Ndani ya boksi: Uwoya na mkopo wa 'Sevisi' ya ndinga zake

Miaka kadhaa nyuma. Tuliambiwa jimbo la Calfornia, lilikuwa tajiri zaidi kwa Marekani. Uchumi wake ulikuwa sawa na wa Taifa la Ufaransa na mara tisa zaidi ya uchumi wa bara zima la Afrika. Unajua kitu kinachowapa nguvu ya uchumi? Soma mpaka mwisho.

Akili yake ilifunga ndoa na pesa ya burudani iliyozunguka kwenye mbavu zake. Ikamtii. Umaarufu wake ulikuwa tofauti sana na shati alilovaa siku zote. Wakati Kusaga akiwa ‘bize’ kuhesabu namba kwenye akaunti akawa ‘masta plani’ wa kila kitu pale mjengoni.

Hakujua kuimba ila alikuwa na sikio la tatu la muziki. Uliza wanaotamba hii leo kimuziki wakuambie. Hakujua kutangaza wala sauti ya kukita mawimbi ya radio. Lakini ndiye aliyemwambia Gardner ‘wei baki’ kuwa: ‘’I think wewe utafaa kwenye Bambataa’”. Sasa ndio ‘Kapteini’ imebaki stori.

Alipojua mtu fulani ni pesa yeye aligeuka mnyenyekevu mpaka unyenyekevu ungeshangaa. JK katika utawala wake mjengoni ilikuwa kama ofisi ndogo ya Ikulu ya Magogoni. Ukimshangaa Jakaya alivyojenga urafiki na mjengoni. Utakuwa ni boya. JPM siyo tu alikuwa rafiki yake. Alikuwa sehemu ya watazamaji na wasikilizaji wazuri wa mjengoni. Na akaenda mbali zaidi kwa kupiga simu mara kwa mara kwenye runinga hiyo. Huyu ni Ruge alipotumia vyema fursa ya kumiliki akili nyingi, jicho la kujua nani anafaa kuwa rafiki yake ili atengeneze pesa kupitia burudani. Utawala huu wa Mama Samia unaikosa akili ya kiumbe huyu kwenye sanaa. Yes! Alikuwa na mapungufu mengi sana kama binadamu. Alijijali yeye na taasisi yake siyo dhambi wala kosa kisheria. Alitumia nafasi yake kusaidia wanaomzunguka jambo tunalolifanya wengi.

Kwa akili yake alisaidia na pengine kuliko yeyote kabla na baada yake. Kuinua wanamuziki na sanaa ya muziki wenyewe. Ukaribu wake na JK, ukafanya Bongofleva itawale kuanzia mtaani mpaka Ikulu. Kilichofanyika ni kwamba ‘ungemesapu’ naye, ‘automatikale’ ungejiwekea uzio mkubwa kati yako na ‘indastrii’. Masilahi mapana ya muziki ndio yalimtengenisha na baadhi ya wasanii na kumuweka karibu na wasanii, wanasiasa na viongozi wengi. Usingetaja kitu chochote kuhusu Bongofleva bila ‘linki’ ya jina lake. Mazingira ya namna hii hutengenezwa na wenye akili kubwa. Akili kisoda huwezi kujiwekea himaya yako kwenye ‘indastrii’ yoyote kibwege. Yes! Alijipambania na kuwapambania sana wasanii wake Ni ‘prinsipo’. Alimshika mkono Lady Jaydee, Q Chillah, Ray C, Stara Thomas, Bushoke, Marlaw, Mwasiti, Linnah, Amini, Barnaba, Recho, Ditto na wengine kibao. Kama Nature na wengine kibao. Huyu ni Rugemalira Mutahaba ‘Jasiri Muongoza Njia.’ Leo hii Mohammed Mchengerwa, akiwa Waziri wa Sanaa Utamaduni na Michezo, (kahamishiwa Wizara ya Maliasili na Utalii). Alikuwa na ajenda ya mikopo kwa wasanii. Hili ni wazo zuri ili kukuza sanaa na wasanii, lakini halina mashiko. Walichofanya ni kama kifuta jasho kwa wasanii kwa makubwa waliyofanya. Mkopo ni milioni 40, kakopeshwa ‘Tajiri’ Irene Uwoya, Vincent Kigosi ‘Ray’, JB na wengineo wenye ushawishi. Hii pesa walikopeshwa miaka 10 iliyopita na Steps pale Kariakoo na waliwapa ili wakaandae filamu moja tu. Leo wanakopeshwa ili kuendeleza sijui kukuza sanaa yao. Mchengerwa na kikundi chake hawakusoma mchezo ni dili lilikosa mashiko na sioni hizi pesa zitalipwaje.

