Kwa nini Bi Kidude na Kanumba hawatumii Instagram?

Wakati nguli wa muziki wa Rege duniani, Bob Maley anafariki mwaka 1981, hakukuwa na mitandao kama Instagram, YouTube na Spotify lakini sio ajabu kumuona hii leo katika mitandao hiyo na akadiriwa kutengeneza Sh388.3 bilioni kila mwaka.

Hadi leo wasanii wakubwa duniani waliofariki kama Michael Jackson, 2Pac, The Notorious B.I.G, Whitney Houston, Aaliyah Haughton na John Lennon kurasa zao za mitandao ya kijamii tena zilizoidhinishwa zinafanya kazi.

Baadhi yao wamefariki kabla ya kushika kasi mitandao ya kijamii mwanzoni mwa 2000, mfano 2Pac (1996) na The Notorious B.I.G (1997), lakini menejimenti zao ziliona umuhimu na fursa zilizopo kwenye mitandao. Ni hatua nyingine ya kuuza, kulinda na kuendelea kuenzi chapa, kazi na taswira ya msanii husika kwa vizazi vya sasa na vijavyo, ukuaji wa digitali duniani ndio hasa umetengeneza jukwaa hilo.

Hata hivyo, nchini Tanzania mambo ni tofauti kabisa, hakuna kurasa wala akaunti rasmi mitandaoni za watu mashuhuri katika sanaa waliotangulia mbele za haki, kama Bi Kidude, Steve Kanumba, King Majuto, Ngwea, Sajuki, Godzilla, Sharo Milionea na wengineo.

Aina ya mikataba ya usimamizi wa kazi zao wanayoingia wasanii Bongo imetajwa kama kikwazo hadi kushindwa kuendeleza na kuenzi alama, kazi na chapa wanazoacha baada ya kufariki.

Uchunguzi wa The Guardian, Uingereza ulibaini ifikapo mwaka 20100, miaka 77 kutoka sasa, watu bilioni 5 waliokuwa wanatumia mtandao wa Facebook watakuwa wamefariki na kuziacha akauti na kurasa zao.

Akilizungumzia hilo, msanii wa Bongofleva na mbobezi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), King Kapita anasema kwa Tanzania inaonekana kuwa vigumu kutokana na suala zima la hakimiliki, wasanii wengi wakishafariki haki zao huwa hazina menejimenti maalumu ya kuzisimamia ipasavyo

“Menejimenti zinazosimamia wasanii wengi hazjiendelezi kielimu, msanii akishafariki kila mtu huangalia kilichobaki na kugawana bila kujali kuwa kuna uwekekano wa kuja vitu vingi kama fursa za kibiashara baadaye” anasema King Kapita ambaye aliunda kundi la Wakacha wakiwa na kina Jux.

Mtandao wa Facebook ambao unakadiriwa watumiaji wake milioni 30 wameshafariki, Februari 2015 iliruhusu watumiaji kuteua rafiki au mwanafamilia kuendesha ukurasa wa aliyekufa au kuufuta kabisa.

Kwa upande wake msanii Hip Hop Bongo, Wakazi anasema sio kila msanii anayefariki alikuwa na menejimenti, na hata walionazo ni vigumu kufanya hivyo kwa sababu ya aina ya mikataba wanayoingia.

Hata hivyo utafiti uliofanywa na tovuti ya money.co.uk mwaka uliopita, ulibaini kuwa Bob Maley anatengeneza Dola1.66 milioni, wastani wa Sh388.3 bilioni kila mwaka kwa machapisho yake Instagram na usikilizaji wa nyimbo zake Spotify na YouTube.

Aliyekuwa msanii wa Rock Marekani, Elvis Presley ambaye alifariki mwaka 1977 ndiye anamfuatia Bob Maley kwa ukaribu akiwa anaingiza Dola1.60 milioni, wastani wa Sh374.2 bilioni kila mwaka.

Ikumbukwe mitandao yote hiyo ilianzishwa baada ya vifo vyao, Instagram (2010), YouTube (2005) na Spotify (2006) ambao una watumiaji milioni 489 kila mwezi, huku milioni 205 wakiwa kwenye huduma ya malipo, data hizo ni hadi kufikia Desemba 2022.

Utafiti huo ulijumuisha akaunti rasmi za Instagram, Spotify na YouTube za wasanii 50 duniani waliofariki, kisha kutoa makadirio ya mapato ya kila mmoja kulingana na idadi ya wanaosikiliza kazi zao na wafuasi walionao.