapo Valentino anakumbukwa kama mtetezi wa wapendanao na sikukuu yake kuadhimishwa ulimwenguni kote.
Kwa mujibu wa mafundisho ya Kanisa Katoliki, baadaye, Padri Valentino alikuja kutangazwa kuwa mtakatifu.