KUTOKA BASATA: Mwenye wazo tofauti la kuanzisha tuzo alete

Muktasari:

Malengo haya ndiyo sasa kwa pamoja yanakuja kwenye lengo kuu la tuzo ambalo ni kukuza na kuendeleza sekta husika. Yaani kadri wasanii wanavyoshindana kubuni kazi zenye ubora zinazoingia kushindana kwenye tuzo, ndivyo kazi za wasanii zinakuwa na ubora na hatimaye kuvuka mipaka ya nchi yetu.

Katika mfululizo wa makala haya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) linaeleza namna mtu anavyoweza kuja na wazo la kuanzisha tuzo mpya nchini. Ieleweke kwamba lengo la tuzo siyo kutafuta fedha na kufanya biashara bali kuthamini na kutambua mchango na kazi zinazofanywa na wasanii. Aidha, lengo lingine ni kujenga hamasa kwa wasanii kubuni kazi zenye ubora zenye kuweza kushindana miongoni mwao na kuibuka na ushindi katika ubora.

Malengo haya ndiyo sasa kwa pamoja yanakuja kwenye lengo kuu la tuzo ambalo ni kukuza na kuendeleza sekta husika. Yaani kadri wasanii wanavyoshindana kubuni kazi zenye ubora zinazoingia kushindana kwenye tuzo, ndivyo kazi za wasanii zinakuwa na ubora na hatimaye kuvuka mipaka ya nchi yetu.

Kwa maana hiyo kwa jinsi sekta ya sanaa na hata tasnia yenyewe ya muziki ilivyo pana haitarajiwi hata kidogo wadau kuja na miradi ya tuzo yenye kufanana katika kila kitu. Hata kama ni kufanana, basi Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) linatarajia uwapo wa ubunifu katika mifumo na taratibu za uendeshaji wa tuzo.

Mathalan, kwa muda mrefu tuzo za muziki za Kilimanjaro maarufu KTMA zimekuwa ndizo zikitamba na kudumu kwenye tasnia ya muziki. Tuzo hizi zinatumia mfumo wa Academy kupendekeza wasanii kwa kila kipengele kinachoshindaniwa na baadaye wananchi kuruhusiwa kupiga kura na kuamua mshindi. Aidha, majaji wamekuwa na nafasi katika kuangalia weledi na ubora ingawa hawawezi kupindua kura za wananchi.

Sasa katika hali ya kawaida, Baraza halitarajii mdau mwingine kuanzisha tuzo kwa kufuata mfumo na taratibu hizi za KTMA. Mategemeo ni kupata fikra na mawazo ya tofauti ambayo yatamtambua na kumthamini msanii katika maeneo mbalimbali.

Kwa mfano, ukiacha mfumo huo wa KTMA ambao unahusisha wananchi kuamua nani awe mshindi kwenye vipengele mbalimbali vya tuzo kwa sasa teknolojia ya mawasiliano na hata uendeshaji wenyewe wa tasnia ya sanaa imekua kwa kasi.

Kuna kampuni zinazofanya biashara ya kuuza wimbo mmojammoja wa msanii sokoni kupitia mtandaoni, kuna yale yanafanya kazi ya usambazaji wa kazi za wasanii kupitia mfumo wa stempu za ushuru wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Aidha, kuna kampuni imewekeza teknolojia ya kuweza kutambua ni mara ngapi katika wiki na hata mwaka wimbo wa msanii fulani umechezwa kwenye kituo cha redio au runinga ukilinganisha na wenzake.

Ukiyatazama maendeleo haya yote kwenye tasnia ya sanaa hasa muziki utaona fursa kubwa iliyopo kwa kampuni kuwekeza katika tuzo ambazo hazihitaji wananchi kupiga kura ili kuamua mshindi.

Kuna fursa ama ya kuwa na tuzo ambazo zinaweza kujikita katika kutambua na kuwapa tuzo wasanii au kazi zao kulingana na mwenendo wa usambazaji sokoni au kutoa tuzo kwa kufuatilia mwenendo wa mauzo ya kazi za wasanii kwenye mitandao.

Pia, kuna fursa ya kutoa tuzo kwa wasanii au kazi zao kwa kuzingatia watazamaji (viewers) kwenye mitandao ya kijamii au namna wimbo ulivyoombwa na kuchezwa kwenye vituo vya radio au luninga. Yote haya yako wazi na ni mfumo wa uhakika na wa wazi wa kuendesha tuzo pasipo malalamiko maana uhalisia ndiyo hutawala.

Moja ya maeneo haya yanaweza kuzalisha tuzo nyingi za muziki kulingana na ubunifu na utofauti wa uendeshaji. Mfano mdogo tu, kama mdau akichukua eneo la uuzaji wa nyimbo mitandaoni anaweza kabisa kuwapanga wasanii katika vipengele mbalimbali na kuja na wazo la tuzo zenye utofauti na mvuto wa hali ya juu.

Taarifa za mauzo ya kazi za wasanii katika mfumo wa albamu zinapatikana

TRA, taarifa za nyimbo za wasanii kuchezwa kwenye vituo vya radio na luninga ziko wazi na zinapatikana. Rekodi za mauzo ya nyimbo za wasanii mitandaoni ziko wazi kama ilivyo za idadi ya watazamaji wa kazi za wasanii mitandaoni.

Kwa hiyo, kama ni mtu kujikita kuandaa tuzo zenye kulenga moja ya maeneo hayo kuna uwezekano kabisa kukawa na tuzo nyingi za kisasa na za kisayansi zenye kulenga uhalisia wa mafanikio ya msanii kulingana na maendeleo ya kazi zake.

Hata hivyo, pamoja na kuwepo kwa fursa pana katika sekta ya sanaa bado wadau wanaojitokeza kutaka kuendesha tuzo wote wanaangalia eneo moja tu. Itaendelea…

Kwa mawasiliano, maoni na ushauri wasiliana nasi kwa e-mail;[email protected] simu; 0756 700 496/0715 082 889/0715 973 952