NANI NI NANI SERIKALI YA JPM?: Selemani Jafo – Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora
Muktasari:
Jafo Selemani Saidi ndiye Naibu Waziri wa TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora. Wizara hii iko chini ya Ofisi ya Rais katika Serikali ya Awamu ya Tano, ameteuliwa katika baraza la mwanzo la mawaziri la Rais John Magufuli.
HISTORIA NA ELIMU
Jafo Selemani Saidi ndiye Naibu Waziri wa TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora. Wizara hii iko chini ya Ofisi ya Rais katika Serikali ya Awamu ya Tano, ameteuliwa katika baraza la mwanzo la mawaziri la Rais John Magufuli.
Hivi sasa Jafo ana miaka 42 na ifikapo mwezi Mei mwaka 2016 atatimiza miaka 43 kwani alizaliwa Mei 26, 1973, huyu ni mmoja wa mawaziri vijana kabisa kwenye siasa za nchi yetu.
Kama ilivyo kwa vijana wengi wa enzi hizo, Jafo alianza darasa la kwanza mwaka 1984 akiwa na miaka 11, katika Shule ya Msingi Kwala na kuendelea katika Shule ya Msingi Kisarawe ambako alihitimu darasa la saba mwaka 1990.
Elimu ya sekondari aliipatia katika Shule ya Sekondari Maneromango iliyopo hukohuko Kisarawe, hii ilikuwa ni kati ya mwaka 1991 hadi 1994 na baadaye kidato cha tano sita katika Shule ya Sekondari Minaki iliyoko jijini Dar es Salaam aliposomea mchepuo wa sayansi.
Baada ya kufaulu kidato cha sita vizuri, alichaguliwa kujiunga katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua) kilichoko mkoani Morogoro, huko akabobea katika masuala ya Uchumi wa Nyumbani na Lishe ya Binadamu (Home Economics and Human Nutrition), alikuwapo chuomo hapo kuanzia 1998 hadi 2001 alipohitimu na kutunukiwa Shahada ya Sayansi ya Uchumi wa Nyumbani na Lishe ya Binadamu (B.sc in Home Economics and Human Nutrition).
UZOEFU
Jafo alirejea nyumbani kwao Kisarawe mwaka huohuo 2001 na kupata ajira katika ya serikali, akafanya kazi kama Ofisa Kilimo wa Wilaya ya Kisarawe akisimamia miradi ya kilimo kwa wakulima wadogo na wakubwa, mbinu za ukulima wa kisasa na matumizi ya teknolojia katika kilimo. Aliifanya kazi hii kwa miaka minne hadi mwaka 2005.
Alipoacha katika Wizara ya Kilimo, Jafo Alijiunga na Shirika la Kimataifa la “Plan International” mwaka 2006 kama ajira mpya, akapewa wadhifa wa kuwa Meneja wa Tawi la Kisarawe. Shirika hili linafanya kazi katika nchi karibia zote ulimwenguni likijihusisha na ushirikishwaji wa watoto katika masuala muhimu, ulinzi wa watoto, usalama wa uchumi na kusaidia wakulima na wajasiriamali mbalimbali, masuala ya dharura, miradi ya kuinua elimu na miradi ya maji safi na salama.
Jafo alitumia vizuri programu za “Plan International” akajenga jina lake vijijini katika wilaya ya Kisarawe, ilipotimu mwaka 2010 akaona ni vyema aachane na sekta binafsi na kuingia bungeni ili kuvaa viatu vya aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kisarawe kupitia CCM wakati huo, Athumani Janguo.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 jimboni Kisarawe CCM ilishinda kwakupata kura 19,832 sawa na asilimia 78.15 na kumpa Jafo nafasi ya ubunge, mshindi wa pili kwenye uchaguzi huo alikuwa ni Kondo Adui Seif wa CUF aliyepata kura 3,577 sawa na asilimia 14.1 na mgombea wa Chadema, Kitiku Theodory Edward alipigiwa kura 1,153 sawa na asilimia 4.54
Baada ya utumishi wa ubunge wa miaka mitano ya kwanza (2010 – 2015), Jafo alishinda kura za maoni kwa mara ya pili ndani ya CCM kwa ajili ya kugombea kwenye uchaguzi wa Oktoba mwaka huu 2015. Alifanikiwa kumshinda mpinzani wake mkubwa kutoka CUF na Ukawa, Rashid Mwinshehe ‘Kingwendu’, msanii mkubwa wa vichekesho hapa nchini Tanzania. Jafo alipata kura 28,054 huku Kingwendu akipata 8,863.
