Zifuatazo ni tabia za mzungumzaji bora

Muktasari:

Lugha ya mwili huusisha vitu kama vile; muonekano wa sura, mikunjo ya uso, macho yalivyowekwa, kinywa kilivyo tumiwa, pua inavyofanywa wakati wa kuongea, mikono na pozi ya mwili ilivyo wakati wa kuzungumza.

Lugha ya mwili ni vile tunavyoweza kutumia miili yetu kuonyesha nia zetu. Mwili ni kiungo muhimu cha mawasiliano. Tafiti zinasema hata wakati mtu anazungumza kupitia mdomo, asilimia 60 ya ujumbe wake kupitia au kueleweka sio kwa kwa sababu ya maneno ya kinywani mwake bali ni kwa lugha ya mwili. Jambo hili ndilo hutiliwa mkazo na ule usemi usemao “matendo huzungumza zaidi kuliko maneno”

Lugha ya mwili huusisha vitu kama vile; muonekano wa sura, mikunjo ya uso, macho yalivyowekwa, kinywa kilivyo tumiwa, pua inavyofanywa wakati wa kuongea, mikono na pozi ya mwili ilivyo wakati wa kuzungumza.

Ni vema kujikumbusha kila wakati kuhusu umuhimu wa lugha ya mwili ili itusaidie kujijua sisi wenyewe na ule ujumbe tunaoutuma.

Hapa nataka kujaribu kueleza baadhi ya maeneo ya lugha ya mwili ambayo yatakusaidia kuweza kubadilika au kujirekebisha katika mchakato mzima wa mawasiliano kupitia mwili wako.

Unapozungumza mbele za watu tumia sentensi zinazokuelekea wewe zaidi ya sentensi zinazo waelekea wengine. Jilenge wewe zaidi ya kuwalenga wenzako unapozungumza. unapotumia sentensi za “ninyi” au “wewe” mara nyingi unaweza kuonekana usiye na ujasiri, tofauti na pale unapotumia sentensi zenye “mimi”. Unaweza kuonekana pia kama usiye yaamini maneno yako.

Sentensi zenye ujasiri na zenye kukulenga wewe binafsi ni kama vile

“nimefurahi kukuona”

“Ningependa kuzungumza na wewe”

“Sijafurahishwa na maneno yako”

Katika mazungumzo yako tumia zaidi sentensi na siyo maswali. Hii itakuwezesha pia kuonyesha kuwa una ujasiri katika kile unachokisema na unajiamini.

Mfano wa mazungumzo yakutumia swali: “Hivi ninyi mnamwonaje yule rafiki yetu?”

Badala yake ungetakiwa kusema “mimi sifurahishwi na matendo ya huyu rafiki yetu”

Au mara nyingine baba wa nyumba anapouliza “Hivi mnadhani nani baba humu ndani?” hii huonyesha kutojiamini kwake

“Hivi unafikiri mimi mjinga?”

“Hivi jamani sisi hatupewi huduma?”

Namna nyingine bora zaidi ya kuuliza swali

Je, unaweza kunisaidia tafadhali? Au je, utakubali kuoana na mimi?

Namna bora ya kuzungumza katika sentensi

Nitafurahi sana ikiwa utakubali kuoana namimi au nitafurahi sana kupata msaada kutoka kwako

Tumia zaidi sentensi zenye “kukiri” na sio sentensi zenye lawama. Sentensi zenye ukiri au kukiri ni zile ambazo anayezungumza anasema kile ambacho angetaka aone kikifanyika au kile ambacho angependa akione kikitendeka.

Kinyume chake ni sentensi zenye lawama; hizi ni zile ambazo mzungumzaji ana sema kile asichotaka, au kile asichokipenda kitokee au kifanyike.

Sentensi zenye lawama

“Sipendi kabisa vile unavyonichukulia au sipendi kabisa unavyoniingilia katika maongezi”

Sentesi zenye kukiri

“Ningefurahi kama ungesubiri nimalize kwanza kuongea halafu na wewe utaongea.”

Sentensi zenye lawama huonyesha ukosefu wa ujasiri kwa mzungumzaji, mbaya zaidi, sentensi hizi hazisaidii chochote katika kubadili tabia ya yule anayeambiwa maana hazionyeshi bayana ni nini kinachotakiwa kufanyika.

Sentensi zenye lawama pia huonyesha wazi tabia yako sugu ya kulaumu, pia huonyesha vitu usivyovipenda tu na kuvisahau vile vizuri unavyovipenda. Ni ngumu sana kumsaidia mtu ambaye analaumu usiku na mchana kuwa hapendi hiki, hapendi kile, hataki hiki na wala hataki kile na bado hawezi kusema anapenda au kutaka nini badala yake. Kwa hali hii watu hawa wanabaki kuwa walaumu mara dufu.

Kutembea kwa kudunda au kunesa

Kutembea huku kuwasilisha hisia za ujasiri. Tabia hii huweza kuwa ya asili au ya kujizoeza hususani apale unapodhani kuwa unachofanya ni cha muhimu zaidi na unapoamini kuwa wewe ni bora zaidi. Kutembea kwako kunaweza kuonyesha kila kinachoendelea akilini mwako.

Kupanda, kushuka, uzito au wepesi wa sauti

Pale unapojua hauna ugomvi au uadui na yeyote basi sauti yako itakuwa nzuri, na yakiasi cha kusikika na yeyote. Vituo vyako na misemo yako itakuwa ya kawaida na yenye uwiano. Pale unapohisi hofu, au kuwepo kwa wabaya wako, mara nyingi sauti yako huwa chini na isiyo na ujasiri.

Unashauriwa kwa hali yoyote ujitahidi kuzungumza kwa sauti ya kati, isiyo chini sana wala juu sana.

Mavazi sahihi

Unapohisi una nafasi fulani katika jamii au sehemu fulani utajikuta unajali sana suala la kuvaa kwako. Mavazi huweza kuzungumza nia ya moyo na huweza kuonyesha picha mbaya au nzuri kwa wanao kutazama. Mavazi ya aina fulani huweza kukupa tafsiri mbaya kwa watu tofauti na vile ulivyo kihalisia, au kwa upande mwingine mavazi mengine yamefanya wengine kuonekana kama vile ni wa maana sana na wakutegemewa wakati uhalisi haukuwa hivyo