Ndoto za Sh20 milioni kwa mkali wa BSS 2023

Wengi wanashauri kuwaiga waliofanikiwa. Rai hiyo ni tofauti kwa mwimbaji wa Marekani na mshindi wa tuzo nyingi za Grammy, Beyonce Knowles ambaye katika moja ya mahojiano yake aliwahi kusema, “Anaamini mtu akifanya kazi kwa bidii, chochote anachotaka, kitatimia,”

“Niliamini ipo siku nitafanya vizuri, hivyo niliporudi kwenye shindano hili kwa mara ya pili niliona ndiyo wakati wa kutimiza ndoto zangu,”anasema Asagwile Mwasongwe ambaye ni mshindi wa shindano la kusaka vipaji vya kuimba la Bongo Star Search (BSS), MWAKA 2023 lililokuwa linajulikana kama ‘All stars Bongo star search’ kutokana na washiriki kuwa ni wale waliowahi kushiriki shindano hilo na kumaliza kwenye Top 10. Akizungumza na Mwananchi kwenye mahojiano maalumu mshindi huyo wa BSS, ambaye hivi karibuni alijinyakulia kitita cha Sh20 milioni, anasema ana matamanio mengi, lakini kubwa ni kufika mbali kimuziki.

Asagwile ambaye hupendelea kuimba nyimbo za injili, licha ya kuwa na uwezo wa kuimba aina nyingine ya muziki, anasema , “Nia yangu hasa ni kuhamasisha au kusimamia uimbaji muziki live, badala ya kutumia play back.

“Watu wengi wamenitambua kwa kupitia muziki wa live, hivyo nitawekeza nguvu huko kuhakikisha naendelea kufanya aina hii ya muziki, japo pia nitaendelea kutengeneza nyimbo nyingine studio."

Anasema anajua kuimba live kwa kizazi hiki nitaonekana ninajichelewesha sana, lakini mimi lengo langu pamoja na kupata pesa pia ni kuburudisha muziki halisi na si vinginevyo,”anasema. Anasema matamanio yake pia ni kuufikisha muziki wake kimataifa. “Ndio nina ndoto ya kufikisha wa injili anga za kimataifa, na nina imani siku moja hilo litafanikiwa,”anasema.

Anasema pia anatamani kufanya kazi na wanamuziki wakubwa wa muziki wa injili kama Christina Shusho, Rehema Simfukwe na Ambwene Mwasogwe.

“Christina Shusho ni mwimbaji ambaye ananivutia kutokana na aina yake ya uimbaji, matamshi, na jinsi anavyowasilisha ujumbe wake, ninatamani siku moja kufanya naye kazi,”anasema.

Mshindi huyo wa BSS anasema ili muziki ufike mbali unahitaji jicho la wabobezi kwenye anga hiyo, ndiyo maana anatamani kufanya kazi na watayarishaji na waongozaji wakubwa wa muziki.

“Siku nitakayofanya kazi na mwongozaji Hanscana nitafurahi sana kama ambavyo nitafurahi nikifanya na mtayarishaji wa muziki RingTong.

“Mbali na Hanscana, pia ninatamani kufanya kazi na mwongozaji Kenny na Ivan,”anasema.

Gazeti hili lilimpigia mwongozaji Hanscana kupata maoni yake kuhusu kauli ya Asagwile kutaka kufanya naye kazi. “Akiwa na pesa na madini anayotaka kuwapa mashabiki zake aje tufanye kazi ambayo ataipenda yeye na mashabiki zake,”anasema Hanscana.


Aliingiaje kwenye muziki

Anasema akiwa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Malela, alifanya kosa ambalo adhabu yake ilimfanya atamue kipaji chake cha uimbaji.

“Nikiwa kidato cha kwanza, tulikua tunapiga makelele darasani, ndipo mwalimu aitwaye Isaya, akaja na kutupatia adhabu ya kuimba ushairi, ili aweze kumpata mtu atakayeimba kwenye mahafali ya kidato cha nne.

“Kwa bahati mbaya wakati ule, nzuri wakati huu nilikuwa wa mwanzo mwanzo kutumikia adhabu hiyo.

“Niliimba lile shairi kwa ustadi mkubwa na kuliwekea manjonjo kiasi cha wanafunzi wenzangu na mwalimu kunipongeza na kuelewa nilichokifanya,”anasema nyota huyo aliyewahi kushika namba tisa katika shindano hilo mwaka 2018.

Anasema baada ya tukio hilo, alianza kuwa na ndoto ya uimbaji.

“Nilianza kwa kuimba miondoko ya Hip Hop, lakini nilikuwa nikipata maoni kwa watu waliokuwa wakinisikia kuwa siwezi, nikaamua nigeukie muziki wa injili.

“Kabla ya kujikita katika muziki wa injili nilikua nahisi nafsi yangu inanisukuma kufanya muziki wa aina hiyo, nashukuru Mungu naendelea vyema,”anasema.

Asagwile anasema amepata uzoefu mkubwa katika mashindano ya BSS mwaka huu, ikiwamo kujifunza kukaa na watu wa aina mbalimbali, kuwa na tabia njema na akiwa mbele za watu afanye nini.

“Kila mtu ana tabia yake kama mnavyojua ila ninashukuru Mungu mambo yalienda poa hata baadhi ya changamoto nilizokumbana nazo nilikua ninazitatua.

“Biblia inasema imani ni kuwa na uhakika hivyo nilikua ninaaamini nitafika mbali,”anasema.

Akizungumzia mashindano hayo Asagwile anasema kuwa majaji ni kiungo kikubwa kwani wamekuwa wakihukumu kwa haki bila ya upendeleo wowote.

“Kwa kweli majaji walikua wakitoa maoni ya kweli na ya haki, kama umekosea wanakueleza umekosea na kama umefanya vizuri pia wanakueleza,” anasema.

Kuhusu vijana wanaofanya muziki wa dunia na injili. Asagwile aliwakumbusha kumtukuza Mungu popote walipo kwa sababu bila yeye mambo hayaendi sawa.

“Kila mmoja kwa imani yake, bila kujali anafanya muziki wa dunia au wa injili ilimradi anatafuta riziki, na amtukuze Mungu kwa ajili ya mustakabali na mawanda mapana ya muziki,”anasema Asagwile.

Anasema hatoacha kumtukuza Mungu kwa sababu ameuona ukuu wake.