RTD ina mchango mkubwa katika kulinda na kuendeleza utamaduni wa TZ
Muktasari:
- Broadcasting Station, wenyeji waliita Redio Dar es Salaam.Kituo hicho kilianza kwa kurusha vipindi vya Kiingereza na kukawa na kipindi kimoja tu cha Kiswahili katika wiki, baada ya kuonekana kinapendwa, kipindi hicho kikaanza kurudiwa mara mbili kwa wiki.
Mwaka 1951 afisa mmoja wa BBC alipendekeza kuanzishwa kwa kituo cha redio katika koloni la Uingereza la Tanganyika. Ili kupata ujuzi wa kutengeneza vipindi kwa ajili ya wenyeji wa nchi hii, serikali ya Uingereza ikatoa kiasi cha dola 30,000 na fedha hizo zikawezesha kuanzishwa kwa kituo kidogo cha redio kilichoitwa Dar es Salaam
Broadcasting Station, wenyeji waliita Redio Dar es Salaam.
Kituo hicho kilianza kwa kurusha vipindi vya Kiingereza na kukawa na kipindi kimoja tu cha Kiswahili katika wiki, baada ya kuonekana kinapendwa, kipindi hicho kikaanza kurudiwa mara mbili kwa wiki.
Kutokana na uhafifu wa mitambo, ilikuwa vigumu kusikia matangazo ya kituo hiki cha redio nje ya mji wa Dar es salaam. Taratibu vipindi vya Kiswahili vikaongezeka na mitambo nayo ikaboreshwa na vipindi vikaweza kusikika kwa umbali zaidi hatimae jina pia likabadilishwa na kituo hicho kikaanza kuitwa Tanganyika Broadcasting Corporation (TBC).
Kufikia 1954 pamoja na mapungufu mengi ya vifaa, radio ilikuwa na wataalamu wote wenyeji, wataalamu ambao walikuja kuwa na mafanikio sambamba na nchi nyingine nyingi zilizokuwa ni koloni za Uingereza.
Mwaka 1961 bila kumwaga damu Tanganyika ikapata Uhuru chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere na chama chake cha TANU. Serikali mpya ikaona redio ni kiungo muhimu cha kuunganisha wananchi na mipango ya serikali yao, lakini chombo hicho kilikuwa bado ni chombo binafsi hivyo mara nyingine kutokuwa na msimamo ulioafikiana na ule wa serikali.
Mwaka 1965, Serikali ya Tanzania iliitaifisha kituo cha redio cha Tanganyika Broadcasting Corporation(TBC) na kukibadili jina na kukiita Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD), na kituo hicho kikawa chombo cha kuelimisha sera mipango na taratibu mbalimbali za serikali, na kusindikizwa na burudani.
Radio ikawa chombo kimoja kilichoweza kuunganisha watu wa nchi hii ambao walitokana na makabila zaidi ya 120, RTD hakika haiwezi kukwepeka kuwa nayo ilikuwa nyenzo kubwa ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya Taifa. Nchi nyingine nyingi za Kiafrika ziliona suluhisho la kupata lugha ya Taifa ilikuwa ni kuchukua lugha ya wakoloni waliowatawala, na redio zao za Taifa zilikuwa ndio nyenzo kubwa ya kueneza lugha hizo za kurithi.
Mpaka leo tuna nchi nyingi za Kiafrika ambazo lugha zao za Taifa ni Kireno, Kifaransa au Kiingereza.
Lakini tukumbuke kuwa wakati wa kupata Uhuru nchi nzima kulikuwa na watu wachache wenye radio, inasekemekana wakati tunapata uhuru kulikuweko na redio zisizozidi 100,000 nchi nzima, na nyingi zilikuwa Dar es Salaam kwa vile hata matangazo yenyewe hayakuweza kusikika mbali.
Hata kufikia mwishoni mwa miaka ya 60 ni chini ya asilimia 30 ya wananchi walikuwa na uwezo wa kusikiliza RTD kila siku, ndipo serikali ikasambaza redio mashuleni na hata vijiji vingi vilipewa redio na kukawepo mahala pa kusikilizia redio, japo redio hizo zilitumika zaidi katika vipindi vya ‘kuhamasisha maendeleo’ na hotuba mbalimbali za viongozi wakitoa maagizo mbalimbali, na zile redio zilizosambazwa mashuleni zilikuwa haswa ni kwa ajili ya kufwatilia vipindi vya masomo ya shule vilivyokuwa vikirushwa na RTD.
Kiwanda cha kutengeneza redio za bei rahisi kikaanzishwa Dar es Salaam. Kiwanda hiki kiliweza kutengeneza redio maarufu kama National Panasonic 177, iliyopewa jina ‘redio ya mkulima’, ilikuwa ya bei rahisi na ilienea karibu kila kona ya nchi mijini na vijijini.
Ili redio isikilizwe, vipindi vya burudani na muziki ni muhimu, umuhimu wa kuwa na muziki wa nyumbani ulionekana wazi, ilifika hatua mpaka Bunge la Tanzania wakati huo likaingia katika mjadala wa kupiga marufuku muziki kutoka nje.
Hili bahati nzuri halikutimia japo RTD ilielekezwa kuwa katika vipindi vyake vya muziki , ule wa kutoka nje usizidi asilimia 30 ya muziki wote utakaopigwa na kituo hicho.
Ili kuweza kujaza asilimia 70 hiyo RTD ilifanya kazi kubwa ya kurekodi muziki wa aina mbalimbali kutoka kila kona hapa nchini, na hili limeifanya mpaka leo RTD sasa TBC, kuwa wameweza kuwa na maktaba kubwa sana ya muziki wa Tanzania wenye historia ya nchi yetu na watu wake na siasa zake na ndoto na mafanikio yake. Bila ubishi wowote RTD ilitoa mchango mkubwa katika kuhifadhi na kukuza utamaduni wa Tanzania na hasa muziki wa Tanzania.