Lamata: Askari Polisi wameigiza Katika filamu yangu
Muktasari:
- Mwanamke huyo mwenye umbo kubwa, mchangamfu, mnene na mweupe kiasi ni miongoni mwa waongozaji filamu wa kike wachache wanaotisha katika katika tasnia hiyo.
Wapo Watanzania wengi ambao wamepata mafaniko makubwa kutokana na kufanya vizuri katika uigizaji na utayarishaji wa filamu nchini.
Pamoja na mafanikio hayo, uliwahi kusikia au kuona filamu ambayo waigizaji ni askari wa Jeshi la Polisi Tanzania?
Unaweza kujiuliza nani amewaruhusu kucheza filamu hiyo, maana wanatumia silaha na sare za jeshi hilo. Hilo linawezekana kama muandaaji wa filamu hiyo ataomba na kuruhusiwa kuwatumia askari hao katika filamu yake, pia filamu husika lazima stori yake ikubalike, stori ambayo inalenga zaidi kuelimisha jamii na si vinginevyo.
Mmoja wa watu waliofanikiwa kuandaa filamu hiyo inayoitwa ‘The safe Catch’ ni Leah Mwendamseke maarufu kama Lamata.
Mwanamke huyo mwenye umbo kubwa, mchangamfu, mnene na mweupe kiasi ni miongoni mwa waongozaji filamu wa kike wachache wanaotisha katika katika tasnia hiyo.
Uigizaji wa kuvutia, uchangamfu unaopambwa na nguo zilizopangiliwa vizuri unaofanywa na muigizaji Jackline Wolper, unachangiwa kwa kiasi kikubwa la Lamata, ambaye pia ni meneja wa msanii huyo.
Starehe:Mambo vipi?
Lamata:Poa, lete stori.
Starehe: Kwa nini uliamua kuwa muongozaji wa filamu?
Lamata: Awali sikuwahi kuwa muongozaji wa filamu, bali nilikuwa mwandishi wa maudhui ya filamu.
Starehe: Nini sababu za kutoka huko na kuingia kwenye uongozaji wa filamu?
Lamata: Nilipokuwa nikiandika maudhui ya filamu waongozaji walikuwa hawafanyi kile ninachotaka, ilifikia wakati nilikuwa mpaka nalia kutokana na jinsi walivyokuwa wanavuruga nilichokipanga.
Starehe: Ujuzi wa kutambua upigaji picha mbaya na mzuri, uliupatia wapi?
Lamata: (Kicheko), hata mimi sijui, nilipoanza uandishi nilitamani sana kuwa muongozaji wa filamu, naweza kusema kuwa uwezo huo nilikuwa nao, lakini sikuwa nikitambua hilo. watu ndiyo walikuwa wakiniambia kuwa naweza.
Starehe: Baada ya kukwambia kuwa unaweza kuwa muongozaji ulichukua hatua gani? Je, kuna waliokusaidia?
Lamata: Hapana, hakukuwa na mtu zaidi ya mimi mwenyewe kuamua kuanza kufuatilia kazi za waongozaji wengine, ikiwemo pamoja na kusoma vitabu vya waongozaji wa filamu. Nilitaka kuwa muongozaji mzuri wa filamu ili kufikia malengo yangu, hasa kufuatilia kwa usahihi nilichokiandika katika maudhui.
Starehe: Unaikumbuka filamu ya kwanza kuiongoza?
Lamata: Filamu ya kwanza ilikuwa ya Jackline Wolper inaitwa Candy. Filamu hiyo ndiyo ilimfanya Wolper kunikubali na kunieleza kuwa atutafanya kazi pamoja, huo ndiyo ukwa mwanzo wa kuingia mkataba wa kuwa meneja wake.
Starehe: Tangu uanze kazi hii mpya, filamu ipi ilikusumbua zaidi wakati ukiiandaa?
Lamata: Ni filamu ya ‘ The safety Catch’ ambayo itatoka Septemba au Oktoba mwaka huu, hii ni filamu yangu ya kwanza ya mapigano (action) tangu nianze kuongoza filamu. Unajua nini, katika filamu hii waigizaji zaidi ya 60 ni askari wa ukweli (Polisi), ni waigizaji wawili tu ambao si askari, silaha zilizotumika ni za kweli, filamu hiyo ina mapigano, yaani ni kukimbizana tu na silaha mitaani.
Starehe: Ilitumia mbinu gani mpaka polisi wakubali kuigiza filamu yako? Je, wameruhusiwa na mwajiri wao?
Lamata: Naishukuru Serikali kwa kutuunga mkono na kukubali kuwaruhusu askari hao kucheza filamu hiyo, filamu hii imelenga zaidi kuelemisha jamii, ndiyo maana ilikuwa rahisi kuwapata polisi na kutumia silaha za kweli.
Starehe: Wapo watu wanaoziponda filamu za Kitanzania, ikiwa ni pamoja na kukosa mpangilio, unalizungumziaje hilo?
Lamata: Hali hiyo inatokana na waongozaji wengi wa filamu kuiga filamu za nje, ndiyo maana filamu zao zinakosa mwelekeo kwa sababu wanaandaa kitu ambacho hawakukipanga na kikapangika, hilo linatokana na tofauti ya mazingira ya Tanzania na yale ya nchi za Ulaya au Amerika.
Starehe: Tangu uingie katika tasnia hii, umekutana na changamoto zipi katika utendaji wako wa kazi?
Lamata: Mbali na changamoto za kawaida, tatizo kubwa ni kuwa na mtaji mdogo wa fedha ambao unasababisha kuandaa filamu na kufanya kitu ambacho hukukusudia kukifanya. Kwa mfano, kuna baadhi ya filamu ukiwa unaongoza utahitaji makaburi halisi sita, jambo ambalo linahitaji fedha, kwani wachimbaji inatakiwa uwalipe Sh600,000 kwa kaburi moja, kitu hicho ni kigumu kukifanya.
Starehe: Je una mpango wa kuendeleza kipaji chako cha kuandaa filamu?
Lamata: Mungu akinijalia uzima na afya Juni, 2014 nitakwenda kusoma katika Chuo cha Brand University kilichopo nchini Uingereza.
Starehe: Nashukuru kwa ufafanuzi wako, nakutakia kila la kheri katika shughuli zako.
Lamata:Nashukuru karibu tena.
Wolper anamzungumziaje
meneja wake
Starehe:Mambo!
Wolper:Poa, mambo yanakwendaje?
Starehe: Safi, unamzungumziaje Lamata?
Wolper: Lamata ni Meneja wangu, ninafanya naye kazi kwa muda sasa, nikiwa naye nahisi niko huru zaidi kama kitu hakiwezekani anakuwa muwazi na tunakiacha hata kama kitakuwa na maslahi makubwa kwetu.
Starehe: Je, hayo yanatosha kukufanya umuamini?
Wolper: Hiyo ni moja ya sababu niko naye kwa sababu anafanya kazi yake kwa ufanisi na kutambua majukumu yake kama Meneja na muongozaji wangu, kinyume na hapo siwezi kufanya naye kazi.