Shule zizalishe watatua matatizo

Muktasari:

  • Shule inachochea vipaji, vipawa na uwezo wa watu katika kukabiliana na changamoto za maisha yao katika jamii husika.

Shule ni sehemu muhimu katika mustakabali wa Taifa.

Shule inachochea vipaji, vipawa na uwezo wa watu katika kukabiliana na changamoto za maisha yao katika jamii husika.

Shule ni wakala muhimu wa lugha, utamaduni, maadili, amani, umoja na kukuza uzalendo wa jamii husika.

Shule ni muhimu kama vile elimu kwa taifa ilivyo mhimili ambao huweza kujenga jukwaa imara la kudumisha upendo katika jamii kwa kujenga stadi za kutatua migogoro, kujenga umoja wa kijamii na mshikamano.

Upo umuhimu wa kuwa na elimu ya amani ambayo hulenga kuwasaidia wanafunzi kupata uwezo wa kuzuia na kutatua migogoro kwa amani inapotokea miongoni mwa watu, kati ya watu au baina ya makundi, kitaifa au kimataifa.

Malengo ya uwepo wa shule yanathibitishwa katika malengo ya elimu nchini ambayo baadhi yake ni kama haya yafuatayo:

Moja, kuelekeza na kukuza maendeleo, kuboresha haiba ya wananchi wa Tanzania, rasilimali zao na matumizi bora ya rasilimali hizo katika kuleta maendeleo ya mtu binafsi na ya kitaifa.

Mbili, kukuza upatikanaji wa fursa za kusoma, kuandika na kuhesabu na matumizi sahihi ya maarifa na stadi za kijamii, kisayansi, kiufundi, kiteknolojia, kitaalamu na aina nyingine za maarifa na ujuzi, kwa ajili ya maendeleo na kuboresha hali ya mtu na jamii.

Tatu, kukuza na kuendeleza kujiamini, kudadisi, weledi na kuheshimu utu wa mtu na haki za binadamu na kuwa tayari kufanya kazi kwa kujiendeleza na kwa maendeleo ya taifa.

Nne, kuwezesha na kupanua mawanda ya kujipatia maarifa, kuboresha na kukuza stadi za kiakili, kivitendo, uzalishaji na nyinginezo zitakiwazo katika kukidhi mabadiliko ya mahitaji kiuchumi.

Tano, kumwezesha kila raia kuelewa misingi ya Katiba ya nchi pamoja na kuthamini haki za binadamu na uraia, wajibu na majukumu yanayoendana nayo.

Sita, kukuza utashi wa kupenda na kuheshimu kazi za kujiajiri na kuajiriwa na kuboresha utendaji kazi katika sekta za uzalishaji na huduma.

Ni wajibu wa wasomi popote pale duniani kuja na majibu ya changamoto na matatizo yanayoikabili jamii yao; wanaposhindwa kufanya hivyo, wanakuwa kama wasaliti wa elimu yao na jamii. Shule ni kichocheo cha mawazo hayo yenye majibu.

Shule huanzia katika kaya, katika jamii ambayo hugusa mfumo wa elimu isiyo rasmi na yenye mtalaa usioonekana mpaka shule ambayo wengi husema huwakilisha mfumo wa elimu rasmi.

Zao bora la shule hupaswa kuonekana katika jamii kwa kuwa na watu walioelimika ambao huweza kuthubutu kuhoji mifumo kandamizi, kujiamini kusimamia ukweli ulio kweli daima na wala siyo ukweli wa kipindi fulani.

Pia, kushauri kama wataalamu wa eneo husika na huwa sehemu ya majibu ya matatizo yanayowakumba wao kama binadamu, matatizo ya jamii yao na zaidi matatizo ya ulimwengu kwa sababu nao ni sehemu yake.

Kinyume cha hayo ni wasomi kuonekana kuwa sehemu ya matatizo badala ya kuwa sehemu ya majawabu au suluhisho.

Aidha, kwa wasomi kutoona fursa mbalimbali za uzalishaji mali, ni uthibitisho wa kuwepo kwa tatizo la kuachana kwa mahitaji ya shule na mahitaji ya jamii ambapo hatari yake inawezekana jamii ikawa na wasomi ambao huishia tu kulalamika.

Uwezekano huo ni mkubwa wa kuwa na wasomi ambao hata wanapohitimu elimu ya juu, bado wanajikuta hawakidhi mahitaji ya kitaaluma yanayohitajika katika jamii na hivyo kuwalazimu kwenda tena kusoma kozi fupifupi ili kupata stadi.

Hili kwa hakika sio suala la kiafya kwa mustakabali wa nchi yetu.

Pia, jamii kujikita katika ushindani wa vyeti na ufaulu wa majaribio na mitihani mbalimbali kuliko kusisitiza katika umahiri wa stadi na maarifa na uwajibikaji; hizi ni baadhi ya changamoto zinazopaswa kujibiwa na elimu inayotolewa katika hatua mbalimbali za kielimu nchini.

Ni dhahiri shule zinapaswa kuwa kitovu cha elimu bora. Mathalani, katika karne hii ya sasa, ili kila mtu aweze kuboresha maisha yake na ya jamii yake, lazima awe na elimu.

Elimu hiyo iliyo bora ndiyo humwezesha mtu huyo kujitambua na kujimiliki yeye mwenyewe kwanza.

Pia humwezesha kuzikabili changamoto ambazo humsonga, humwezesha kuyatawala na kuyatumia mazingira yanayomzunguka ili kuboresha maisha yake na jamii kwa jumla.

Ndani ya utandawazi ambao huchagizwa na maendeleo na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, elimu isiyotosheleza au isiyo bora, hutafsiriwa kuwa kichocheo cha umaskini na matatizo ya kimaadili na mengine mengi.

Wakati huohuo, elimu bora zaidi hupata tafsiri ya kuwa kichocheo cha maisha bora zaidi na uwajibikaji wa jamii kwa faida ya ulimwengu.

Hivyo, ili elimu iweze kuleta mabadiliko ya kweli kimaendeleo, ni lazima iwe elimu bora ambayo inalenga kumbadilisha mtu na kumwezesha kufikiri, kubuni, kujitambua, kuhoji, kudadisi, kupenda kazi, kuwa na mwenendo mwema na kuboresha afya na maisha yake binafsi na ya jamii.

Elimu ni ukombozi iwapo italenga kumpatia mtu uwezo wa kupambana na changamato zinazoikabili jamii na taifa kwa ujumla. Elimu inamjenga mtu kuwa raia makini na mzalishaji ndani ya nchi yake.

Ni vema mitalaa ya elimu na mafunzo katika ngazi mbalimbali za elimu, ikaendelea kuandaliwa kwa kuzingatia haki na kujenga Taifa lenye amani na utulivu.

Hii ni kwa sababu ubora wa elimu na mafunzo, unatokana na ubora wa mitalaa iliyopo, umahiri wa watekelezaji wa mitalaa hiyo, uongozi, usimamiaji, mazingira ya kutolea elimu na mafunzo, tathmini na rasilimali zilizopo.

Hivyo, jamii ya wasomi haina budi kuja na majibu ya changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa na dunia kwa ujumla.

Hili litawezekana tu kwa shule kuwa sehemu ya kutengeneza wasomi wenye upeo na umahiri wa kutatua matatizo yaliyopo, yajayo na ambayo hayajawahi kuwepo.