Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Elimu yetu sawa na kuchuma papai kwenye mwembe - 2

Muktasari:

Kuelimisha watu ni sayansi ya kuumba mtu ili mtu aumbe huduma, vitu na atoe huduma pamoja na kutatua changamoto zake. Ni uwekezaji makini unaohitaji watu makini, mipango makini, ufanyike kwa umakini mkubwa na kwa manufaa ya wengi.

Hoja yangu tangu wiki iliyopita ni umuhimu wa kuelimisha watu kwa usahihi. Nilisema kuwa kuelimisha watu siyo suala la hiari, siyo suala la kubahatisha, siyo suala la miujiza wala kuhadaa watu. Ni hatua za kifikra na vitendo sahihi. Ni kipaumbele namba moja kwa nchi yoyote.

Kuelimisha watu ni sayansi ya kuumba mtu ili mtu aumbe huduma, vitu na atoe huduma pamoja na kutatua changamoto zake. Ni uwekezaji makini unaohitaji watu makini, mipango makini, ufanyike kwa umakini mkubwa na kwa manufaa ya wengi.

Kuelimisha watu hutokea pale hatua za kivitendo zinaposhabihiana na maneno ya wafanya uamuzi. Hutokea pale fikra mpya zinapotawala mazoea, na uzoefu wa kuvuruga na kufanya kazi kwa mazoea kutupwa kando. Hutokea pale kinachoendelea darasani kati ya mwalimu na mwanafunzi kinashabihi mahitaji ya mtu mmojammoja na kinaendana na mahitaji ya jamii na kinachangia kuitoa jamii kwenye dhiki kuelekea kwenye neema.

Tukitaka wasomi sahihi lazima tutoe elimu sahihi. Tukielimisha watu ovyo ovyo tutapata wasomi wa ovyo ovyo, nchi haitasonga mbele.

Hatua ya kwanza ya kuelimisha watu ni kujenga utambuzi ndani yao ii wajitambue. Utambuzi ni weledi wa ung’amuzi wa vipawa ulivyoumbiwa na Mungu. Ni hali ya uelewa wa hisia, utashi, mitazamo na ujuzi wa kuitafsiri dunia na sababu ya mtu kuwapo duniani. Ni hali ya akili kufahamu mazingira yanayokuzunguka, wajibu wako wa ndani ya dhamira ya ndani na ya nje inayochangamanana mwingiliano wa uhusiano na watu wengine. Utambuzi ni kufahamu umeumbwa na nini, kwa manufaa gani, ili ufanye nini, kwa nguvu na muda upi kufanikisha nini na kwa manufaa ya nani.

Utambuzi ni tunu na zawadi kutoka kwa Mungu. Utambuzi haufundishwi darasani, hautokani na mtu kupata digrii, haukuzwi na shahada za uzamivu, haukuzwi na lugha ya Kiingereza wala Kifaransa. Huzalishwa na Mungu, hukuzwa na mila, desturi, jadi na misingi jadidi ya makuzi na malezi yanayojenga maadili ya mtu wa ndani.

Ni utambuzi ndio unaomjenga mtu kupata maarifa, ufahamu, weledi na hata umaizi. Ngazi ya kwanza kabisa ya kujenga mtu aliyekamilika kifikra na kimang’amuzi ni stadi ya utambuzi. Kujitambua ndiko kunajenga msingi wa kuelimika, kujitambua ndiko kunajenga msingi wa kuchanua vipaji, ndiko kuna weka weledi wa uvumbuzi na ubunifu.

Wanasayansi wote na wataalamu waliobobea kwenye uvumbuzi, ubunifu na ugunduzi waliochangia maendeleo ya sayansi na taknolojia, chanzo cha uwezo wao huo ni kujitambua kulikozaa michepuo ya akili inayovumbua, inayogundua, inayobuni na kung’amua maarifa mapya.

Bila kujitambua kwanza binadamu anaweza kupata digrii lakini hawezi kuelimika. Bila kujitambua binadamu anaweza kuitwa msomi, lakini asiye na maarifa, bila kujitambua kwanza digrii inaweza kuwa tiketi ya kumpeleka mtu kuzimu. Bila kujitambua hakuna usomi bali ni kukariri masomo na kuzika akili na vipawa asilia.

Hatujiulizi kwa nini wenzetu kama Wahindi, Wakorea, Wachina na Wazungu waliopo hapa Tanzania wanaendelea kung’ang’ania na kushikilia jadi zao, mila zao na asili zao? Wazungu wanaozunguka kila mahali dunia kwanini hawazitupi jadi zao, mila zao na asili zao? Kwa nini hawapotezi tunu asilia walioumbwa nazo? Jibu ni kwamba, wanafahamu humo ndimo kwenye vyanzo vya akili, ubunifu, uvumbuzi na umaizi; yaani, utambuzi!

Nimesema mara nyingi kuwa tunahangaika kumaliza silabasi badala ya kumaliza ujinga. Tutahangaika kupeana digrii, kujenga shule, kupeana ufaulu wa dezo kuunda sera na mipango lukuki, haya yote hayatatusaidia kama hatutang’amua siri ya maarifa na kuelimika ni nini. Bila kuboresha michepuo ya akili ambayo chanzo chake ni jadi, malezi stahiki, utamaduni na mila kukuzwa, hatuwezi kupata wavumbuzi na wagunduzi Tanzania.

Masomo tunayowafundisha watoto wetu sasa hayawaandai kutafuta suluhu au kujiuliza namna ya kujikwamua. Tumebaki kulalamika na kukosa matumaini. Kimsingi, elimu ya inayotolewa sasa inalazimisha kuua asili ya Mtanzania, kuua mila na desturi, kuua jadi ya mifumo asilia ambayo ndiyo chanzo cha utambuzi.

Sisi tunapigana vikumbo kubebeshana lundo la vyeti na digrii tukifikiri humo ndimo kuna elimu. Tumebeba zigo la vyeti na nadharia zisizotekelezeka na kusahau hata asili ya vipaji vyeti. Hakuna tunachoweza kufanya.

Vipaji tulivyozaliwa navyo vimetupwa kapuni, sasa ni kukariri nadharia mfu. Tukitaka barabara watakuja wenye maarifa kutujengea. Tukitaka majengo mazuri kwenye miji mikubwa watakuja wenye maarifa kutoka nje kutujengea. Hata kuvuna maji ya mvua hatuwezi japo tuna wasomi wa maji wenye digrii saba.

Narejea tena kusomea kuwa huwezi kupanda uyoga ukatarajia kuvuna mahindi. Huwezi kupanda mlimau ukatarajia kuvuna machungwa. Huwezi kupanda nadharia za masomo ukatarajia kuvuna maarifa au utaalamu.

Ukipiga porojo kwenye elimu utavuna porojo kwa wasomi. Ukifanya usanii kwenye elimu utavuna usanii kwa wasomi na watumishi. Ukiwapa watu elimu bandia utavuna watumishi bandia, mipango bandia, vyeti bandia, wabunge bandia, majaji bandia, walimu bandia, wanasheria bandia, wahandisi bandia, na mipango na sera bandia. Watawala wataendelea kusubiri kuvuna papai kwenye mwembe hadi lini?