Tataki na maendeleo zaidi ya Kiswahili
Muktasari:
- Hilo limebainika hivi karibuni katika wiki ya utafiti iliyofanyika chuoni hapo. Miradi ya Tataki iliyoonyeshwa katika wiki hiyo ni pamoja na mradi wa kamusi ya simu ya kiganjani, mradi wa kutafsiri nyaraka na kuunda istilahi za Kiswahili na mradi wa Kiswahili kwa wageni.
- Katika makala haya, mradi wa kutafsiri nyaraka na kuunda istilahi za Kiswahili’ ndio utakaozungumziwa.
Kuongezeka kwa thamani ya Kiswahili, matumizi na mahitaji ya taaluma za Kiswahili duniani, kunaifanya Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, izidi kupanua wigo wa huduma zake.
Hilo limebainika hivi karibuni katika wiki ya utafiti iliyofanyika chuoni hapo. Miradi ya Tataki iliyoonyeshwa katika wiki hiyo ni pamoja na mradi wa kamusi ya simu ya kiganjani, mradi wa kutafsiri nyaraka na kuunda istilahi za Kiswahili na mradi wa Kiswahili kwa wageni.
Katika makala haya, mradi wa kutafsiri nyaraka na kuunda istilahi za Kiswahili’ ndio utakaozungumziwa.
Kutokana na mwingiliano mkubwa wa jamii na tamaduni, kumekuwa na hitaji kubwa la kutafsiri nyaraka mbalimbali kutoka katika lugha moja kwenda nyingine.
Kazi hiyo ni moja ya majukumu ya Tataki kupitia kituo chake cha istilahi, tafsiri, ukalimani na teknolojia ya lugha.
Kwa wakati huu ambapo utandawazi umeshamiri, kumekuwa na mahitaji makubwa zaidi ya ufasiri wa nyaraka mbalimbali.
Kutokana na hitaji hilo, Tataki imeamua kujizatiti maradufu ili kuwawezesha wahitaji wa huduma hiyo kutokwama kwa namna yoyote.
Taasisi hii ya Serikali ambayo miongoni mwa majukumu yake ni kuandaa wataalamu wa lugha, kufanya tafiti na kutoa matokeo ya tafiti hizo; ina wajibu wa kukiendeleza Kiswahili na kuwawezesha wadau na wapenzi wa Kiswahili kupata huduma mbalimbali wanazohitaji, huduma ya kutafsiri nyaraka mbalimbali ikiwemo.
Dk Shani Omari, mkuu wa kitengo cha istilahi, tafsiri, ukalimani na teknolojia ya lugha, ambaye pia ni msimamizi wa mradi wa kutafsiri nyaraka, anaeleza kuwa kwa muda mrefu kumekuwa na tatizo la ufasiri wa nyaraka.
Kwa kuwa tafsiri ni taaluma, wakati mwingine kumekuwa na wafasiri ambao hawana weledi katika uga huo hivyo kubananga kazi za watu.
Kwa kubaini hilo, Tataki imejizatiti kutoa huduma bora za tafsiri za lugha mbalimbali. Lengo la kufanya hivyo ni kukuza na kueneza Kiswahili kote duniani.
Anasema, “Tunatafsiri nyaraka, mikataba, sera, sheria, tovuti na majina ya nyadhifa na vitengo anuwai vya kiserikali na binafsi…”
Dk Omari anasema kuwa, wao kama taasisi ya Serikali, wanafanya huduma hiyo kwa gharama nafuu, lengo likiwa ni kuwahudumia Watanzania na watu wengine kwa ajili ya kukiendeleza Kiswahili.
Anaongeza kusema, “Tafsiri tunazofanya zinahusisha kufasiri Kiswahili kwenda Kiingereza, Kifaransa, Kichina, Kijerumani, Kikorea na lugha nyingine za kigeni; tunaamini kuwa, kwa kufanya hivyo tunazidi kukisambaza Kiswahili katika mataifa mbalimbali duniani.”
Neema Sway, msimamizi msaidizi wa mradi huo, anafafanua kuwa, wao kama taasisi wameazimia pia kufanya kazi na kampuni mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya viwanda ili kufikia lengo la ‘Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati’.
Anasema, “Tafsiri tunazofanya licha ya kuwawezesha watu kuelewa matini husika, zinakuza lugha na wakati mwingine kutupatia istilahi mpya…”
Matokeo tarajali ya mradi huu wa tafsiri ni kuwawezesha wananchi kupata taarifa muhimu kwa lugha wanayoielewa; asasi anuwai kuwa na nyaraka za Kiswahili na kuweza kufikisha huduma kwa wateja, hivyo kuharakisha maendeleo na kupatikana kwa istilahi nyingi zaidi zitakazoendeleza lugha ya Kiswahili.
Dk Omari anatoa wito kwa Watanzania, asasi na kampuni kufasiri kazi zao kitaaluma ili kukiendeleza Kiswahili na kutunza hadhi yake.