MAONI YA MHARIRI: Tuchangamkie fursa za mikataba hii

Muktasari:

Mbali ya kutoa fursa hiyo, nchi hiyo ilikubali kuimarisha na kuboresha kilimo cha mazao hayo kwa kusaidia teknolojia, mbegu na mbolea mwafaka.

Julai mwaka huu, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi alifanya ziara ya kikazi nchini ambako pamoja na mambo mengine, alisema nchi yake inahitaji zaidi ya tani milioni saba za mazao jamii ya kunde hususani, choroko na dengu.

Mbali ya kutoa fursa hiyo, nchi hiyo ilikubali kuimarisha na kuboresha kilimo cha mazao hayo kwa kusaidia teknolojia, mbegu na mbolea mwafaka.

Mwaka jana Tanzania iliuza tani 100,000 za mazao hayo yenye thamani ya dola za Marekani milioni 200, kiasi ambacho ni kidogo mno kulinganisha na mahitaji ya nchi hiyo, hiyo ikiwa na maana kwamba ipo fursa kubwa inayoweza kuwakwamua wakulima wetu na nchi kwa ujumla.

Juzi, Tanzania ilipata fursa nyingine baada ya Serikali kutiliana saini mikataba 21 ya makubaliano (MoU) na Morocco katika nyanja mbalimbali zikiwamo za kilimo, gesi, madini na usafiri wa anga.

Miongoni mwa mikataba hiyo ni ule wa makubaliano ya jumla katika ushirikiano wa uchumi, sayansi, ufundi na utamaduni; makubaliano kwenye sekta ya uvuvi; ushirikiano baina ya Shirika la Mbolea la Morocco (OCP) na Shirika la Mbolea la Tanzania katika kuendeleza soko la mbolea na kilimo nchini.

Pia mkataba wa ushirikiano baina ya kampuni ya kuchanganya chai ya Morocco na Kampuni ya Afri Tea and Coffee ya Tanzania.

Kama Rais John Magufuli alivyokaririwa akisema, makubaliano yote hayo yamelenga kuijenga Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati wa viwanda na kwamba hilo linawezekana kwa kuwa hata sasa hali ya uchumi wa nchi ni nzuri kwa kuwa unakua kwa asilimia 7.2; huku taarifa za uchumi zikionyesha kuwa kwenye robo ya pili ya mwaka, uchumi umekua kwa asilimia 7.9.

Tumezungumzia mikataba michache kati ya mingi mizuri na yenye manufaa kwa Taifa ambayo ilisainiwa juzi ikiwamo ahadi ya Mfalme huyo wa Morocco ya kujenga uwanja wa michezo mjini Dodoma ambao utakuwa mkubwa kuliko ule wa Taifa sambamba na kujenga msikiti mkubwa jijini Dar es Salaam.

Tumejikita zaidi katika mikataba inayohusu kilimo tukiamini endapo kutakuwa na mkakati wa mahsusi, itawakwamua Watanzania wengi hasa ikizingatiwa takwimu za miaka mingi kwamba sekta hiyo inabeba asilimia 80 ya wananchi wote.

Ili kunufaika na mikataba pamoja na fursa hizo, lazima kuwe na mipango iliyowekewa kimkakati itakayojumuisha ngazi zote husika kwa maana ya Serikali hadi kwa wakulima.

Tunataraji kusikia kutoka serikalini kupitia Wizara ya Kilimo na ile ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), zikiibua mikakati ya kuwafikia wakulima na kuwapa mbinu za kulima mazao ambayo soko linayasubiri.

Tunataka kuusikia wimbo wa kilimo cha zao hili lina soko Ulaya, India au kwingineko sambamba na uwazi katika utaratibu mzima kuanzia namna ya kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia, kuvuna, kufungasha, kusafirisha hadi kuuza.

Mambo yote hayo yakiwa wazi kwa kila mmoja na ukawepo utaratibu wa ufuatiliaji na tathmini (monitoring and evaluation), ndani ya miaka michache tutakuwa tumepata majawabu ya lile swali la kwa nini uchumi wa Tanzania unakuwa katika makaratasi lakini ukuaji huo hauonekani kwa wananchi.