NGUVU
Uzoefu na ushiriki wa Bunge la 10 ni jambo la kwanza linalompa nguvu Seleman Jafo. Kiongozi huyu kijana aliingia kwenye bunge la kumi na kujifunza mambo mengi na yapo yale ambayo aliyafanya kwa juhudi kubwa na yakaonekana na kila mtu. Mathalani, Agosti 2012 Selemani Jafo alifanya tukio la kishujaa sana bungeni, alisimamia hoja nzito ambayo ni nadra kukuta mbunge wa CCM ameisimamia. Hoja yake ilipelekea Bunge lipitishe azimio lililoridhiwa na Serikali kurudisha Bungeni Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kujadili mahususi kifungu cha ‘fao la kujitoa’.
Jafo ndiye alikuwa kinara wa kulipigania jambo hili ambalo lilikuwa na maslahi makubwa sana kwa taifa kuliko chama chake. Hakujali kama yeye ni mbunge wa CCM na kubebwa na ile kasumba ya wabunge wa chama hicho kukubali kila jambo ilimradi wahakikishe Serikali haisumbuliwi na mtu yeyote. Kituo cha Haki za Binadamu na Sheria (LHRC) ni moja kati ya taasisi muhimu zilizojitokeza hadharani kumpongeza Jafo, jambo ambalo pia huwa ni nadra kufanywa na taasisi huru kwa wabunge wa CCM.
Lakini pili, Kufanya kazi katika sekta binafsi kunamuongezea ujuzi wa kutosha wa masuala ambayo atakwenda kuyasimamia wizarani. Ikumbukwe kuwa wizara ya Tamisemi inashughulika na masuala mengi yanayowahusu wananchi wa vijijini, ikiwemo elimu na afya.
Hii ni wizara mtambuka ikihusu pia masuala ya watumishi. Uzoefu wa Jafo kufanya kazi vijijini na wananchi kupitia “Plan International” unambeba moja kwa moja. Kazi yake ni kuhamisha tu nini alijifunza katika sekta binafsi, kutambua nini kinafanyika serikalini na kwa utaratibu gani na kutumia maarifa ya ziada kufanya kwa ufanisi wa kutosha.
UDHAIFU
Mara kadhaa imewahi kutokea Jafo ameonekana “kuwananga na kuwakejeli” wapinzani bila hoja za msingi bungeni. Tabia ya namna hiyo kuna siku (kwenye Bunge la 10) iliwahi kuyumbisha Bunge na kutaka kuleta “kizaazaa”.
Jafo hivi sasa ni Naibu Waziri, bila shaka mapungufu hayo atapaswa kuyafanyia kazi kwa uthabiti. Huu ni wakati ambapo itampasa kujibu hoja za wabunge wote kutoka vyama vyote na kuweka pembeni kabisa masuala ya ushabiki na utetezi usio na hoja, wenye lengo la kuibeba CCM bila sababu.
MATARAJIO
Matarajio ya Jafo katika wadhifa anaopewa hivi sasa ni kutenda kazi na kutumia uzoefu na vipaji vyake bila kuangalia huko nyuma uwezo wake ulipimwa kiasi gani. Jafo anajipanga kuhakikisha kuwa changamoto za Tamisemi na Utumishi zinakuwa na utaratibu wa kushugulikiwa kama ambavyo wadau wa maeneo hayo wamekuwa wakidhani. Bahati nzuri yeye pia amewahi kuwa mtumishi wa umma na amefanya kazi na watu wa chini wanaohudumiwa na Tamisemi, anajua changamoto za kuwa mtumishi na za mazingira ya watendaji na wananchi wa kada ya chini, anasema anahitaji muda mfupi tu kujipanga na kukamilisha kazi kubwa.
