Madogo wa IT jiongezeni muokote maokoto

Muktasari:

  • Wakati wa ujenzi wa msingi wa nyumba mawe huwa ni kitu cha kwanza kwa umuhimu. Lakini nyumba ikishapauliwa, mawe yote hukusanywa na kutupwa nje ya eneo.  Labda mjenzi akifikiria kuzungusha ukuta nyumba yake, hapo mawe yatatafutwa tena.

Kila jambo lina wakati wake. Suleiman alisema kuna wakati wa kuokota mawe na wakati wa kutupa mawe. 

Wakati wa ujenzi wa msingi wa nyumba mawe huwa ni kitu cha kwanza kwa umuhimu. Lakini nyumba ikishapauliwa, mawe yote hukusanywa na kutupwa nje ya eneo.  Labda mjenzi akifikiria kuzungusha ukuta nyumba yake, hapo mawe yatatafutwa tena.

Watu wengi wanakosea kudhani kwamba simba anakula majani pale anapokosa nyama. Kiu ya maji haiwezi kukatwa na bia, hivyo mwili wa kiumbe yeyote hutafuta kile unachikihitaji kwa wakati.

Anapohitaji maji hatakula nyama kama mbadala wa maji, na anapohitaji majani kama dawa ni lazima ayale ili kukidhi mahitaji ya mwili wake. Ukiwa na kiu ya kabia ka baridi, hata umwe pipa zima la maji haitasaidia.

Hapa duniani tumefundishwa kushukuru kwa kila jambo. Kama ni jambo zuri basi huwa faida kwa anayelipokea, lakini likiwa baya basi huenda likawa hasara kwake. 

Jambo lolote gumu huja na fursa inayoweza kuwa msaada kwa wengi na kwa muda mrefu. Binadamu alipata maendeleo kupitia changamoto.

Watu wa kale waligundua moto, meli, bunduki na kadhalika kutokana na changamoto.
Sasa tupo kwenye wakati wa sayansi na teknolojia. Kila mtu analazimika kuwemo kwenye mtandao huo apende asipende. 

Maisha yamehamia humo kwani kuna mambo mengi yanayohitajika maishani kama elimu, mawasiliano, ajira, biashara na kadhalika. 

Watu wengi duniani wamejiongeza kwenye matumizi ya teknolojia na wamejikuta wakiondokana na baadhi ya matatizo yao.

Penye mzoga ndipo wanapokutana nzi, lakini kama kawaida penye miti panakosekana wajenzi. Vijana wa sasa wana nafasi kubwa ya kujipatia maendeleo kwa kutumia teknolojia. 

Tofauti na zamani ambapo haikuwezekana kwa mtu binafsi kumiliki nyenzo za mawasiliano kama kompyuta, hivi sasa bidhaa hizo zinapatikana kirahisi na kila mahali.
Kompyuta hizo zilijengwa kwa ukubwa wa nyumba, na muundo wake uliwataka watumiaji kwenda kozi ya utaalamu wa kuiendesha mitambo hii. 

Hata hivyo, kutokana na ulimwengu wa teknolojia kwenda kasi, mwanadamu alifanikiwa kuuhamishia mtambo mezani na hatimaye kiganjani. Sasa kila kinachoweza kufanyika kwenye kompyuta kinafanyika pia kwenye simu janja.  

Toka vijana wetu wapewe uwezo wa kutumia simu janja kama kompyuta, tumeona baadhi ya fursa zikifikiwa kwa urahisi. Wapo wachache wanaofanya kazi kwa weledi na kurahisisha maisha, japokuwa wapo wengi wanaofanya madudu na kuharibu maisha.  

Hili linafanana sana na kumiliki silaha. Baadhi ya vigezo vya kumiliki ni uraia, akili timamu na umri. Kigezo cha umri kinamhakikishia mmiliki wa silaha kutumia silaha yake kwa maamuzi ya kiutu uzima.

Hata kama atavamiwa, mtu mzima anaweza kutotumia silaha aliyonayo kwa kuhofu usalama wa silaha hiyo. Pia anaweza kutoitumia kuepusha madhara kwa wengine wasio na hatia.

Ni tofauti na mtoto anayeweza kuitumia kwa kujifurahisha. Anaweza kukesha akiwatungua popo. Yupo mmoja aliyeingia shuleni na bunduki, akasimama kwenye lango la ofisi za walimu na kuwaamuru wabusu viatu vyake kwa zamu. 

Hivyo hata matumizi ya mtandao yanapaswa kuwekewa vigezo.
Labda awali tutafakari faida na hasara za mitandao (hasa ya kijamii). Kwangu naona ni njia rahisi ya kuhabarika, kuburudika na kuelimika. Lakini ni lazima pia tuelewane ni nini hasa wasomaji wanachohitaji. 

Ni mikwatuo na mashauzi, au habari na elimu?

Jibu rahisi “Ni vyote” kwa sababu dunia ina watu wa kila aina. Wapo watu wenye akili zao wanaosikiliza muziki, lakini pia wapo wajinga wanaosikiliza muziki.

 Kila mmoja kati ya hao wawili ana tafsiri yake katika kila neno analolikuta mtandaoni. Magwiji wa mitandao wanajua mbinu za kila aina za kuwavuta mashabiki. Anaweza kukuvuta kutoka nchi kavu akakutosa baharini. Au akakutoa baharini na kukutupa motoni.

Kwa jinsi anavyokujengea mazingira ni lazima utakubali tu. Ndiyo maana nilitaka tujiridhishe kwanza; watu wanafuata nini instagram? Kwa taarifa yako bingwa aliyekusanya mashabiki wengi instagram alitumia picha ya yai kama yai. 
Inawezekana picha hii ya yai liliwafanya watu wajiulize maswali mengi. “Kuna nini cha ziada kwenye yai hili?”

Huu ni wakati uliokuwa ukisubiriwa na wengi kwa muda mrefu. Vijana Watanzania wanajulikana kuwa mahiri kwenye ubunifu. Iwapo wangekuwa na uwezo wa kusafirisha na kuonesha bidhaa zao ulimwenguni, wangeweza kuwa matajiri wa kutupa duniani kote.
Lakini kwa umasikini wao uliokithiri, walibaki na bunifu zao zikawaozea masandukuni.

Mimi mpaka sasa nashangaa tunazalisha wataalamu wa IT wanaoongeza idadi ya wazururaji mitaani. Wataalamu wengine wanazalisha matusi yasiyovumilika mitandaoni. Laiti mabwege hawa wangejua matumizi sahihi ya akili, nchi ingekuwa mbali sana.