Kuna tofauti kati ya uwezo na kipaji cha mtu

Muktasari:

Mwanamuziki bingwa wa kupiga gitaa, huenda alijifunza mpaka vidole vyake kutoa damu na bingwa wa mahesabu huenda alikaribia kuwehuka kwa mapenzi yake kwa namba.

Unaweza kuwa mzuri katika kitu fulani bila hata kuwa na kipawa. Kukipenda kitu na kukifanyia bidii kunaweza kukufanya uonekane ulizaliwa kufanya hivyo.

Mara nyingi tunapomuona mtu anafanya maajabu katika jambo fulani huwa tunashangazwa na kuona kama miujiza au ni kipaji tu, lakini ukweli inawezekana nyuma yake kuna miaka mingi ameitumia kujibidiisha. Wanariadha wanaojishindia medali katika mashindano ya olimpiki, hutumia muda mwingi katika mazoezi kuanzia alfajiri wakati watu wengine wakiwa wamejifunika mablanketi  na kukoroma katika usingizi mororo.

Mwanamuziki bingwa wa kupiga gitaa, huenda alijifunza mpaka vidole vyake kutoa damu na bingwa wa mahesabu huenda alikaribia kuwehuka kwa mapenzi yake kwa namba.

Wapo wasanii wengi wameingia kwenye sanaa kwa sababu tofauti ya kuwa na kipaji lakini wanaendelea kupiga shoo. Nani alijua Shilole, Lulu Diva na Snura wanaweza kutajwa katika kundi la wanamuziki nchini, lakini mdogomdogo wanajipatia riziki yao. Huenda muda ukawafanya wawe bora zaidi.

Sasa hivi ameibuka Harmorapa. Kiutani utani huenda akatoboa na kuanza kupiga hela. Yeye amechagua kupitia mlango wa nyuma kuingia katika Bongo Fleva.

Watu wengi wanamfahamu kuliko nyimbo zake lakini kwake ni nafuu kwa kuwa anakabiliwa na kazi ndogo tu ya kukaza katika muziki.

Wapo wasanii wengi nchini pamoja na kuwa na kazi nzuri wanasubiri katika foleni ya kutoka kwa miaka mingi, lakini Harmorapa ndani ya muda mfupi tu ameipata.

Mwenyewe kwa kinywa chake anakiri kuwa muziki umekuwa zali tu. Alikuwa anauza mitumba lakini mwonekano wake ukampa dili. Kila mtu alimwita Harmonize akimfananisha na yule wa WCB.

Kijana akaona anaweza kuutumia mwonekano huo kutoboa ndio maana hata alipochagua jina hakutaka kwenda mbali, akacheza humo humo.

Kilichobaki sasa hizi mbwembwe awaachie aliowakuta yeye afanye kazi. Umaarufu wake umekuja kwa lifti huenda ukarudi chini kwa lifti. Utarudi kwa ngazi iwapo tu atayafanyia kazi mapungufu yake.

Ni kijana mdogo ambaye mengi anayofanya unaona kabisa anaongozwa na walio nyuma yake. Inaonekana kuna fedha nyingi zimewekwa kumfikisha hapo, sasa kama mwekezaji anataka kuzirudisha lazima awekeze katika kazi yake.

Watu wanapenda kufuatilia matukio ya watu, muda sio mrefu mvuto wa hadithi za Harmorapa utakwisha watu watataka kusikia ama kazi zake au hadithi za mtu mwingine mpya.