Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shafi ADam Shafi: Galacha wa fasihi anayelia na uharamia wa vitabu

Shafi ADam Shafi

Muktasari:

Asema kwa mazingira yaliyopo nchini, uandishi ni utashi wa mtu na siyo njia ya kutafuta kipato

Kuna kila dalili kuwa fasihi Tanzania inaelekea shimoni, kizazi cha watunzi mahiri cha kina Shaaban Robert, Saadani Kandoro, Penina Mlama, Ibrahim Hussein na wengineo  kinaonekana kukosa warithi.

Wachache waliobaki na kujaribu kuvaa viatu vya magwiji wa fasihi, nao wanalia na changamoto mbalimbali ikiwamo wizi na uharamia wa kazi wanazotunga.

Changamoto hii pia ni kilio cha mmoja wa magwiji wa fasihi nchini, Shafi Adam Shafi, anayetamba na riwaya maarufu ya Kuli inayoendelea kutumika katika mitalaa shuleni.

Hata hivyo, uharamia wa kazi za galacha huyu wa fasihi umevuka mipaka ya kimataifa. Katika mahojiano na gazeti hili pamoja na masuala kadhaa kuhusu fasihi na uzoefu wake katika tasnia ya utunzi, anazungumzia namna kitabu chake cha Kasri ya Mwinyi Fuad kilivyotafsiriwa kwa njia ya wizi na mchapishaji mmoja nchini Ufaransa.

Swali: Unayatazamaje maendeleo ya tasnia ya utunzi wa vitabu sasa na zamani?

Jibu: Hivi sasa tasnia ya utunzi wa vitabu tunaweza kusema kuwa imeshuka kwa kiasi fulani. Huko nyuma, katika miaka ya 1970 waliibuka waandishi wengi ambao ni Said Ahmed, Faraji Katalambula, Hammie Rajab, Ben Mtobwa, Agoro Anduru, William Mkufya na wengine wengi. Hivi sasa kuna waandishi wachache  waliojitokeza kuwa waandishi mahiri akiwamo Hussein Tuwa na wengineo.

Uandishi wa vitabu umeshuka siyo kwa sababu hakuna waandishi, la hasha! Bali kuna uhaba wa vishawishi vya kuwasukuma wale wenye vipaji vya uandishi waandike. Huko nyuma vilikuwapo vishawishi vingi vya kuwachochea waandishi kuandika.

Kwa mfano, yalikuwapo mashindano ya muswada bora yaliyokuwa yakiendeshwa na Tepusa. Mashindano haya sasa hayapo. Yalikuwapo mashindano ya kitabu bora cha mwaka yaliyokuwa yakiendeshwa na Umoja wa Wachapishaji Tanzania wakati wa tamasha la wiki ya vitabu. Mashindano haya sasa hayapo tena. Yalikuwapo mashindano ya uandishi wa riwaya kwa wanafunzi wa shule za sekondari yaliyokuwa yakiandaliwa na Umoja wa Waandishi wa Vitabu Tanzania (Uwavita).

Swali: Ulianza kazi ya utunzi lini na vitabu vingapi umeshatunga hadi sasa?

Jibu: Nilianza rasmi utunzi wa vitabu mwaka 1968, kitabu changu cha kwanza kilitoka mwaka 1978, hadi sasa vitabu vitano ambavyo ni ‘Kasri ya Mwinyi Fuad’, ‘Kuli’, ‘Vuta n’ kuvute’, ‘Haini’ na ‘Mbali na Nyumbani’. Pia nimeandika vitabu vingine kadha ambavyo siyo riwaya.

Swali: Umekumbana na changamoto zozote katika kazi hii?

Jibu: Changamoto kubwa niliyopambana nayo katika uandishi ni pale kitabu changu kiitwacho ‘Kasri ya Mwinyi Fuad’ kilipotafsiriwa kwa lugha ya Kifaransa na mchapishaji mmoja huko Ufaransa. Niliwasilisha malalamiko yangu kuhusu wizi huo katika ubalozi wetu wa Ufaransa, lakini umeshindwa kunisaidia. Mpaka hivi sasa bado napambana na changamoto hii na naendelea kuwasiliana na wanasheria wa huko Ufaransa.

Changamoto nyingine ni pamoja na kukataliwa kwa muswada wa kitabu cha Kasri ya Mwinyi Fuad mwaka 1968. Ilinibidi nipambane na changamoto hii kwa kuufanyia marekebisho makubwa muswada huo mpaka ulipokubaliwa na mchapishaji.