Watendaji wa wizara hii ambao nimeongea nao wanasema kuwa kwa muda mrefu sana Serikali imekuwa ikitoa ahadi ya kurekebisha utaratibu wa utendaji ili kufanya mabadiliko ambayo kila mara wanayashauri katika idara zao, lakini hilo limekuwa halipewi uzito kwenye maamuzi ya juu ya viongozi wa Tamisemi. Mmoja ameniambia kuwa katika idara yao wameshaelekezwa kuorodhesha kero na changamoto zao na kwamba wanaweza kuwa na vikao vya ki-idara muda si mrefu, anasema wao wanaamini kuwa hivi sasa Serikali itapaswa kusikiliza ushauri wao ili mambo yabadilike. Watendaji wengi wanasema Tamisemi inahitaji waziri na naibu waziri wenye usikivu ili kufikia matarajio ya wananchi na watumishi wenyewe. Matarajio haya ya watendaji ni salamu tosha kwa Jafo na waziri wake, kwamba watapaswa kuwa wasikivu kiasi cha kutosha.
CHANGAMOTO
Changamoto kubwa ya kwanza itakayomkabili Jafo na waziri wake ni maslahi ya watumishi wa umma. Kwa miongo kadhaa sasa watumishi wa Serikali wamekuwa wakilalamikia hali ya kudharauliwa kwa maslahi yao. Wengi wao wanalipwa mishahara kiduchu huku wakifanya kazi kubwa kupitiliza na mara nyingi ikiwa nje ya muda halisi wa kazi. Na wakati huohuo kumekuwa na ongezeko kubwa la gharama za maisha huku wao wakiendelea kubanwa katika kipato kile kile.
Nyumba za watumishi, afya zao na vifaa vya utendaji kazi ni changamoto ambazo hadi leo zinasubiri muujiza kuondolewa. Ukienda katika maeneo ya miji na vijiji unakuta watumishi wa umma wakiwa hawajui nini wafanye ili kujikwamua katika mazingira magumu waliyomo, wengi wao huishi mbali maeneo yao ya kazi, wanatumia muda mwingi kusafiri kwenda kazini kuliko kufanya kazi zao. Hali hii imeendelea kukatisha tamaa na inahitaji suluhisho la kudumu. Ni Jafo na mwenzake ndiyo wanapaswa kuwa vinara wa utatuzi wa masuala haya magumu.
Kwa upande wa pili kuna mambo magumu kwenye utaratibu wa uendeshaji wa serikali za mitaa. Nchi nyingi duniani zilizopata maendeleo ya uhakika zimewekeza nguvu kubwa katika uendeshaji wa serikali za mitaa, serikali za mitaa zina madaraka na maamuzi muhimu yanayohusu masuala yote ya maisha ya wananchi kwa ngazi za chini.
Hapa Tanzania hali hiyo ni tofauti sana, pamoja na kuwapo kwa ngazi hii ya uongozi, “serikali haijashusha madaraka” ya kutosha kwa ngazi hizo. Watendaji na viongozi wa vijiji, mitaa, vitongoji wameporwa madaraka yao ya utendaji na amri zinazotoka ngazi ya kata na wilaya (halmashauri). Na hata ngazi hiyo ya halmashauri nayo kuna mambo mengi inakwama kwa sababu ya kusubiri miongozo na masharti lukuki kutoka Serikali Kuu. Kama hali hii itaendelea utakubaliana na mimi kuwa nchi yetu itachelewa sana kufikia maendeleo ya kweli.
Kama hiyo haitoshi, ngazi ya halmashauri na manispaa imekuwa ikijiendesha kwa uvundo mkubwa wa rushwa, ufisadi na matumizi makubwa ya pesa za umma kwa manufaa binafsi ya watendaji na viongozi. Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zinaonyesha kuwa manispaa na halmashauri nyingi zinaponda mabilioni ya fedha kila mwaka, badala ya kuingiza mabilioni hayo kwenye miradi ya maendeleo yanaishia mikononi mwa wakurugenzi, watendaji wa halmashauri, mameya, manaibu meya na madiwani.
Mchezo huu kwa kiasi kikubwa umekuwa ukifanywa endelevu, mbaya zaidi, viongozi wa Tamisemi wamekuwa wakiwalinda baadhi ya watendaji na viongozi waliofuja fedha za umma. Huenda hilo linafanywa kwa lengo la kutengeneza mtandao mpana zaidi wa ulaji kwenda ngazi ya taifa.
