Oya! watu wangu wa Sinza futari 'hainaga' swaga
Muktasari:
- Sinza ile ya wajanja ilikuwa kila baada ya nyumba bar. Sasa hivi kila baada ya hatua moja duka la nguo. Fremu ni nyingi kama Narung’ombe na Tandamti. Sinza imekuwa yoyote kwa sasa. Haina ‘testi’ ya ‘Usinza wa Kiabajalo’, ‘Usinza Staa’ na ‘Usinza’ wa Kimawela.
Nimetumia wiki yote iliyopita kufuturu mitaa ya Sinza. Kule nina familia, washikaji na kumbukizi nyingi za nyakati za balehe. Sinza imebadilika, na watu wake wamebadilika. Siyo Sinza ile tena. Nyakati za Sinza kwa wajanja, zimelala na Banza Stone pale Sinza Makaburini.
Sinza ile ya wajanja ilikuwa kila baada ya nyumba bar. Sasa hivi kila baada ya hatua moja duka la nguo. Fremu ni nyingi kama Narung’ombe na Tandamti. Sinza imekuwa yoyote kwa sasa. Haina ‘testi’ ya ‘Usinza wa Kiabajalo’, ‘Usinza Staa’ na ‘Usinza’ wa Kimawela.
Usinza wa sasa shalo. Awamu ya Jakaya, ‘gesti’ zote Sinza zilitekwa na ‘Riali Madridi’. Zile pisi kali za Kitanga ambazo kwa makusudi zilivamia Dar kutafuta maisha kwa kuuza miili. Sinza ilipambwa na maua haswa. Asubuhi ungeamka ungekutana na toto bichi flani, kanga moko lipo dukani kwa Mangi.
Unakutana na pisi asubuhi. Unapiga hatua mbili mbele na hatua tano nyuma kuitazama tena upya. Unajiridhisha kwa macho, figo, bandama, mapafu na kongosho kuwa pisi ya maana. Unawaza kuiposa kabisa na siyo kulewa nayo tu. Lakini ukirudi jioni unakutana nayo iko na wenzake tayari kwa jukumu zito la usiku.
Mtaani anakuita kaka, usiku viwanja pesa zako anazitaka na hakuiti tena kaka. Sinza ilikuwa ni ukanda wa ‘vicheche’ wenye viwango vya juu vya ubora wa ngozi. Kulikuwa na ‘klasi’ tofauti ya Sinza na maeneo mengine kama Kinondoni, Buguruni, Tabata, Mbezi, Kimara, Ubungo, Keko na kwingineko.
Hata bei za Sinza zilikuwa zimechangamka sana. Pesa ambayo ungetumia kwa kicheche wa Sinza. Ungeweza kutumia kwa vicheche vitano vya Kinondoni. 10 vya Buguruni, Keko ama Magomeni. Mitaa mingi ungekutana na vicheche vyenye majina ya Amina, Ashura, Sikujua nk. Sinza ilikuwa tofauti.
Sinza ndiko alikosema Mwana Fa kwamba Amina amekuwa Mayna, Naima, Clara na Rayyah. Kuna Tayana hata Bongo kuna Aaliyah, Candy, Nicole, Uenice au labda Mariah. Sikitu hataki jina na Asia anajiita Ayshier. Hizi mbanga za mademu sampuli hii ungekutana nazo mitaa ya Sinza tu.
Kwa mabwege wengi ambao hamjui kitu. Sinza ilikuwa zaidi ya vitongoji vyote Daslama mjini. Bata la kweli lilipatikana Sinza. Kuna wanetu kibao ambao walistahili kuwa matajiri hii leo. Lakini utajiri wao ulitoweka kwa sababu ya eneo ambalo liko katikati ya Shekilango ya Ubungo na Bamaga Mwenge (Sinza).
Ungeweza kutokea mkoani na milioni 10. Ukishuka kwenye basi pale Ubungo, ukachukua taksi ambayo ingekupitisha pale Shekilango na kukuingiza njia ya kushoto kuelekea Sinza. Kesho yake ungerudi na njia ileile kurudi kwenu mkoani ukiwa na nauli tu. Na maajabu ya Sinza bana, ungerudi kwenu bila kujutia.
Sinza ilikuwa watu wanatumia pesa mpaka wanafurahia yale matumizi makubwa waliyotumia. Sinza ungepata chochote unachotaka ukiwa na mzigo wa kutosha. Bar za mitaa ya Sinza zimekata mitama sana akaunti za masela wetu. Sinza kulikuwa na ‘jini tumizi’, ‘jini shawishi’ na ‘jini furahia’.
