Tamasha la utamaduni, utalii la kimataifa lazinduliwa Bariadi

Mkuu wa Wilaya ya Itilima Anna Gidarya (katikati) akizindua tamasha la kimataifa la utamaduni na utalii lililoandaliwa na Kampuni ya  Kilimanjaro One Travel and Tours. Kutoka kulia ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo, Christina Emmanuel, mkurugenzi wa kampuni hiyo Mohamed Hatibu, Ofisa Maendeleo ya Vijana, Zena Mchujuko na Ofisa wa Baraza la Sanaa la Taifa, Gabriel Awe

Muktasari:

 Imeelezwa kuwa, utamaduni ni jambo kubwa la kujivunia, ni lazima uenziwe na kuendelezwa

Simiyu.  Tamasha la kimataifa la utamaduni na utalii limezinduliwa wilayani Bariadi mkoani Simiyu, huku wananchi wakihamasishwa kuendeleza utamaduni uliopo.

 Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Anna Gidarya amezindua tamasha hilo jana Jumamosi Machi 16 2024 akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,  Dk Yahaya Nawanda, huku wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa Serikali wakihudhuria.

Gidarya  ameipongeza aliipongeza Kampuni ya Kilimanjaro One Travel and Tours kwa kubuni tamasha hilo na na kuamua lifanyike Mkoa  wa Simiyu.

Amesema utamaduni ni jambo kubwa la kujivunia, ni lazima uenziwe na kuendelezwa kwa nguvu zote kwa sababu ni “urithi tuliopokea kutoka kwa babu zetu, hivyo  na sisi hatuna budi kuuendeleza.”

Amesema tamasha hilo litasaidia kutangaza utamaduni wa Simiyu kupitia shughuli zitakazofanyika, hivyo kuufanya mkoa ufahamike zaidi ndani na nje ya nchi.

“Nimearifiwa kuwa leo ni uzinduzi tu, ili tupate kionjo cha kinachotarajiwa kufanyika mwezi wa saba 2024 kwamba, kutakuwa na tamasha kubwa la siku tatu mfulululizo  na litahusisha watu zaidi ya 7,000 wakiwamo washiriki wa maonyesho,” amesema Gidarya.

“Hii ni hatua kubwa na ni fursa kwa washiriki kufanya biashara na kujifunza mambo mbalimbali wakati wa tamasha, 

hivyo, sekta ya utalii wa utamaduni itakuwa kwa sababu wageni wote watakaokuja  watapata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya mkoa wetu na kujionea vivutio.”

Pia, amewapongeza waandaaji kwa kuunga mkono  juhudi za Serikali za kuhakikisha utamaduni unatangazwa na kuufanya kivutio kikubwa cha watalii wa ndani na nje ya nchi.

“Napenda kutoa wito kwa wadau mbalimbali, wakiwamo watu binafsi, mashirika, taasisi na kampuni kujitokeza kudhamini tamasha hili kubwa katika kanda ya ziwa na nchini kwa jumla ili lifanyike kwa ukubwa unaostahili na kukuza utamaduni na utalii wetu hapa nchini,” amesema Gidarya.

 Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na waandaaji wa tamasha hilo kuhakikisha linafanyika kila mwaka na kuwa chachu ya maendeleo kiutamaduni na kiuchumi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kilimanjaro One Travel and Tours Christina Emmanuel amesema hiyo ni mara ya kwanza kwa kampuni hiyo  inayojihusisha na masuala ya utalii na utamaduni kuandaa tamasha wanalotarajia kuwa na muitikio mkubwa kwa wakazi wa Simiyu na mikoa ya jirani. 

“Tamasha hili linatarajiwa kufanyika mwezi wa saba na ninayo furaha kukufahamisha kuwa litafanyika kwa siku tatu mfulululizo Julai 5, 6 na kilele chake kitakuwa Julai 7, tunategemea kuwa na maonyesho mbalimbali ya masuala ya utamaduni na utalii katika Uwanja wa Halmashauri na kuwavutia washiriki na watazamaji zaidi ya 7000 kwa siku hizi tatu.

 Pia, litakuwa na vionjo mbalimbali ikiwamo ngoma inayohusisha makabila ya Wagika na Wagulu,” amesema Emmanuel.

Ametoa wito kwa wafanyabiashara, kampuni, taasisi na mashirika kujitokeza na kuunga mkono kama njia moja wapo pia ya kuiunga mkono Serikali katika kuutangaza utamaduni na utalii wa nchi yetu.

Ofisa wa Baraza la Sanaa nchini (Basata) Gabriel Awe amewasifu waandaaji kwa kuandaa tamasha hilo katika kuendeleza utamaduni na utalii hapa nchini, akitoa wito kwa wadau wengine kuliunga mkono tamasha hilo kwa hali na mali.

“Ni tamasha kubwa la aina yake ambalo sisi kama Watanzania tunapaswa kujivunia kuwa hili ni tamasha la kwetu kwa maendeleo ya utamaduni na utalii wetu,”amesema Awe.

“Hivyo ni vema wadau wakajitokeza na kuhakikisha linakuwa tamasha kubwa zaidi na kuvutia watu kutoka mataifa ya nje kujua thamani ya utamaduni na utalii wetu hapa nchini.”