Unampa Uwoya pesa ya kufanyia ‘sevisi’ gari zake hapo Nairobi? Milioni 40 siyo pesa kwa sanaa yetu. Ni pesa ambayo Mbosso hawezi kufanyia ‘shutingi’ kwa video moja tu. JB akiandaa filamu kwa pesa hiyo, haitaisha na madeni atabaki nayo. Na wao wanajua, lakini nani wa kukataa mkopo usio na riba? Hata kama ni buku tano atabeba tu, watu wametumwa pesa mjini. Kina Mafufu tamthiliya zao pale Azam hulipwa vizuri, hawana njaa hivyo. Lakini sanaa yenyewe ina njaa na changamoto nyingi. Sidhani kama Mchengerwa alikaa na wasanii na kumwambia hiyo ndio shida ya sanaa na kama walimwambia hivyo, basi ni wabinafsi na wahuni wenye tamaa ndogondogo. Hiyo pesa siyo shida ya msanii mkubwa kama Irene Uwoya.

Serikali inaanzaje kukopesha msanii mmoja mmoja? Wasanii wako wangapi? Tunavyojua Serikali kazi yake ni kutengeneza miundombinu mizuri ya kila sekta. Badala ya kukopesha pesa za ‘sevisi’ za magari, wangewekeza katika vyuo vya sanaa vingi zaidi, kulipa vizuri walimu wa sanaa na kuleta wawekezaji wakubwa kutoka nje. Kama inavyofanyika kwenye madini, michezo, kilimo, usafiri wa anga na ardhini nk.

Jakaya aliwaletea TFF, kocha Maximo na wenzake. Sanaa pia inawahitaji sana kina Maximo wao. Waje ‘kubrashi’ akili za wasanii wetu. Hakuna ‘Arena’, hatuna vijiji na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uigizaji. Wizara inageuka vikoba vya wasanii. Badala ya kurasimisha sanaa ili wasanii kupitia sanaa zao wawezeshwe kukopa pesa kwenye taasisi za kifedha. Ajabu ni kwamba hata kituo cha polisi, ukidakwa ukijitambulisha kama msanii hupati dhamana. Unaonekana muhuni tu. Hapa ndipo inapokasekana akili ya Ruge katika utawala huu, alifanya muziki uvuke kutoka mtaani hadi viunga vya Ikulu. Wasanii wakaaminika zaidi na kuheshimika na viongozi hata wananchi. Mtu alijivunia usanii baada kuvushwa kiheshima na siyo kukopeshwa pesa. Muda huu tulitaka kuona miundombinu zaidi ya kisanaa ikijengwa. Kuweka bajeti kubwa kwenye sanaa, lakini ajabu wizara husika inageuka vikoba vya wasanii. Poa siyo kesi. Ndio milioni 40? Sanaa ni biashara na inaweza kuingiza pato kubwa kwa Taifa kuliko hata madini na korosho. Sanaa hujenga uchumi wa nchi, wa msanii na mtu mmojammoja mitaani. Kama Calfornia ndio jimbo tajiri zaidi ndani ya Marekani halafu tunaambiwa uchumi wake hutokana na sanaa. Unataka nini zaidi?

Hata kamari huchezwa muda ambao sanaa inafanya kazi zaidi.