Sinza ungeweza kutumia pesa yote mpaka ya pango la nyumba. Halafu badala ya kujuta, wewe ungechekelea na kukenua meno kama zuzu, ukiwasimulia washikaji zako jinsi ulivyotapanya pesa usiku wa jana yake. Na washikaji zako badala ya kukuonea huruma na kusikitika, wangekuonea wivu kwa bata ulilokula.
Kuna dogo alipata pesa baada ya kuuzwa kwa nyumba yao ya urithi. Yeye kama yeye alipewa milioni 150. Akajichimbia kitaa cha Sinza Sinzani, Sinza ile ya Mitungi, Mikasi Blanti ya Ngwea. Sinza ya Latifah wa MB Dog, Sinza ya Wife wa Daz Baba na Barua ya Bushoke. Sinza kama Sinza.
Baada ya mwezi dogo akawa mhudumu wa mapokezi kwenye hoteli ileile aliyojichimbia mitaa ya Sinza. Aliishiwa pesa zote akawa hana sehemu ya kwenda. Ndugu zake walishagawana pesa kila mtu chake. Ndani ya mwezi mmoja utawaambia nini? Umeibiwa? Umetapeliwa?
Dogo akawa ‘risepshenisti’ bila kupenda. Na waliochangia kutoweka kwa pesa zake za urithi, wakawa wanakuja na mabwana wengine hotelini palepale na yeye ndiye aliwahudumia. Yaani mwezi uliopita alikuwa tajiri. Mwezi unaofuata kageuka stafu wa ‘hoteli’ aliyotumia enzi za utajiri wake. Hiyo ndiyo Sinza.
Kuna wakati huwa nashangaa wasanii wa Bongo Movie kukosa stori tamu. Ambazo zingesadia filamu zao kuuza sana tena kimataifa. Sinza pekee mikasa yake inaweza kukutengenezea stori za movie kibao. Kuna matukio mengi ya watoto wa mjini kwenye mitaa yetu, ambayo ni filamu tosha badala ya masikini kumpenda tajiri.
Lakini Sinza ya sasa siyo ile. Sinza ya sasa ina vijana wengi lakini ni vijana wanaokuja asubuhi na kuondoka jioni. Wengi ni vijana walioajiriwa kuuza maduka yaliyojazana Sinza. Hakuna tena ile ‘testi’ ya Usinza. Kuna mchanganyiko wa bangi na gongo. Kila mtu mgeni na kila kitu kigeni.
Unakutana na mshikaji mitaa ya Sinza Mori, ukipiga stori za mitaa ya Lion Hotel hakuelewi. Kumbe ni mtaa wa nyuma palepale alipo. Kifupi wanetu wa ‘Displini’ Mapambano, Suwa Side na ‘Vaibresheni’ Kwa Remmy, wengi wako Mtoni na waliobaki wamehamia Kinzudi, Goba ama Kinyerezi huko.
Achana na yote hayo. Kilichonikera ni kuona hata futari ya Sinza ya sasa ni ya ovyo kinoma. Usione uzuri wa migahawa iliyojazana Sinza ya sasa. Mwezi huu Mtukufu tafuta maeneo ya kwenda kupata futari nzuri lakini siyo Sinza. Labda kama unaenda nyumbani kwa mtu na siyo kwenye migahawa yao ile.
Unakunywa uji utadhani ‘eneji drinki’. Unakula magimbi yamejazwa karoti na viungo vingi utadhani pilau. Hata wahudumu wengi wao hawajui hata utamaduni wa Pwani. Wanahudumia utadhani mkesha wa mwenge. Hawana swaga, vichwa wazi vimini vingi. Yaani hawajui ‘testi’ ya mwezi huu inataka nini.
Nadhani wamiliki wengi wa migahawa ya Sinza, ni wageni na wanaokoteza wahudumu. Ambao wanatoka katika maeneo ambayo hawajui lolote la Upwani na ufahamu wa mwezi mtukufu hawana. Ndo maana futari kama mchemsho. Magimbi, ndizi, vizi unachanganya na makaroti kweli?
Unaulizia njugu mawe hakuna. Maharagwe hakuna. Chapati za maji hakuna. Uji wenyewe kama wa ‘bodingi skuli’ na zaidi una ladha kama ‘eneji drinki’. Nawashitua wanangu wa nguvu kwamba tafuteni machaka yenye ‘testi’ ya mwezi huu lakini siyo Sinza. Kule Sinza wabaki na starehe za bata batani tu .