Jafo na mwenzake wana kazi kubwa ya kufanya kwenye eneo hili ili imani ya watendaji wa serikali za mitaa irejeshwe na wananchi wanufaike na kazi ya uwepo wa ngazi hiyo ya uongozi.
Kwa kiasi kikubwa, Tamisemi hawawezi kukwepa lawama zinazotokana na matatizo ya ardhi katika nchi yetu. Mamlaka zinazohusika na utapanyaji wa ardhi, kuigawa kwa njia za rushwa na upendeleo ni mamlaka za vijiji, vitongoji, mitaa na kata zikisimamiwa na halmashauri za wilaya na manispaa.
Tanzania inakua kwa kasi lakini kiholela huku maeneo mengi yakiendelezwa hovyo hovyo bila usimamizi thabiti wa Serikali. Hali hii inasababisha ardhi kuwa na ugomvi usiokwisha, ikiwa Jafo na mwenzake hawatakuwa makini na changamoto hii wanaweza kufanya vibaya sana katika uongozi wao.
Pamoja na kuwa ardhi ni suala mtambuka lakini ardhi ngazi ya chini inalindwa na mamlaka ambazo ziko chini ya Tamisemi Kwa hiyo Tamisemi ikiamua kulivalia njuga jambo hili, matatizo ya ardhi yatakwisha kwa wakati.
Katika ngazi ya siasa kumekuwa na tatizo la namna gani chaguzi za serikali za mitaa zinafanywa. Kwa kiasi kikubwa na mara kadhaa Tamisemi imewahi kuwa na rekodi za kukutana na wadau wa uchaguzi, kukubaliana nao namna ya kuendesha uchaguzi wa serikali za mitaa na kutunga masharti, kanuni na taratibu. Baada ya makubaliano ya awali, wakuu wa Tamisemi huenda kujifungia wizarani na kujitungia kanuni mpya za uendeshaji wa uchaguzi ambazo kwa kiasi kikubwa huwa na malengo ya kukisaidia chama tawala, mwisho wa siku chaguzi za serikali za mitaa katika nchi hugeuka kuwa tatizo na vurugu zilizopitiliza.
Hali hii ikiendelea inazidi kushusha hadhi ya wizara hii muhimu ambayo mbaya zaidi hivi sasa iko ofisi ya Rais kwa hiyo mambo yakiharibika naye hawezi kukosa lawama.
Katika hatua ya ukomavu wa kidemokrasia katika nchi ni vyema Jafo na waziri wake wakae chini na kuachana na mipango yoyote ya kuendelea kuufanya uchaguzi wa serikali za mitaa kama ngazi za CCM kupandia kuelekea ushindi wa uchaguzi mkuu ambao hufanyika mwaka mmoja baadaye. Hii itarudisha morali ya wananchi na ushiriki wao katika chaguzi hizo.
HITIMISHO
Naamini kuwa rais John Pombe Magufuli ana makusudi yake ya maana kumweka Jafo katika wizara hii. Kubwa kuliko yote, huyu ni kiongozi kijana anayekuja vizuri katika siasa za kitaifa, akiamua kujinoa zaidi na kufanya vizuri anaweza, kwa sababu anazo silaha zote muhimu, elimu, uzoefu wa utumishi serikalini, uzoefu wa ngazi ya juu katika shirika la kimataifa na kufanya kazi nyingi za kijamii na wananchi vijijini, uzoefu wa uendeshaji wa Bunge na kwa hiyo Serikali.
Jambo ambalo Jafo anapaswa kulitambua ni kwamba anakwenda kufanya kazi kwenye wizara yenye changamoto lukuki na sugu, lazima avae sura ya “simba” kila mara pale ambapo taratibu na kanuni za kazi zitakapovunjwa na watu walioko chini yake, hapo atakuwa anaitendea haki wizara hii, rais mwenyewe na wananchi.
Kuhusu Mchambuzi
Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii, ni mmoja kati ya vijana wenye uzoefu mkubwa na siasa za Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi (“Cert of Ling”), Shahada ya Sanaa “B.A” katika Elimu (Lugha, Siasa na Utawala), Shahada ya Umahiri (M.A) ya Usimamizi wa Umma na Shahada ya sheria (LLB); +255787536759, [email protected], https://www.facebook.com/JuliusSundayMtatiro/, - Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni binafsi ya mwandishi).