Swali: Je, utunzi wa vitabu hapa nchini unaweza kumsaidia mtu kukuza kipato.

Jibu: Kwa mtizamo wangu kwa mazingira ya Tanzania yalivyo, sidhani kama utunzi wa vitabu unaweza kumsaidia mwandishi kiuchumi. Nimesema hivyo kwa mazingira ya Tanzania ambapo pamoja na kazi nzuri inayofanywa na waandishi na watunzi pia hakuna anayethamini kazi yao zaidi ya kuwanufaisha wengine.

Swali: Kitabu chako maarufu cha Kuli kinaendelea kutumika katika mitalaa, unadhani maudhui yake bado yana nafasi katika dunia ya sasa ya utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia?

Jibu: Maudhui ya kitabu cha Kuli ni juu ya mapambano ya kitabaka, mapambano kati ya wafanyakazi na mabepari, kati ya mafukara na matajiri chini ya mfumo wa kibepari. Mfumo wa ubepari na unyonyaji bado upo na mapambano ya kitabaka bado yapo. Tena mapambano haya yamezidi zaidi katika dunia ya sasa ya utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Machafuko yote yanayotokea sehemu mbalimbali duniani, ni matokeo ya mapambano ya kitabaka. Ni matokeo ya mapambano kati ya wanyonyaji na wanyonywaji chini ya mfumo wa kibepari.

Kwa hiyo, maudhui ya kitabu cha Kuli bado yana nafasi kubwa katika dunia ya sasa ya utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia na kitaendelea kuwa na nafasi wakati wote ule ambao mfumo wa kibepari utakuwepo.

Swali: Tukiacha changamoto binafsi kama ulivyoeleza awali, changamoto gani zinaikabili tasnia ya utunzi wa vitabu kwa ujumla wake?

Jibu: Changamoto kubwa ninayoiona ni uchapishwaji wa kazi. Waandishi wamekuwa wakiendelea kuandika, lakini mara nyingi miswada yao huishia makabatini kwa sababu ya kukosa mchapishaji. Waandishi wengi wamekuwa wakiwasilisha miswada kwa wachapishaji lakini imekuwa ikikataliwa.

Hii ni changamoto kubwa kwani lazima ieleweke kuwa uchapishaji ni biashara na mchapishaji ni mfanyabiashara. Anapochapisha kitabu ni lazima ahakikishe kuwa kitabu anachokichapisha kitapata soko zuri na kumwezesha kurejesha gharama zake na kupata faida kidogo.

Katika hali kama hii, ufumbuzi kwa waandishi ni kuhakikisha kuwa wanaandika vitabu vitakavyoweza kukubaliwa na wachapishaji.

Changamoto nyingine inayoikabili tasnia ya utunzi wa vitabu ni uharamia wa haki miliki. Uharamia wa haki miliki ni wizi unaofanywa na wachapishaji wezi wanaochapisha vitabu vya wachapishaji halali kwa njia haramu.

Kwa tasnia ya uandishi wa vitabu, changamoto hii inazidi kuwa ngumu, kwani chombo cha Serikali kinachoshughulikia udhibiti wa haki miliki yaani Cosota, kinashughulika zaidi na kudhibiti uharamia wa muziki na filamu kuliko vitabu.

Swali: Una wito gani kwa waandishi vijana au watu wenye mapenzi na fani ya uandishi?

Jibu: Wasikate tamaa pale miswada yao inapokataliwa na wachapishaji. Kadhalika wasichoke kuufanyia kazi muswada pale unaposomwa na mtaalamu na kupewa maoni na mtaalamu huyo.

Pia wasiwe na haraka ya kutaka kuona miswaada yao imeshakuwa vitabu mara moja.

Ni lazima wawe na uvumilivu na watafute maoni ya watu wengine ili kuifanya miswada yao iwe bora zaidi. Kadhalika, uandishi ni utashi wa mtu siyo njia ya kutafuta kipato. Mtu asiingie katika fani ya uandishi kwa kutegemea kuwa uandishi utamletea kipato.

Nawashauri wasikimbilie kutaka miswada yao ichapishwe kuwa vitabu tu. Ni lazima watumie vyombo vingine kama vile magazeti na majarida ili miswada yao ichapishwe kidogokidogo katika safu za hadithi ndani ya magazeti na majarida.

Hii ni njia moja nzuri ya mwandishi kuweza kujijenga na kujitengenezea uwezekano wa kazi zake kuchapishwa kama vitabu.